Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake
01-Umuhimu Na Baadhi Ya Fadhila Zake
Alhidaaya.com [4]
Kutoa salaam ni funzo muhimu tulilofundishwa na kuamrishwa katika Dini yetu, lakini tunaona kwamba limechukuliwa kuwa ni jambo jepesi lisilotiliwa hima na ilhali lina fadhila nyingi na kubwa sana, mojawapo ni kumuingiza mtu Peponi kwa dalili Hadiyth ifuatayo:
عن أبـي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((لا تَدْخُـلُوا الـجَنَّةَ حتـى تُؤمِنُوا، ولا تُؤمِنُوا حتـى تَـحابُّوا أوَلا أدُلُّكُمْ علـى شَيءٍ إذا فَعَلْتُـمُوهُ تَـحَابَبْتُـمْ؟ افْشُوا السّلامَ بَـيْنَكُمْ)). صحيح مسلـم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hamtoingia Jannah hadi muamini, na wala hamuwezi kuamini hadi mpendane. Je, nikujulisheni jambo ambalo mtakapolifanya mtapendana? Toleaneni Salaam baina yenu)) [Muslim]
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, mafunzo ya maamkizi ya salaam yalikuwa ni katika mafunzo ya mwanzo kabisa kuwapa Maswahaba alipoyatoa katika khutba zake za mwanzo huko aliposema:
((ايها الناس ،أفشوا السلام، وأطعموا الطعام، وصلّوا بالليل والناس نيام تدخلوا الجنة بسلام)) رواه الترمذي، حديث صحيح
((Enyi watu, enezi (amkianeni kwa) salaam, na lisheni chakula, na Swalini watu wakiwa wamelal (Tahajjud), mtaingia Jannah kwa amani)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Swahiyh]
Waislamu wanapokutana au kuwasiliana kwa njia yoyote inawapasa kusalimiana kwa maamkizi ya Kiislamu kama tulivyoamrishwa; yaani kusema: "Assalaamu 'Alaykum." Haya ndio maamkizi ya Kiislamu yanayopaswa kuanziwa katika kuamkiana. Lakini aghlabu wa wasiojua umuhimu wake huanzia kwa kauli kama: "Hujambo? "Habari gani?" "Hali?" "Vipi mzima?" "Habari za asubuhi" au 'Swabaahal-khayr" "Ahlan" "Marhaba".
Maamkizi haya ya Kislamu hayapasi kufupishwa hata katika maandishi, mfano ambayo yanafupishwa katika mawasiliano ya kimaandishi ni: A.A, au A.A.W, au A.A.W.W.B.
Hakika kufupisha maamkizi ya Kiislamu ni kukosa fadhila zake kubwa. Kuandikia kikamilifu haimchukui mtu hata dakika moja. Inavyopaswa ni kuandika: 'Assalaamu 'Alaykum' au Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh'.
Tunatumai kwamba baada ya kuzijua fadhila zake katika Makala hizi Waislamu tutaweza kuthamini maamkizi ya Kiislamu kama yalivyokuja katika Shariy’ah.
Zifuatazo ni Aayah na Hadiyth zenye amri na mafunzo muhimu ya maamkizi ya Kiislamu:
Tunapoingia majumbani mwa wenzetu tunatakiwa tuanze kusalimia kwa maamkizi ya Kiislamu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾
Enyi walioamini! Msiingie nyumba zisizokuwa nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salamu wenyewe. Hivyo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka. [An-Nuur: 27]
Tuna mifano kutoka kwa Malaika pindi Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alipoingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiweko Mama wa Waumini: kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
عن عائشة رضي الله عنه قالت: قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((هذا جبريل يقرأ عليك السلام)) قالت: قلت: "وعليه السلام ورحمة الله وبركاته" متفق عليه
Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Huyu Jibriyl anakutolea salaam)) Nikamjibu: "Wa ‘Alayhis-Salaam wa RahmatuLLaahi Wa Barakaatuh" [Al-Bukhaariy na Muslim]
Pia kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu Malaika walipopita nyumbani kwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) kuelekea mji wa Nabiy Luutw (‘Alayhis-Salaam) kuuangamiza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ﴿٢٤﴾
Je, imekufikia hadithi ya wageni wahishimiwao wa Ibraahiym?
إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٢٥﴾
Walipoingia kwake wakasema: “Salaam! Akasema: “Salaam watu wasiotambulikana.” [Adh-Dhaariyaat: 24-25]
Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake
02-Kuwajibika Kwake
Alhidaaya.com [4]
Maamkizi ya Kiislamu yamewajibika kwetu kutokana na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa dalili zifuatazo:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا ۚ فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾
Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa, na wala nyinyi wenyewe kama mtakula majumbani mwenu, au majumbani mwa baba zenu, au majumbani mwa mama zenu, au majumbani mwa kaka zenu, au majumbani mwa dada zenu, au majumbani mwa ‘ammi zenu, au majumbani mwa shangazi zenu, au majumbani za wajomba wenu, au majumbani mwa makhalati zenu au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Hakuna ubaya kama mkila pamoja au mbali mbali. Mtakapoingia majumbani toleaneni salaam; maamkizi kutoka kwa Allaah, yenye Baraka, mazuri. Hivyo ndivyo Anavyokubainishieni Allaah Aayaat ili mpate kutia akilini. [An-Nuwr: 61]
Aayah tukufu hiyo inaashiria jinsi maamkizi ya Kiislamu yalivyokuwa na umuhimu mkubwa hadi kwamba tunapoingia majumbani mwa wenzetu au hata majumbani mwetu na ikawa hakuna mtu tunapaswa kusalimia kwani kufanya hivyo ni kujitakia kheri na Baraka kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Pia Hadiyth zifuatazo za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن أنس رضي الله عنه قال: قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((يا بُني، إذا دخلت على أهلك، فسلم، يكن بركة عليك، وعلى أهل بيتك))" ((رواه الترمذي وقال: حديث حسن صحيح)).
Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ee mwanangu! Unapoingia nyumbani mwako toa salaam itakuwa Baraka kwako na kwa watu wa nyumbani mwako)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh]
Jambo la mwanzo alilofunzwa Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam) baada ya kuumbwa lilikuwa ni maamkizi ya Kiislamu kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
عن أبـي هريرة رضي الله عنه عن النبـي صلى الله عليه وسلم قال: «خَـلَقَ اللَّهُ عَزَّ وجَلَّ آدَمَ علـى صُورَتِهِ طُولهُ سِتُّونَ ذِراعاً، فَلَـمَّا خَـلَقَهُ قال: اذْهَبْ فسَلِّـمْ علـى أولئِكَ: نَفَرٍ مِنَ الـمَلائِكَةِ جُلُوسٍ فـاسْتَـمعْ ما يُحَيُّونَكَ فإنَّها تَـحِيَّتُكَ وتـحِيَّةُ ذُرِّيَّتِكَ، فقال: السَّلامُ عَلَـيْكُمْ، فقالوا: السَّلامُ عَلَـيْكَ وَرَحْمَةُ اللَّهِ فَزَادُوهُ: وَرَحمَةُ اللَّهِ )) البخاري و مسلم
Kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Amemuumba Aadam ('Alayhis Salaam) katika umbo Lake, akiwa urefu wa dhiraa sitini. Alipomaliza kumuumba, alimwambia: Nenda ukawaamkie kundi la Malaika waliokaa na Usikilize watakavyokuamkia, kwani hayo ndio yatakavyokuwa maamkizi yako na ya kizazi chako. Akasema (Aadam): "Assalaamu 'Alaykum". Wakajibu: "Assalamu 'Alayka wa RahmatuLLaah." Wakazidisha: 'Wa RahmatuLLaah')) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Pia maamkizi ya Kiislamu ni haki ya Muislamu kwa Muislamu mwenzake kurudisha maamkizi hayo. Kwa maana mtu anapoanza kukuamkia kwa maamkizi ya Kiislamu inakupasa nawe urudishe kumuamkia la sivyo itakuwa hukumtizimia haki yake:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صبى الله عليه وسلم قال: ((حق المسلم على المسلم خمس رد السلام وعيادة المريض واتباع الجنائز وإجابة الدعوة وتشميت العاطس)) متفق عليه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Haki ya Muislamu kwa Muislamu ni mambo matano; kurudisha salaam, kumtembelea mgonjwa, kusindikiza jeneza, kuitikia mwaliko, na kumuombea Rahma mwenye kupiga chafya)). [Al-Bukhaariy na Muslim].
Juu ya hivyo mwenye kuamkiwa inampasa arudishe maakimizi ambayo ni bora zaidi kuliko ya yule aliyemuamkia. Tutazame namna gani tunatakiwa kurudisha maamkizi ya Kiislam:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾
Na mtapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima ni Mwenye kuhesabu kila kitu. [An-Nisaa: 86]
Ina maana kwamba ikiwa mtu atakuamkia kwa kusema: "Assalaamu 'Alaykum" basi ni vizuri wewe kuitikia: "Wa 'Alaykumus Salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh". Hata ukijibu "Wa 'Alaykumus Salaam" pia inatosha ila ya mwanzo ni bora zaidi kutokana na mafunzo ya Allaah tuliyoyapata katika Aayah hiyo.
