05-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Zuhd Yake: Akibaki Na Njaa Na Chakula Chake Kilikuwa Duni

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

05-Zuhd Yake: Akibaki Na Njaa Na Chakula Chake Kilikuwa Duni  

 Alhidaaya.com

 

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akibaki na njaa yeye pamoja na ahli zake, na aghlabu ya chakula chake kilikuwa ni duni.  Hadiyth kadhaa zimethibiti kuhusu hali hizi, miongoni mwazo ni Hadiyth zifuatazo:

 

Aghlabu ya chakula chao kilikuwa ni mkate wa shayiri:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال :  "كَانَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَبِيتُ اللَّيَالِي الْمُتَتَابِعَةَ طَاوِيًا ، وَأَهْلُهُ لاَ يَجِدُونَ عَشَاءً ، وَكَانَ أَكْثَرُ خُبْزِهِمْ خُبْزَ الشَّعِيرِ" رواه الترمذي (2360) وحسنه الألباني في صحيح الترمذي .

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akipitisha nyusiku kadhaa na ilhali ahli zake hawakupata chakula cha usiku, na aghlabu ya chakula chao kilikuwa ni mkate wa shayiri.” [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy]  

 

Hakupata kula nyama ya kuoka wala mkate mwembamba:

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ سِنَانٍ، حَدَّثَنَا هَمَّامٌ، عَنْ قَتَادَةَ، قَالَ: "كُنَّا عِنْدَ أَنَسٍ وَعِنْدَهُ خَبَّازٌ لَهُ فَقَالَ مَا أَكَلَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم خُبْزًا مُرَقَّقًا وَلاَ شَاةً مَسْمُوطَةً حَتَّى لَقِيَ اللَّهَ"‏.‏  البخاري

Ametuhadithia Muhammad bin Sinaan, ametuhadithia Hammaam, kutoka kwa Qataadah amesema: Tulikuwa kwa Anas na mwokaji mikate alikuwa pamoja naye. Anas akasema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakupata kula mkate mwembamba wala mbuzi wa kuokwa mpaka kukutana kwake na Allaah (kufariki kwake).”  [Al-Bukhaariy]

 

Hakupata kula supu ya nyama ya kuwashibisha siku tatu mfululizo:

 

عَنْ عَائِشَةَ رضى الله عنها قَالَتْ: "مَا فَعَلَهُ إِلاَّ فِي عَامٍ جَاعَ النَّاسُ، أَرَادَ أَنْ يُطْعِمَ الْغَنِيُّ الْفَقِيرَ، وَإِنْ كُنَّا لَنَرْفَعُ الْكُرَاعَ بَعْدَ خَمْسَ عَشْرَةَ، وَمَا شَبِعَ آلُ مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم مَنْ خُبْزِ بُرٍّ مَأْدُومٍ ثَلاَثًا"‏.‏

‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema:  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakufanya hivyo (yaani: kukataza uhifadhi wa nyama ya Udhwhiya kwa siku tatu) isipokuwa (aliruhusu kuhifadhi nyama) ili tajiri awalishe masikini. Lakini baadaye tulikuwa tunaweka makongoro (ya mbuzi) zaidi ya siku kumi na tano. Familia ya Muhammad haikupata kula mkate wa ngano kwa nyama au supu ya kuwashibisha kwa siku tatu mfululizo.”   [Al-Bukhaariy]

 

Faida:

 

‘Aaishah (رضي الله عنها) aliulizwa katika Hadithi hii kuhusu ukatazaji wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kula nyama ya Udhwhiyah baada ya siku tatu. Akasema kuwa Nabiy aliamrisha  hivyo yaani kuhifadhi nyama ya Udhwhiyah. (Kuchinjwa mnyama siku ‘Iydul-Adhwhaa) kwa siku tatu katika mwaka uliokuwa ni mwaka wa njaa ili tajiri waweze kulisha maskini nyama ya Udhwhiyah.

 

 

Share