05-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Al-Huduwd (Adhabu): Mlango Wa Ta’ziyr Na Hukumu Ya Mshambuliaji
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلْحُدُودِ
Kitabu Cha Haddi (Adhabu)
بَاب اَلتَّعْزِيرِ وَحُكْمِ اَلصَّائِلِ
05-Mlango Wa Ta’ziyr[1] Na Hukumu Ya Mshambuliaji
1074.
عَنْ أَبِي بُرْدَةَ اَلْأَ نْصَارِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّهُ سَمِعَ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ يَقُولُ: {" لَا يُجْلَدُ فَوْقَ عَشَرَةِ أَسْوَاطٍ، إِلَّا فِي حَدِّ مِنْ حُدُودِ اَللَّهِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abuu Burdah[2] Al-Answaariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alisema kuwa alimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Asichapwe mtu zaidi ya mijeledi kumi[3] isipokuwa katika haddi (adhabu) miongoni mwa haddi za Allaah.” [Bukhaariy, Muslim]
1075.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {" أَقِيلُوا ذَوِي اَلْهَيْئَاتِ عَثَرَاتِهِمْ إِلَّا اَلْحُدُودَ"} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Wasameheni wenye tabia nzuri[4] kuteleza kwao isipokuwa katika haddi.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]
1076.
وَعَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {مَا كُنْتُ لِأُقِيمَ عَلَى أَحَدٍ حَدًّا، فَيَمُوتُ، فَأَجِدُ فِي نَفْسِي، إِلَّا شَارِبَ الْخَمْرِ، فَإِنَّهُ لَوْ مَاتَ وَدَيْتُهُ} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Msimamishieni haddi yeyote na akifa nikahuzunika isipokuwa mnywaji pombe, kwani lau atakufa nitamtolea diya.”[5] [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
1077.
وَعَنْ سَعِيدِ بْنِ زَيْدٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {" مِنْ قُتِلَ دُونَ مَالِهِ فَهُوَ شَهِيدٌ"} رَوَاهُ اَلْأَرْبَعَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ
Kutoka kwa Sa’d bin Zayd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Anayeuwawa kwa kutetea mali zake huyo ni Shahidi.” [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha At-Tirmidhiy]
1078.
وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ خَبَّابٍ قَالَ: سَمِعْتَ أَبِي رَضِيَ اللهُ عَنْهُ يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ يَقُولُ: {" تَكُونُ فِتَنٌ، فَكُنْ فِيهَا عَبْدَ اَللَّهِ اَلْمَقْتُولَ، وَلَا تَكُنْ اَلْقَاتِلَ"} أَخْرَجَهُ ابْنُ أَبِي خَيْثَمَةَ. وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ
وَأَخْرَجَ أَحْمَدُ نَحْوَهُ: عَنْ خَالِدِ بْنِ عُرْفُطَةَ
Kutoka kwa ‘Abdillaah[6] bin Khabbaab[7] amesema amemsikia Baba yangu (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) akisema kuwa alimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Kutakuwa na fitnah,[8] kuwa mja wa Allaah mwenye kuuwawa wala usiwe mwenye kuua.”[9] [Imetolewa na Abiy Khaythamah na Ad-Daaraqutwniy]
Na Ahmad ameipokea Hadiyth kama hii kutoka kwa Khaalid bin ‘Urfutwah[10]
[1] Kuadhiri na kuadhibu.
[2] Huyu ni Hani bin Niyaar aliyekuwa Swahaba kutoka katika kabila la Balawi. Alikuwa ni mshirika wa Al-Answaar na alishuhudia vita vya Badr na vita vinginevyo. Alifariki mwaka 41, na inasemekana 42 na wengine 45 Hijriyyah.
[3] Hadiyth hii imefahamika na baadhi ya Fuqahaa kuwa ni dalili hawezi mtu kuchapwa zaidi ya mijeledi kumi isipokuwa mtu huyo ameingia katika adhabu ya haddi. Imaam Shaafi’iy na Maalik kuongeza inaruhusiwa ilimradi isifikie kile kiwango cha haddi kilichotajwa. Wengine wanaona kuwa huwezi kuongeza maadamu adhabu imetajwa. Wengine wanaona kuwa inaweza kuongezeka zaidi ya mijeledi kumi ikiwa ni adhabu ya kosa kubwa, wakati makosa madogo huwezi kzidisha zaidi ya mijeledi kumi.
