Wanawake Kuvaa Nguo Wazi Fupi, Zisizo Na Sitara Mbele Ya Wanawake Wenzao Wakiwa Harusini

 

Wanawake Kuvaa Nguo Wazi Fupi, Zisizo Na Sitara Mbele Ya

Wanawake Wenzao Wakiwa Harusini

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je, wanawake wanaruhusika kuvaa nguo za wazi zisizositiri baadhi ya mwili kama kanzu fupi zinazoonyesha miguu au mikono yote kuwa wazi au kuvaa bega na moja liko wazi, baadhi ya au kifua kuwa wazi, au kanzu kumbana (tight) hadi mwili wote viungo vyake vinaonekana, au mgongo kuwa wazi wakiwa na wanawake wenzao kama vile harusini?

  

Je ni kweli awrah (uchi)  ya wanawake mbele ya wanawake wengine ni kutoka kitovu cha magoti?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayahi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza tambua kwamba mwanamke mwili wake wote ni 'awrah mbele ya wanaume ambao si Mahram zake (anayeweza kumuoa), na haijuzu kwake kuonekana mbele ya wanaume hata kama atakuwa ni mwenye kujisitiri, kwa kuhofia fitnah kwa kumuangalia na kuona jinsi ni alivyo na jinsi anavyotembea.  Amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]

 

 

Pili kuhusiana na lililosemwa kuhusu 'awrah ya mwanamke mbele ya wanawake wenziwe kuwa ni kutoka kitovu hadi magoti, hii inatumika tu wakati atakuwa kwenye nyumba yake miongoni mwa dada zake na wanawake ambao anaishi nao.

 

 

Shariy’ah bado zinasisitiza asitiri mwili wake wote ili achukuliwe kama kiigizo bora na haya mazoea maovu yameenea miongoni mwa wanawake. Vile vile, anapaswa kusitiri uzuri wake mbele ya mahram wake na wanawake wageni ili baadhi ya mahram wake wavutiwe (waathirike) nae kitabia na adabu, au ili baadhi ya wanawake wasije kwenda kumuelezea yeye wasifu wake kwa wengine (wanaume). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رضى الله عنه قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ لاَ تُبَاشِرِ الْمَرْأَةُ الْمَرْأَةَ فَتَنْعَتَهَا لِزَوْجِهَا، كَأَنَّهُ يَنْظُرُ إِلَيْهَا ‏"‏‏.‏ البخاري

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya-Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Haitakiwi mwanamke kumuelezea mwanamke mwengine kwa mume wake, hivyo ni kama (mumewe) anamuona yeye" [Al-Bukhaariy]

 

 

Kinachomaanishwa ni kuwa uzuri wake, kama vile kifua chake, mabega yake, tumbo lake, nyuma, mikono yake, shingo yake na ndama yake inakuwa wazi, kila mtu anaona kwamba ni jambo lisiloweza kuepukwa, mtu kuwa na hisia yake.

 

 

Na ni kawaida wanawake huelezea juu wa waliyoyaona kwa familia zao, sawa wanamume na wanawake. Hivyo mwanamke anaweza kutaja hayo mbele ya watu ambao si Mahram wake, kwa namna ambayo inaweza kuwafanya wao kuvutiwa kwake [huyo mwanamke], au ambayo inaweza kusababisha watu wabaya kutafuta njia kuanzisha uhusiano naye.

 

 

Kwa sababu hii, wanawake wanatakiwa kufunika 'awrah [sehemu zisizotokiwa kuonekana katika miili] yao - kama vile vifua vyao, migongo, mikono, ndama, n.k, - vile vile hata mbele ya mahram wake na wanawake wengine.

 

 

Kujisitiri huku kunakuwa muhimu zaidi katika sehemu za makundi, maeneo ya sherehe, hospitali, na mashule, hata kama kutakuwepo wanawake tu, kwa sababu baadhi ya wanaume ambao si Mahram na hata vijana wanaweza kuwaona au kuwachukua picha hali ya kuwa hawana stara zao kamili, na hiyo  itakuwa ni sababu ya fitnah kwa wale wanaowaona.

Onyo kali imetolewa kwa wale [wanawake] ambao wanajionyesha na wavaao nguo za kuonyesha au za kubana, wakati Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliposema katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا: قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ، وَنِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلاَتٌ مَائِلاَتٌ رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ، لاَ يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلاَ يَجِدْنَ رِيحَهَا، وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah(رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Aina mbili za watu wa motoni sijawaonapo [hawapo katika zama zangu]: Watu walio na mijeledi mfano wa mikia ya ng’ombe wanawapiga watu kwa mijeledi hiyo [kwa dhulma], na wanawake waliovaa nguo na ilhali wako uchi, wakitembea kwa maringo huku wakiyanyonga mabega yao na wakiwafunza wengineo kutenda kama hivyo, vichwa vyao ni kama nundu za ngamia-bukhti wanaodemadema. Hawatoingia Jannah wala hawataisikia harufu yake, na kwa hakika harufu yake husikika umbali kadha wa kadhaa)). [Muslim]

 

 

Kinachomaanishwa ni kwamba wamevaa nguo za kuonyesha au nguo za kubana ambazo zinaonyesha maumbile yao, au kunapokuwepo fursa ya ajira kwenye kampuni ambayo [mavazi yao] huonyesha vifua vyao, matiti yao na sehemu zingine zisizofaa kabisa kuonekana. Hili limeenea katika makundi na katika mikusanyiko ya ujumla yote. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share