05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Shuruti Za Uwajibu Wa Kutoa Zakaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

05-Shuruti Za Uwajibu Wa Kutoa Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah si waajib katika mali isipokuwa kwa shuruti. Ni katika Hikma ya Allaah ‘Azza wa Jalla katika kufaradhisha Sharia Zake kuwa Ameziwekea shuruti; yaani sifa maalumu ambazo sharia hizo haziwi waajib bila kuwepo shuruti hizo, ili sharia hizo ziwe sawa madhubuti. Na kama kusingelikuwepo shuruti, basi kila kitu kingeweza kubeba uwezekano wa kuwa waajib au si waajib. Lakini pia kuna vizuizi vinavyoondosha uwajibu wa Zakaah pamoja na kuwepo shuruti, na vitu vyote havitimu ila kwa kukamilika shuruti zake na kutokuwepo vizuizi vyake.  [Ash-Sharhu Al-Mumti’u]

 

 

Shuruti hizi zina vigawanyo viwili. Shuruti kwa mwenye mali aliyewajibikiwa Zakaah, na shuruti katika mali yenyewe.

 

Masharti ambayo ni lazima yakamilike kwa mwenye mali ili Zakaah iwe wajibu kwake

 

Mwenye mali ambaye amewajibikiwa na Zakaah ana masharti mawili:

 

1- Awe huru (muungwana)

 

Zakaah si waajib kwa mtumwa, kwa kuwa mtumwa hamiliki, bali bwana wake ndiye anayemiliki mali zake. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa Salllam) anasema:

((من باع عبدا له مال، فماله للذي باعه إلا أن يشترط المبتاع))

((Mwenye kumuuza mtumwa anayemiliki mali, basi mali yake ni ya mwenye kumuuza ila tu kama mnunuzi atashurutisha)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2379) na Muslim (1173)

 

Na kauli ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

((ليس في مال العبد زكاة حتى يعتق))

((Mali ya mtumwa haina Zakaah mpaka aachwe huru)). [Al-Bayhaqiy (1/108) kwa Sanad Swahiyh. Angalia Al-Irwaa (3/252)].

 

Na toka kwa Kiysaan bin Abiy Sa’ad Al-Maqbariy amesema: ((Nilimwendea ‘Umar na dirham mia mbili ya Zakaah ya mali yangu– nami ni mtumwa niliyeandikishiana mkataba na bwana wangu–akaniuliza: Je, umeachwa huru? Nikamwambia: Na’am. Akasema: Nenda ukaigawe)). [Muswannaf Ibn Abiy Shaybah kwa Sanad Jayyid katika Al-Irwaa (2/252)]

 

 

2- Awe Muislamu

 

Zakaah si waajib kwa kafiri kwa Ijma’a kwa kuwa Zakaah ni ‘ibaadah takatifu, na kafiri hana utakaso madhali yupo kwenye ukafiri wake.  Tunaposema Zakaah si katika mali yake, tunamaanisha kuwa hatumlazimishi aitoe ili awe salama au apate amani. Zakaah haikubaliwi toka kwa makafiri, na hakuna faida kuwalazimisha kuitoa. Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

((وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ ))

((Na haikuwazuilia ikubaliwe kwao michango yao isipokuwa kwa kuwa wao walimkufuru Allaah na Rasuli Wake)). [At-Tawbah (9:54)]

 

Lakini hii haina maana kuwa kafiri hatohisabiwa kwa kuacha kutoa, kwa kuwa makafiri wanasemeshwa na vipengele vya sharia kwa mujibu wa ilivyopitishwa katika taaluma ya Uswuwl. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

Hukmu hii yote ni kwa kafiri wa kuzaliwa. Ama aliyeritadi –tunajilinda kwa Allaah na hilo-, ikiwa Zakaah ilikuwa imemwajibikia wakati bado ni Muislamu, basi haisameheki kwa kuritadi kwa mujibu wa kauli ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali, kwa kuwa ni haki ambayo uwajibu wake ulithibiti. Kuritadi hakuipomoshi, na mfano wake ni kama faini ya kuharibu vitu. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/233 Kuwait) na Fiqhu Az-Zakaah (1/115)]

 

Lakini Hanbali anasema inafutika kwa kuritadi.

 

Je, Zakaah ni waajib kwa mali ya mtoto mdogo na mwendawazimu?

 

‘Ulamaa wana kauli mbili mashuhuri katika suala hili:

 

Ya kwanza:

 

Si waajib, sawasawa kwa mali yote au sehemu ya mali. [Al-Mughniy (2/622), Badaai’u Asw-Swanaai’i (2/4-5), Al-Majmuw’u (5/329), Al-Muhallaa (5/205) na Fiqhu Az-Zakaah (1/125)]

 

Hili kalisema Abu Haniyfah, na limesimuliwa pia toka kwa baadhi ya Masalaf. Wamesema kuwa Zakaah ni ‘ibaadah halisia kama Swalaah ambayo inahitajia niya, na mtoto au mwendawazimu hawana niya.

