02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Hukmu Ya Zakaah Na Hadhi Yake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

02-Hukmu Ya Zakaah Na Hadhi Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Zakaah ni Fardhi ‘Ayn kwa kila mtu ambaye zimekamilika kwake shuruti za kuwajibikiwa. Ufaradhi wake umethibiti katika Qur-aan, Sunnah na Ijma’a.

 

Katika Qur-aan, kuna Aayah nyingi zinazozungumzia uwajibu wa Zakaah na ulazima wa kulichukulia hima sana suala hili. Na kutokana na uzito wake, Zakaah imewekwa sambamba na Swalaah katika jumla ya Aayah 82.  Kati ya Aayah hizo, ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ))

((Basi simamisheni Swalaah na toeni Zakaah)). [Al-Hajj (22:78)]

 

Na Kauli Yake:

 

 ((خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ))

((Chukua katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah)). [At-Tawbah (9:103)]

 

Aidha, makamio ni makubwa na mazito kwa mwenye kufanya ubakhili wa kuitoa. Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa Anasema:

 

(( وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ • يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ))

((Na wale wanaorundika dhahabu na fedha [silver] na wala hawazitoi katika Njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo • Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): “Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika)). [At-Tawbah (9:34 na 35]

 

Imepokelewa kwa njia swahiyh toka kwa Ibn ‘Umar na Jaabir bin ‘Abdillaah kwamba wamesema: “Mali iliyotolewa Zakaah yake, haihesabiwi kuwa hazina ya mali [kanz]”.

 

Sunnah nayo imethibitisha wajibu wa Zakaah. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema:

 

((إنك تأتي قومًا أهل كتاب، فادعهم إلى شهادة أن لا إله إلا الله وأني رسول الله، فإن هم أطاعوا لذلك فأعلمهم أن الله عز وجل  افترض عليهم خمس صلوات في كل يوم وليلة، فإن هم أطاعوا لذلك فأعلمهم أن الله تعالى افترض عليهم صدقة في أموالهم تؤخذ من أغنيائهم وتُرَدُّ إلى فقرائهم، فإن هم أطاعوا لذلك فإياك وكرائمَ أموالهم، واتقِ دعوة المظلوم؛ فإنه ليس بينها وبين الله حجابٌ))

“Kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwenda Yemen alimwambia: ((Hakika wewe unawaendea watu wa Ahlul Kitaab. Basi walinganie washahadie kuwa hapana mungu isipokuwa Allaah, na mimi ni Rasuli wa Allaah. Na kama watalitii hilo, basi wajulishe kuwa Allaah ‘Azza wa Jalla Amewafaradhishia Swalaah Tano kila mchana na usiku. Na kama watalitii hilo, basi wajulishe kuwa Allaah Ta’aalaa Amewafaradhishia Zakaah katika mali zao, huchukuliwa toka kwa matajiri wao na kurejeshwa kwa masikini wao. Na kama watalitii hilo, basi chunga usije kuchukua mali zao za thamani kubwa [wakati wa kukusanya Zakaah], na ogopa sana du’aa ya aliyedhulumiwa, kwani haina kizuizi kati yake na kati ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1496) na Muslim (19)]

 

Ama Ijma’a, hii imekubaliana kwa sauti moja juu ya ufaradhi wa Zakaah. Hakuna aliyekwenda kinyume na hilo tokea enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka hivi leo.

 

Ama hadhi yake katika diyn, Zakaah ni nguzo kati ya nguzo tano za Uislamu, nayo ni nguzo ya tatu baada ya Shahadah Mbili na Swalaah. Nabiy (Swalla Allaahu alayhi wa ‘aalihii wa sallam) amesema:

((بُني الإسلام على خمس: شهادة أن لا إله إلا الله وأن محمدًا رسول الله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة، وصوم رمضان، وحج البيت لمن استطاع إليه سبيلا))

((Uislamu umejengwa juu ya (nguzo) tano: Kushahadia kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhwaan, na kuikusudia Nyumba kwa atakayeweza kwenda)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (8) na Muslim (16)]

 

Na kwa ajili hiyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichukua kwa Maswahaba bay-‘a ya kwamba lazima wataitoa. Imepokelewa toka kwa Jariyr bin ‘Abdullaah akisema: ((Nilimpa bay-‘a Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa lazima nisimamishe Swalaah, nitoe Zakaah na [nitoe] nasaha kwa kila Muislamu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (57) na Muslim (56)]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuwapiga vita wasiotoa Zakaah. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((أمرت أن أقاتل الناس حتى يشهدوا أن لا إله إلا الله وأن محمدا رسول الله ، ويقيموا الصلاة، ويؤتوا الزكاة))

((Nimeamuriwa kuwapiga watu vita mpaka washahadie kuwa hapana mungu isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (25) na Muslim (22)]

 

 

 

Share