Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

 

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah

Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

 

Alhidaaya.com

 

 

Muziki ni haraam kutokana na dalili dhahiri tulizopewa katika Qur-aan na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Baadhi wa watu bado hawajatambua uharamu wa jambo hili, tunasikia wengi bado wanaimba taarabu na aina nyengine za nyimbo na muziki. Na  mara kwa mara unapomnasihi nduguyo Muislamu kuacha maasi haya, jibu mara nyingi huwa: "Tena nyinyi mmezidi! Wapi inasema kuwa nyimbo haramu?" Au wengine waliobobea katika maradhi haya hunena: "Mimi yote naweza kuacha lakini nyimbo utaniua!" Husema hivyo bila ya kujali amri ya makatazo ya Muumba wake ambaye ni Muweza wa kufutilia mbali masikio yake awe kiziwi na asiweze kusikia tena hizo nyimbo!

 

Inafika hadi Muislam hawezi kulala hadi alazwe kwa muziki, hawezi kula ila muziki uwe unapigwa, hawezi kufanya kazi za nyumbani bila muziki kufunguliwa, hawezi mtu kutembea bila kuwa na walkman au mp3 yake ikicheza, hawezi kufanya kazi akiwa kazini…hawezi kusafiri…hawezi hata kufanya mazoezi ya ndani bila kuwepo na muziki wa kumchochea na kumtia hamasa (kama wanavyoitakidi) ya lile analolifanya kwa wakati huo! Kwa kila hali, muziki umekuwa ni sehemu kubwa ya  maisha ya mwana Aadam kwa ambao bado wako katika maasi haya.

 

Hivyo tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuwakumbusha ndugu zetu waepukane na haramu hii ili wajiokoe na ghadabu kali za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambazo zinafika kumgeuza mtu awe nyani au nguruwe kama ilivyothibiti katika dalili zifuatazo:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

Na miongoni mwa watu yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّىٰ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٧﴾

Na anaposomewa Aayaat Zetu, hugeuka huku akitakabari kama kwamba hazisikii, kama kwamba kuna uziwi masikioni mwake, basi mbashirie adhabu iumizayo.   [Luqmaan 6-7]

 

Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu Aayah hii "Naapa kwa Allaah hii inamaanisha ni kuimba" [At-Twabariy 20:127]

 

وعن ابن عباس قال عن آية: ((وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ)، قال :الغناء وأشباهه إسناده صحيح - المحدث: الألباني

Na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) pia amesema kuhusu Aayah: ((Na miongoni mwa watu yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi)) amesema: "Ni nyimbo na maneno ya yanayofanana (ya upuuzi)" [Ameisahihisha Al-Albaaniy -

Swahiyh Adab Al-Mufrad (603)]
 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anamwambia Ibliys:

 

وَاسْتَفْزِزْ مَنِ اسْتَطَعْتَ مِنْهُم بِصَوْتِكَ وَأَجْلِبْ عَلَيْهِم بِخَيْلِكَ وَرَجِلِكَ وَشَارِكْهُمْ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ وَعِدْهُمْ ۚ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا ﴿٦٤﴾

Na wachochee punde kwa punde kiupumbavu uwawezao miongoni mwao kwa sauti yako na waitie na wasaliti kwa kikosi chako cha farasi, na askari waendao kwa miguu, na shirikiana nao katika mali na auladi na waahidi. Lakini shaytwaan hawapi ahadi isipokuwa ni ghururi. [Al-Israa: 64]

 

Hii inamaanisha ni nyimbo kama ilivyo rai ya Mujaahid katika Tafsiyr ya Ibn Kathiyr]

 

Na dalili za maharamisho na maonyo katika Sunnah ni zifuatazo:

 

1-Uharamu wa ngoma:

عن عبدالله بن عباس ((إِنَّ اللهَ حرمَ الخمرَ ، والميسرَ ، والكوبَةَ ، وكلُّ مسْكِرٍ حرامٌ))

و في رواية أحمد قال سفيان: قلت لعلي بن بذيمة: "ما الكوبة؟" قال: "الطبل"

Kutoka kwa 'Abdullaah bin ‘Abaas:   ((Hakika Allaah Ameharamisha pombe na kamari na kuwbah na kila kilinacholewesha ni haraam))  [Swahiyh Al-Jaami’(7336)]

 

Na katika usimulizi mwingine: Sufyaan amesema: Nilimuliza 'Aliy ibn Budhaymah: "Nini Kuwbah?" Akasema: "Ngoma".  [Swahiyh Abiy Daawuwd (3696)]

 

2-Wenye kuimba, kusikiliza muziki watageuzwa nyani na nguruwe!