 

Isitoshe, mtoto na mwendawazimu hawana taklifu, hivyo si lazima kwao. Na Zakaah pia ni kitwaharisho kwa mtoaji wake, na utwaharisho ni kwa uchafu wa madhambi, na wawili hawa hawana dhambi. Kadhalika, kutochukua Zakaah katika mali yao ni sawa na kuilinda, kwa kuwa hawana uwezo wa kuiwekeza kiuchumi.

 

Ya pili:

 

Ni waajib kutoa Zakaah katika mali ya mtoto na mwendawazimu. [Al-Muhallaa (5/201), Al-Majmuw’u (5/329), Majmuw’u Al-Fataawaa (25/17), Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/232) na Ash-Sharh Al-Mumti’u (6/26)]

 

Hii ni kauli ya Jumhuri. Pia ni kauli ya ‘Umar, ‘Aliyy, ‘Abdullaah bin ‘Umar, ‘Aaishah, na Jaabir bin ‘Abdullaah. [Angalia Muswannaf wa ‘Abdul Razzaaq (6986-6992), Muswannaf Ibn Abiy Shaybah (3/149), Sunan Al-Bayhaqiy (4/107), Al-Muhallaa (5/208) na Al-Amwaal cha Abiy ‘Ubayd (uk 448)]

 

Na hakuna Swahaba yeyote anayejulikana kuwa alikwenda kinyume na kauli hii isipokuwa riwaya dhwa’iyf ya Ibn ‘Abbaas ambayo haiwezi kutolewa dalili.

 

Kauli hii inatiliwa nguvu na:

 

- Ujumuishi wa Aayaat na Hadiyth zinazohabarisha uwajibu usio ainishi wa Zakaah katika mali ya matajiri. Katika Aayaat na Hadiyth hizo, mtoto na mwendawazimu hawakutolewa nje ya duara la uwajibu.

 

- Yaliyopokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab aliyesema: ((Wekezeni mali za mayatima katika biashara, ili zisiliwe na Zakaah)). [Dhwa’iyf: Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (641), Muwattwau Maalik, Ad-Daaraqutwniy (2/111) na ‘Abdul Razzaaq (2) kwa Sanad Dhwa’iyf. Angalia Al-Irwaa (788)]

 

- Makusudio ya Zakaah ni kuziba pengo la mahitaji ya masikini kwa mali ya matajiri kama shukrani kutoka kwao kwa Allaah Ta’aalaa na kutakasa mali zao. Na mali ya mtoto na mwendawazimu inaweza kuingia katika matumizi na kulipia faini, kwa hiyo isibanwe kwa kutotolewa Zakaah.

 

- Zakaah ni haki ya mwanadamu, hivyo wajibu wa kuitoa uko sawa kwa mukallaf na asiye mukallaf.

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu. Na juu ya msingi huu, msimamizi wa mali zao atawatolea Zakaah kutoka mali hizo, kwa kuwa ni waajib.

 

Shuruti za mali ili iwajibikiwe na Zakaah

 

Ili mali iwajibikiwe na Zakaah, ni lazima iwe na shuruti zifuatazo:

 

1- Iwe ni katika sampuli (aina) ambazo ni lazima kuzitolea Zakaah. Hili litachambuliwa mbeleni.

 

2- Ifikie kiwango, nacho ni kiasi ambacho kikitimia, Allaah Amekiwekea uwajibu wa kukitolea Zakaah. Mtu ambaye hana kiwango hicho na akamiliki kilicho chini yake, au kamwe hakumiliki chochote, basi hawajibikiwi na Zakaah. Na hili linatofautiana kwa mujibu wa aina ya mali kama tutakavyobainisha mbeleni.

 

3- Mali iwe inamilikiwa umiliki kamili usio na shaka. Na dalili ya sharti hii, ni kunasibishwa mali kwa wamiliki wake kwenye Qur-aan na Hadiyth. [Fiqhu Az-Zakaah cha Al-Qaradhwaawiy (1/150)]

 

Ni kama katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗوَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ))

((Chukua katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.)). [At-Tawbah (9:103)]

 

Na Kauli Yake:

((وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ ))

((Na wale ambao katika mali zao kuna haki maalumu.)). [Al-Ma’aarij (70:24)]

 

Na neno lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((إن الله فرض عليهم في أموالهم))

((Hakika Allaah Amewafaradhia katika mali zao)).

 

Hii ni kwa kuwa Zakaah ni umilikishaji wa mali kwa wastahiki wake, na umilikishaji ni sehemu itokanayo na milki, na kwa hivyo ni lazima Zakaah itoke kwenye milki ya mtoaji.

 

‘Ulamaa wamevutana: Je, milki ni ya kuhodhi (kuwa nayo mkononi)? Ya kuyasarifu (kuyatumia)? Au asili ya milki? [Angalia Majmuw’u Al-Fataawaa (25/45)]

 

 

 

 

Share