33-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno

 

Fadhila Za  Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

33-Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ ﴿٣﴾

 

Na hakika wewe bila shaka una ujira usiokatika. [Al-Qalam: 3]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ ﴿٤﴾

 

Na Tukanyanyulia juu utajo wako (ukawa mwenye kusifika mno)?  [Ash-Sharh: 4]

 

Allaah (سبحانه وتعالى)  Amemfadhilisha na kumkirimu Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kutajwa mno na kusifiwa na akawa maarufu ulimwenguni.  Hutajwa katika kila Adhaana ya Swalaah, katika Iqaamah, katika khutbah za Ijumaa, katika kutamka Shahaadah, na hutajwa ndani ya Swalaah na kila zinapotajwa Hadiyth zake, na anaswaliwa katika kuomba du’aa ambapo du’aa haitaqabaliwi bila ya kumswalia yeye kwanza, na huswaliwa pia inapomalizika du’aa, na katika hali nyingi mbali mbali, na Hadiyth zifuatazo zinathibitisha:

 

عن ابي سعيد الخدري رضي الله عنه ان رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: أتاني جبريلُ فقال: إنَّ ربِّي وربَّك يقولُ لك: كيف رفَعْتُ ذِكْرَك ؟ قال: اللهُ أعلَمُ قال: إذا ذُكِرْتُ ذُكِرْتَ معي

Imepokelewa kutoka kwa Sa’idy Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  “Amenijia Jibriyl akasema: Hakika Rabb wangu na Rabb Wako Anasema: Vipi umenyanyuliwa juu utajo wako? Akasema: Allaah Anajua zaidi. Akasema: (Allaah Anasema): Kila nnapotajwa, nawe unatajwa pamoja nami.” [Ibn Jariyr, Ibn Abiy Haatim, Ibn Hibbaan na Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Hibbaan 3382]

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema ) (kuhusu maana ya):  “Sitajwi isipokuwa unatajwa pamoja Nami”;  katika Adhaan, Iqaamah, Tashahhud, Siku ya Ijumaa, kwenye Minbari (khutbah), Siku ya ’Iydul-Fitwr, Siku ya ’Iydul- Adhw-haa, Ayyaamut-Tashriyq, Siku ya ’Arafah, katika Jamarah, katika Swafaa Wal Marwah, katika Khutbah za Nikaah, Mashariki ya ardhi na Magharibi, na kwamba lau mtu akamwabudu Allaah akaamini Jannah na Moto na kila kitu lakini hashuhudii  kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah,  basi hakuna kitakachomfaa na atakuwa ni kafiri. [Tafsiyr Al-Qurtwubiy]

 

Naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 ((الْبَخِيلُ مَنْ ذُكِرْتُ عِنْدَهُ فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيَّ))

((Bakhili ni yule ambaye nikitajwa haniswalii))  [Hadiyth ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (رضي الله عنه)   - At-Tirmidhiy (5/551) [3546], na wengineo na angalia: Swahiyh Al-Jaami’ (3/25) [2787] na Swahiyh At-Tirmidhiy (3/177)]

 

Share