 

  أَبُو عَامِرٍ ـ أَوْ أَبُو مَالِكٍ سَمِعَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ : ((لَيَكُونَنَّ مِنْ أُمَّتِي أَقْوَامٌ يَسْتَحِلُّونَ الْحِرَ وَالْحَرِيرَ وَالْخَمْرَ وَالْمَعَازِفَ، وَلَيَنْزِلَنَّ أَقْوَامٌ إِلَى جَنْبِ عَلَمٍ يَرُوحُ عَلَيْهِمْ بِسَارِحَةٍ لَهُمْ، يَأْتِيهِمْ لِحَاجَةٍ فَيَقُولُوا ارْجِعْ إِلَيْنَا غَدًا‏.‏ فَيُبَيِّتُهُمُ اللَّهُ وَيَضَعُ الْعَلَمَ، وَيَمْسَخُ آخَرِينَ قِرَدَةً وَخَنَازِيرَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ)) رواه البخاري

 

Amehadithia Abuu ‘Aamir au Abuu Maalik kwamba kamsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:  ((Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Baadhi ya watu watakuwa pembeni mwa mlima na mchungaji wao atawajia jioni na kuwaomba haja [fulani]. Watasema: "Rudi kesho". Allaah Atawaangamiza usiku, Atawaangushia milima kisha Atawabadilisha waliobakia wawe nyani na nguruwe na watabakia hivyo hadi siku ya Qiyaamah)) [Al-Bukhaariy]
 
Hadiyth hii inatuthibitishia kuwa madhambi yote hayo yako sawa sawa uharamu wake, kama vile zinaa na pombe ilivyo haramu, basi na uharamu wa muziki pia ni sawa sawa. Sasa vipi Muislamu aone kuwa muziki sio maasi makubwa ya kujiepusha nayo?
 

Na Hadiyth nyengine:

 

عَنْ أَبِي مَالِكٍ الأَشْعَرِيِّ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ـ صلى الله عليه وسلم ـ ‏ ((لَيَشْرَبَنَّ نَاسٌ مِنْ أُمَّتِي الْخَمْرَ يُسَمُّونَهَا بِغَيْرِ اسْمِهَا يُعْزَفُ عَلَى رُءُوسِهِمْ بِالْمَعَازِفِ وَالْمُغَنِّيَاتِ يَخْسِفُ اللَّهُ بِهِمُ الأَرْضَ وَيَجْعَلُ مِنْهُمُ الْقِرَدَةَ وَالْخَنَازِيرَ)) سنن إبن ماجه

Maalik Al-Ash’ariyy amehadithi kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu katika Ummah wangu watakunywa pombe wakiipa jina jengine lisilokuwa hilo, miziki itapigwa kwa ajili yao na watakuweko waimbaji wanawake. Allaah Atawadidimiza ardhini na Atawageuza wawe nyani na nguruwe)) [Ibn Maajah ameisahihisha Al-Albaniy Swahiyh Ibn Maajah (3263)]

 
3-Ghadhabu za Allaah kuwaangamiza wenye kuimba, kusikiliza muziki, na kucheza ngoma.

   

  عَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏: ((‏فِي هَذِهِ الأُمَّةِ خَسْفٌ وَمَسْخٌ وَقَذْفٌ ))‏ ‏.‏ فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ الْمُسْلِمِينَ يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَتَى ذَاكَ قَالَ: ((إِذَا ظَهَرَتِ الْقَيْنَاتُ وَالْمَعَازِفُ وَشُرِبَتِ الْخُمُورُ))

Kutoka kwa ‘Imraan bin Huswayn kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watakuweko katika Ummah huu mdidimizo wa ardhi, kugeuzwa maumbile ya binaadamu, na maafa ya kuteremshiwa mawe kutoka mbinguni)) Mtu mmoja akuliza: Itatokea lini hiyo? Akasema: ((Itakapodhihirika muziki, ulevi …)) [At-Trimidhy, Swahiyh At-Tirmidhiy (2212)]

 

4-Sauti za nyimbo zimelaaniwa duniani na Aakhirah

 

عن أنس بن مالك: ((صَوْتانِ ملعونانِ في الدنيا والآخرةِ : مزمارٌ عند نعمةٍ ، ورَنَّةٌ عند مُصيبةٍ))
 Kutoka kwa Anas bin Maalik  ((Sauti mbili zimelaaniwa duniani na Aakhirah; mizumari katika furaha na kuombeleza katika misiba)) [Swahiyh At-Targhiyb (3527)]

 

5-Malaika wanamkimbia mwenye sauti kama hizo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((لاَ تَصْحَبُ الْمَلاَئِكَةُ رُفْقَةً فِيهَا كَلْبٌ وَلاَ جَرَسٌ)‏

Kuktoka kwa Abuu Hurayah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Malaika hawafuatani na watu wenye mbwa na walio na kengele)) [Muslim]
 

Ikiwa kengele tu inawakimbiza Malaika, seuze nyimbo, ngoma, mizumari na aina zote za muziki ambazo zinaamsha vishawishi na kuchochea hisia za wana Aadam?