[4] Katika adhabu za haddi zilizoainishwa kulingana na makatazo, adhabu hizo zitawahusu wote bila kubagua, tajiri au masikini, mtu wa kawaida au yule mwenye nafasi kubwa katika jamii. Katika makosa madogo madogo hali inaangaliwa kulingana na muda, aina ya kosa, na mtu aliyehusika na kosa lenyewe.
[5] Hadiyth hii inaonesha pia kuwepo kwa tofauti ya rai baina ya Maswahaba wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ikiwa kumchapa mnywa pombe kwa mijeledi arubaini ilikuwa ni adhabu ya haddi au ilikuwa ni Ta’ziyr (kumuadhibu kwa kumuadhiri). Hilo vile vile lilikuwa ni adhabu ya kumuadhiri mtu mzima kwa sababu adhabu ile haipo katika Qur-aan. Hakuna cha kufanya kwa wale ambao watakufa kwa kutekelezewa adhabu ile kwao. Hata hivyo, ikiwa kama mtu atakufa akipitishiwa hukumu hiyo ya kumwadhiri ni juu ya Dola kutoa fidiya kutoka katika hazina wa warithi wa aliyefariki. Tokea hapo, ikawa kila mnywa pombe atakapoadhibiwa na akafa katika adhabu ile, Fuqahaa wana rai kuwa itolewe fidia walipwe warithi wake.
[6] ‘Abdullaah alikua ni miongoni mwa Taabi’iyna na mkazi wa Madiyna. Hururiya (Khawaarij) walimuuwa katika mwaka wa 27 Hijriyyah baada ya kumuasi ‘Aliy na alikuwa njiani akielekea An-Naharwaan. Baada ya kumuuwa waliingia nyumbani kwake, walimuuwa mjakazi wake na kukatakata kichanga kilichokuwa tumboni mwake. Hili lilipelekea vita maarufu vya An-Naharwaan ambapo ‘Aliy aliwauwa Khawaarij wote isipokuwa tisa miongoni mwao ambao walisababishia fitnah kubwa huko mbele.
[7] Khabbaab bin Al-Arat bin Jandala At-Tamiymi alikuwa mmoja wa Maswahaba walioteswa kwa ajili ya Dini yao. Alishiriki katika vita vya Badr. Alikufa katika mji wa Kufa uliopo ‘Iraaq alipokataa kushiriki katika vita vya Siffin katika mwaka wa 37 Hijriyyah akiwa na umri wa miaka 73.
[8] Fitnah ni mitihani mbalimbali ni ule mtafaruku uliokuwa ukitokea katika Ummah na katika Dini.
[9] Imetajwa katika Hadiyth iliyotangulia kuwa mwenye kufa akitetea nafsi yake, mali na familia yake atakuwa amekufa Shahidi. Akimuua adui kwa njia ya kujilinda hatopata dhambi kwa mauaji yale. Hukumu hii hutekelezwa ikiwa hali ipo kwa uwazi na sababu zimefahamika. Ikiwa jambo halipo wazi na kuna ukinzani na ugomvi hatakiwi mtu kunyanyua mkono wake kuuwa. Njia nzuri kwa mtu za kuwa salama ni kuacha kuuwa, kwa kuwa muuwaji hukabiliwa na adhabu ya moto, ama aliyeuliwa huingia Jannah. Ikiwa wote watapigana na kila mmoja kupupia kumuuwa mwenzake wote watakabiliwa na adhabu ya moto atakapo Allaah.
[10] Huyu ni Swahaba kabila lake ni Quda katika koo za ‘Udhr. Alikuwa ni mwakilishi wa Sa’d bin Abiy Waqqaas katika mji wa Kufa. Alifariki mwaka 61 Hijriyyah na inasemekana kuwa Al-Mukhtar bin Abuu ‘Ubayd alimuuwa baada ya kifo cha Yaziyd mwaka 64 Hijriyyah.