Na pia kila unapozidisha kuongeza maamkizi ya salaam, basi thawabu zinazidi zinazidi kwa dalili:
عن عمران بن حصين رضي الله عنهما قال :جاء رجل الى النبي صلى الله عليه وسلم فقال: "السلام عليكم" فرد عليه السلام ثمجلس فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((عشر)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله" فرد عليه فجلس فقال: ((عشرون)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله وبركاته" فرد عليه فقال ((ثلاثون)) رواه ابو داود والترمذي و قال حديث حسن
'Imraan bin Al-Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesimulia: "Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum.” Akamrudishia (Salaam) kisha yule mtu akaketi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kumi)) [Kwa maana amepata thawabu kumi]. Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaah." Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Nabiy akasema: ((Ishirini)). Kisha akaja mtu mwingine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh." Naye akamrudishia kisha akasema ((Thelathini)) [Imesimuliwa na Abu Daawuwd na At-Trimidhiy na akasema Hadiyth Hasan].
Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake
03-Maamkizi Ya Peponi
Alhidaaya.com [4]
Maamkizi ya Kiislamu yatakayokuwa maamkizi ya Peponi kwa dalili zifuatazo: Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾
Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi.
هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾
Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea.
لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾
Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba.
سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾
“Salaamun!” Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye kurehemu. [Yaasiyn: 55-58]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pindi Waumini wakishaingizwa Peponi watapokelewa na Walinzi wake wakitoa maamkizi ya Kiislamu:
وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴿٧٣﴾
Na wataendeshwa wale waliomcha Rabb wao kuelekea Jannah makundi-makundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake, na watasema walinzi wake: “Salaamun ‘Alaykum! Amani iwe juu yenu furahini na iingieni ni wenye kudumu.” [Az-Zumar: 73]
Vile vile Malaika watakapoingia kupitia milangoni ya Peponi kwa waja wema maamkizi ni hayo hayo ya Salaamun 'Alaykum:
الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ ﴿٢٠﴾
Ambao wanatimiza ahadi ya Allaah, na wala hawavunji fungamano
وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾
Na ambao wanaunga yale Aliyoamrisha Allaah kuungwa na wanamkhofu Rabb wao, na wanakhofu hesabu mbaya
وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾
Na ambao wamesubiri kutaka Wajihi wa Rabb wao, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa katika yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri, na wanaepusha ovu kwa zuri, hao watapata hatima njema ya makazi ya Aakhirah.
جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾
Jannaat za kudumu milele wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao. Na Malaika wanawaingilia katika kila milango.
سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾
“Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu) kwa yale mliyosubiri.” Basi uzuri ulioje hatima njema ya makazi ya Aakhirah. [Ar-Ra'ad: 20-24]
Pia uhai na mwisho wa mwana Aadm umegusia maamkizi haya matukufu. Malaika wanapowatoa roho waja wema huwatoa huku wakiwapa maamkizi haya ya Assalaamu 'Alaykum:
الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ طَيِّبِينَ ۙ يَقُولُونَ سَلَامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٣٢﴾
Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema watasema: “Salaamun ‘Alaykum, (amani iwe juu yenu) ingieni Jannah kwa yale mliyokuwa mkitenda.” [An-Nahl: 32]
Hata Manabii katika uhai wao wa mwanzo na mwisho yamethibiti maamkizi ya Kiislamu kama Nabiy Yahyaa ('Alayhis-Salaam) alipoambiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا يَحْيَىٰ خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ ۖ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا ﴿١٢﴾
“Ee Yahyaa! Chukua Kitabu kwa nguvu.” Na Tukampa hikma angali mtoto.
وَحَنَانًا مِّن لَّدُنَّا وَزَكَاةً ۖ وَكَانَ تَقِيًّا ﴿١٣﴾
Na mwenye upole na huruma kutoka Kwetu, na mwenye utakaso, na akawa mwenye taqwa.
وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُن جَبَّارًا عَصِيًّا ﴿١٤﴾
Na mtiifu mno kwa wazazi wake wawili, na wala hakuwa jabari wala asi.
وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا ﴿١٥﴾
Na (Salaamun ‘alayhi) amani iwe juu yake siku aliyozaliwa, na siku atakayokufa na siku atakayofufuliwa hai. [Maryam: 12-15].
Nabiy 'Iysaa ('Alyahis-Saalam) alipozungumza akiwa mtoto mchanga:
قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾
(Mtoto) Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah; Amenipa Kitabu (Injiyl) na Amenijaalia kuwa Nabiy.”
وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾
“Na Amenijaalia kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko, na Ameniusia Swalaah na Zakaah madamu niko hai.”
وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾
“Na niwe mtiifu kwa mama yangu na wala Hakunijaalia kuwa jabari, muovu.”
وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا ﴿٣٣﴾
“Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa hai.” [Maryam: 30-33]
Waja wengine ambao watakaokuwa baina ya Jannah na Moto kwa sababu amali zao zitakuwa sawa sawa katika mizani zitakapopimwa. Hawatokuweko Motoni wala Peponi, bali watakuwa katika mnyanyuko. Hapo watazungzuma na watu wa Peponi na maamkizi yao yatakuwa ni ya Kiislamu:
وَبَيْنَهُمَا حِجَابٌ ۚ وَعَلَى الْأَعْرَافِ رِجَالٌ يَعْرِفُونَ كُلًّا بِسِيمَاهُمْ ۚ وَنَادَوْا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ أَن سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۚ لَمْ يَدْخُلُوهَا وَهُمْ يَطْمَعُونَ ﴿٤٦﴾
Na baina yao ni kizuizi. Na kwenye Al-A’raaf (ukuta wa mwinuko) patakuweko watu wanaowatambua wote kwa alama zao. Na watawaita watu wa Jannah: “Salaamun ‘Alaykum!” Hawakuingia humo lakini huku wao wanatumaini. [Al-A'raaf: 46]
Ni Ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa wakaazi wa Peponi watapata kila aina ya mazuri na wanachokitamani na katika sifa mojawapo ya Jannah ni kwamba hakuna watakalosikia baya ila maneno mema tu kama hayo maamkizi ya kiislamu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾
Na waliotangulia mbele, watatangulia mbele.
أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾
Hao ndio watakaokurubishwa.
فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿١٢﴾
Katika Jannaat za taanisi.
ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾
Kundi kubwa katika wa awali.
وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿١٤﴾
Na wachache katika wa mwishoni.
عَلَىٰ سُرُرٍ مَّوْضُونَةٍ ﴿١٥﴾
(Watakuwa) Juu ya makochi ya fakhari yaliyotariziwa na kutonewa vito vya thamani kwa ustadi wa hali ya juu.
مُّتَّكِئِينَ عَلَيْهَا مُتَقَابِلِينَ ﴿١٦﴾
Wakiegemea juu yake wakikabiliana.
يَطُوفُ عَلَيْهِمْ وِلْدَانٌ مُّخَلَّدُونَ ﴿١٧﴾
Watazungukiwa na vijana wenye kudumu.
بِأَكْوَابٍ وَأَبَارِيقَ وَكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ ﴿١٨﴾
Kwa bilauri na mabirika na vikombe vya mvinyo kutoka chemchemu inayobubujika.
لَّا يُصَدَّعُونَ عَنْهَا وَلَا يُنزِفُونَ ﴿١٩﴾
Hawatoumizwa vichwa kwavyo na wala hawatoleweshwa.
وَفَاكِهَةٍ مِّمَّا يَتَخَيَّرُونَ ﴿٢٠﴾
Na matunda watakayopendelea.
وَلَحْمِ طَيْرٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢١﴾
Na nyama za ndege katika watakazozitamani.
وَحُورٌ عِينٌ ﴿٢٢﴾
Na mahuwr, wanawake wazuri wa Jannah wenye macho ya kupendeza.
كَأَمْثَالِ اللُّؤْلُؤِ الْمَكْنُونِ ﴿٢٣﴾
Kama mfano wa lulu zilizohifadhiwa.
جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾
Jazaa kwa yale waliyokuwa wakitenda.
لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا تَأْثِيمًا ﴿٢٥﴾
Hawatosikia humo upuuzi na wala yanayosababisha dhambi.
إِلَّا قِيلًا سَلَامًا سَلَامًا ﴿٢٦﴾
Isipokuwa itasemwa: “Salama, salama!” [Al-Waaqi'ah: 10-26].
Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake
04-Nidhamu Zake
Alhidaaya.com [4]
Nidhamu za maamkizi ya Kiislamu kuhusu nani wa kuanza kutoa salaam, hali gani za kutoa salaam na kwa nani wanaofaa kutolewa salaam:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((يسلم الراكب على الماشي، والماشي على القاعد، والقليل على الكثير)) متفق عليه
وفي رواية للبخاري: ((والصغير على الكبير
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliyepanda (kipando) amsalimie anayetembea, anayetembea amsalimie aliyeketi na wachache wawasalimie walio wengi)) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy ((Mdogo amsalimie mkubwa))
Wajibu wa kumsalimia unayemjua na usiyemjua, nayo ni amali iliyo bora katika Uislamu:
عن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما، أن رجلاً سأل رسول الله: أي الإسلام خير؟ قال: ((تُطْعِمُ الطَّعامَ، وتقرأُ السَّلام علـى مَنْ عَرَفْتَ ومَنْ لَـمْ تَعْرِفْ)) البخاري ومسلـم
Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru bin Al-'Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amehadithia kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni amali gani katika Uislamu iliyo bora?” Akasema: ((Ni kulisha chakula na kumtolea salaam unayemjua na usiyemjua)) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Aliye bora kabisa mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla) ni mwenye kuanza na maamkizi, na maamkizi bora ni yale ya Kiislamu kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
عن أبي أمامة الباهلي رضي الله عنه قال :قيل يا رسول الله صلى: رجلان يلتقيان أيهما يبدا بالسلام؟ قال: ((أَولاَهما بالله تعالى )) الترمذي حديث حسن
Kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Baahiliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Watu wawili wanapokutana ni yupi anayepaswa kuanza kutoa salaam?” Akajibu: ((Ni yule aliye mbora kwa Allaah) [At-Tirmidhiy: Hadiyth Hasan].
Inapendekezeka kurudia kutoa salaam kwa uliyekutana naye kipindi kifupi nyuma, kama vile umeingia sehemu ukatoka na kisha ukaingia tena, au mathalan kuna ukuta au mti au kizuizi chochote baina yao kimewakinga na kisha wakakutana tena, basi wanaweza kusalimiana tena kwa dalili:
عن أبي هريررة رضي الله عنه عن رسول الله صلى الله عليه وسلم، قال: ((إذا لقي أحدكم أخاه، فليسلم عليه، فإن حالت بينهما شجرة، أو جدار، أو حجر، ثم لقيه، فليسلم عليه)) رواه أبو داود
Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mmoja wenu atakapokutana na nduguye amtolee salaam, iwapo watazuiwa na mti au ukuta au jiwe kisha akakutana naye basi amsalimie)) [Abu Daawuwd].
Mapendekezo ya kutoa salaam unapofika katika majlisi (kikao) na pindi unapoachana na walioketi katika kikao hicho:
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إذا انتهى أحدكم إلى المجلس فليسلم، فإذا أراد أن يقوم فليسلم، فليست الأولى بأحق من الآخرة)) رواه أبو داود، والترمذي وقال: حديث حسن
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapokomea mmoja wenu katika majlisi (kikao) atoe salaam, na atakapotaka kuondoka atoe salaam, kwani salaam ya kwanza si bora kuliko salaam ya pili)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan].
Unaweza pia kumtolea salaam mwanamke ambaye ni Mahram wako na pia yule ambaye ni ajinabi (asiye Mahram wako) usipochelea fitna na wao (wanawake) wanaweza nao kutoa salaam kwa wanaume kwa sharti kama hilo:
عن سهل بن سعد رضي الله عنه قال: كانت فينا امرأة - وفي رواية: كانت لنا عجوز- تأخذ من أصول السلق فتطرحه في القدر، وتكركر حبات من شعير، فإذا صلينا الجمعة، وانصرفنا، نُسلم عليها، فتقدمه إلينا” - رواه البخاري
Kutoka kwa Sahl bin Sa'ad (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesimulia kuwa, “Kulikuwa na mwanamke” – na katika riwaayah nyingine imesema: “Kulikuwa kuna ajuza (mwanamke mwenye umri mkubwa) akichukua mizizi ya kiazisukari (cheupe) akitia sufuriani na akisaga nafaka za shayiri. Tunapomaliza kuswali Swalaah ya Ijumaa na kutawanyika, tulikuwa tukimtolea salaam naye akituitikia.”[Al-Bukhaariy].