 

6-Mwenye kumpatia taarifa au kumpelekea nduguye ngomani au kusikiliza muziki, nyimbo atabeba dhambi zake na dhambi za nduguye.

 

Mara nyingi Waislamu wenye kufanya maasi haya wanasabisha wenzao kutumbukia pia katika maasi haya; kuna wanaoalika watu katika shughuli zenye maasi hayo (parties) zenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume, wenye kupiga taarabu katika maharusi, na wengine wanaofika hadi kununua kanda, video n.k na kuwapa wenziwao kama zawadi. Basi wenye kufanya hivyo watabeba madhambi yao na madhambi ya wenziwao:  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ﴿٢٥﴾

Ili wabebe mizigo (ya madhambi) yao kamili Siku ya Qiyaamah, na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya elimu. Tanabahi!  Uovu ulioje wanayoyabeba. [An-Nahl: 25]

 

Na pia:

  إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾

Hakika Sisi Tunahuisha wafu, na Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao na kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari bayana.  [Yaasiyn: 12]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

مَنْ سَنَّ فِي الإِسْلاَمِ سُنَّةً حَسَنَةً فَلَهُ أَجْرُهَا وَأَجْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا بَعْدَهُ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَىْءٌ وَمَنْ سَنَّ فِي الإِسْلاَمِ سُنَّةً سَيِّئَةً كَانَ عَلَيْهِ وِزْرُهَا وَوِزْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا مِنْ بَعْدِهِ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَىْءٌ ‏"‏ ‏.‏ مسلم

"Atakayeanzisha mwenendo mwema " سُنَّةً حَسَنَةً katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenenedo mbaya سُنَّةً سَيِّئَةً atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo bila ya kupungua kitu katika madhambi yao " [Muslim] 

 
 

7-Tahadhari! Yasije kukuta mauti ukiwa katika kusikiliza au kuimba kwani mtu atafufuliwa na ‘amali yake ya mwisho!

 
 عن جابر بن عبدالله قَالَ : سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: (( يُبْعَثُ كُلُّ عَبْدٍ عَلَى مَا مَاتَ عَلَيْه ((رواه مسلم

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah: "Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ((Kila mja atafufuliwa katika hali aliyofia nayo))[Muslim]
 

Je, ndugu Muislamu unayependa muziki, umetafakari vipi utakuwa mwisho wako?
 
Je, haikuingii khofu katika moyo wako kuwa huenda mwisho wako ukawa ni kuimba nyimbo badala ya kusema "Laa ilaaha Illa Allaah" neno ambalo ukilitaja mwisho wa maisha yako wakati wa kufa utaingia Jannah? 

 

Muongozo Na Nasaha Za Kujiepusha Kusikiliza Nyimbo, Muziki na kucheza Ngomba:

 

1-Tusikilize Na Kusoma Qur-aan

 

Muziki na nyimbo humjaza mtu mapenzi makubwa moyoni, zimshughulishe zaidi hadi asiwe na muda wa Qur-aan ambayo  ndio ipasayo kukaririwa midomoni mwetu kwa sauti nzuri kama alivyoamrisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) .

  
2-Ni Sunnah Kuziba Masikio Unaposikia Nyimbo, Muziki Bila Ya Kutaka:

 
 عَنْ نَافِعٍ، قَالَ سَمِعَ ابْنُ عُمَرَ، مِزْمَارًا - قَالَ - فَوَضَعَ أُصْبُعَيْهِ عَلَى أُذُنَيْهِ وَنَأَى عَنِ الطَّرِيقِ وَقَالَ لِي يَا نَافِعُ هَلْ تَسْمَعُ شَيْئًا قَالَ فَقُلْتُ لاَ ‏.‏ قَالَ فَرَفَعَ أُصْبُعَيْهِ مِنْ أُذُنَيْهِ وَقَالَ كُنْتُ مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَسَمِعَ مِثْلَ هَذَا فَصَنَعَ مِثْلَ هَذَا ‏.‏

Kutoka kwa Naafi'i ambaye amesema, amesikia sauti ya muziki akaziba masikio yake kwa vidole vyake, kisha akamgeuza mnyama wake aliyempanda [arudi asiendelee kwenda sehemu hiyo iliyokuwa na muziki] akasema: "Ee Naafi'i, umesikia kitu?" Akasema, nikajibu: "Hapana". Akaondosha vidole vyake masikioni mwake akasema: "[siku moja] Nilikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliposikia kama hivi [muziki] akafanya kama hivi [nilivyofanya mimi yaani kuziba masikio yake asisikie sauti ya mizumari] [Abuu Daawuwd  - Swahiyh Abiy Daawuwd (4924)]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ajaalie makaka hii iwe zingatio kwa ndugu zetu walio katika maasi haya, wajiepusha na uharamu huu.  

 

 

   

 

Share