Pia:
عن أم هانئ فاختة بنت أبي طالب رضي الله عنه قالت: أتيت النبي صلى الله عليه وسلم يوم الفتح وهو يغتسل، وفاطمة تستره بثوب، فسلمت، وذكرت الحديث - رواه مسلم
Ummu Haaniy Faakhitah bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ambaye amesema: “Nilimuendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Ukombozi wa Makkah naye anaoga na Faatwimah (binti yake) anamstiri kwa nguo, nikamtolea salaam…” akaendelea mpaka mwisho wa Hadiyth.” [Muslim].
Hii ina uhusiano na Hadiyth ifuatayo:
عن أسماء بنت يزيد رضي الله عنه عنها أن رسول الله صلى الله عليه وسلم، مر في المسجد يومًا، وعصبة من النساء قعود، فألوى بيده بالتسليم. ((رواه الترمذي وقال: حديث حسن)).
Kutoka kwa Asmaa bin Yaziyd (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita msikitini siku moja kulikuwa na kundi la wanawake wameketi, akaashiria mkono wake kwa kutoa salaam.” [At-Tirmidhiy na kasema Hadiyth Hasan].
Hali hii inachukuliwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijumuisha baina ya kutamka na kuashiria na kinachotilia nguvu ni ile riwaayah ya Abuu Daawuwd inayosema “...akatutolea salaam” Kwa kuunganisha riwaayah hizo mbili, tunapata faida ya kujua kuwa mtu anapoashiria ni bora afutilizie ile ishara yake kwa maneno; kama ni ishara ya kusalimia, basi na atoe salaam mdomoni mwake japo haitosikiwa na aliye mbali.
Mafunzo Kutoka Katika Kisa Cha Swahaba:
عن الطفيل بن أبي بن كعب أنه كان يأتي عبد الله بن عمر، فيغدو معه إلى السوق، قال: فإذا غدونا إلى السوق، لم يمر عبد الله على سقاط ولا صاحب بيعة، ولا مسكين، ولا أحد إلا سلم عليه، قال الطفيل، فجئت عبد الله بن عمر يومًا، فاستتبعني إلى السوق فقلت له: ما تصنع بالسوق، وأنت لا تقف على البيع ولا تسأل عن السلع، ولا تسوم بها، ولا تجلس في مجالس السوق؟ وأقول: اجلس بنا هاهنا نتحدث، فقال يا أبا بطن- وكان الطفيل ذا بطن- إنما نغدو من أجل السلام فنسلم على من لقيناه. رواه مالك في الموطأ بإسناد صحيح
Kutoka kwa At-Twufaiyl bin Abiy Ka'ab kwamba 'Abdullaah bin 'Umar alimtembelea kisha akaenda naye sokoni. Walipokuwa njiani hakumpita mtu yeyote asiyeuza au anayeuza, wala masikini wala mtu yeyote ila alimsalimia. Akasema At-Twufayl: “Nikaenda kwa 'Abdullaah bin 'Umar siku moja akanitaka nimfuate sokoni. Nikamwambia: “Utafanya nini sokoni na hali husimami kwa muuzaji wala kuuliza bidhaa, wala kujadiliana nao biashara, wala hukai kikao sokoni? 'Abdullaah bin 'Umar akasema: “Tukae na kuzungumza”. Kisha akasema: “Ee Abaa Batwn” Alikuwa At-Twufayl ni mwenye tumbo! Tunakwenda huko kwa ajili ya kusalimia watu tu, tupate kumsalimia yeyote tunayekutana naye.” [Imaam Maalik katika Al-Muwattwa ikiwa na isnaad Swahiyh].
Baada ya kupata mafunzo na fadhila zote hizo kuhusu maamkizi ya Kiislamu tunatumai kwamba tutazingatia umuhimu wa kuamkiana kama ipasavyo, na umuhimu wa kuikamilisha salaam kwenye matamshi na maawasiliano yetu ya kimaandishi. Hali kadhaalika bial kuacha kumsalimia tunayemjua na tusiyemjua.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/256
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6854&title=Maamkizi%20Ya%20Kiislaam%3A%20Maamrisho%20Na%20Fadhila%20Zake
[4] http://www.alhidaaya.com/sw
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6855&title=01-Maamkizi%20Ya%20Kiislam%3A%20Umuhimu%20Na%20Baadhi%20Ya%20Fadhila%20Zake
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6856&title=02-Maamkizi%20Ya%20Kiislam%3A%20Kuwajibika%20Kwake
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6858&title=03-Maamkizi%20Ya%20Kiislam%3A%20Maamkizi%20Ya%20Peponi
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6860&title=04-Maamkizi%20Ya%20Kiislam%3A%20Nidhamu%20Zake