14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaa Ya Mifugo

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

14-Zakaah Ya Mifugo

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Aina Za Wanyama Ambao Hutolewa Zakaah

 

‘Ulamaa wote kwa pamoja wanasema kuwa Zakaah hutolewa kwa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wametolea dalili hili kwa Hadiyth nyingi ambazo baadhi yake zitatajwa mahala pake husika, In Shaa Allaah.

 

Lakini wamekhitalifiana kwa upande wa farasi. [Al-Mughniy (2/620), Fat-hul Qadiyr (1/502), Sharhu Al-Minhaaj (2/3), na Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/262]

 

Jumhuri, wakiwemo Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah– wanaona kuwa farasi wasio wa biashara, hao hawatolewi Zakaah– (hata kama wanajilia majani yasiyogharamikiwa au wakafugwa ili wazaliane) ni sawa wakiwa wanafanyishwa kazi au hawafanyishwi.

 

Madhehebu yao haya yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:

 

((ليس على المسلم في فرسه وغلامه صدقة))

((Si waajib juu ya Muislamu Zakaah kwa farasi wake na mtumwa wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1464) na Muslim (628)]

 

Lakini Abu Haniyfah anaona kwa mbinde kuwa farasi ikiwa wanajilia majani yasiyogharamikiwa madume na majike, basi watatolewa Zakaah. Na kama ni madume tu, basi Zakaah hakuna kwa kuwa hawazaani, na kadhalika majike tu. Ametoa dalili Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:

 

((الخيل لرجل أجر، ولرجل ستر، وعلى رجل وزر....[وفيه] ولم ينس حق الله في رقابها، ولا ظهورها))

((Farasi kwa mtu ni thawabu, kwa mtu ni sitara, na juu ya mtu ni dhambi…[Hadiyth ikaendelea kusema] na hakusahau haki ya Allaah katika shingo zake, wala migongo yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2371) na Muslim (987)]

 

Amesema: “Haki ya shingo ni Zakaah”.

 

Ama wanyama wengineo kama nyumbu, punda na kadhalika, hao hawana Zakaah madhali si wa biashara. Ni kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) katika Hadiyth ya: ((Farasi kwa mtu ni thawabu…)) alipoulizwa kuhusu punda akasema: ((Sijateremshiwa chochote kuhusiana naye isipokuwa Aayah hii ya kipekee:

 

((فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ))

((Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe (atom) ataiona)). [Al-Zalzalah (7:99)]

Shuruti za kuwajibisha Zakaah kwa mifugo

 

1- Kiwango ambacho tutakibainisha mbeleni.

 

2- Kukamilika mwaka. Ni kwa Hadiyth: ((Hakuna Zakaah katika mali mpaka ipitiwe na mwaka)). [Hadiyth iliyotangulia]

 

3- Wachungwe na kulishwa muda mwingi wa mwaka kwenye malisho halali yasiyo na gharama.

 

Vigawanyo vya mifugo

 

Mifugo (ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo) inaweza kugawanywa vigawanyo vinne:

 

1- Wenye kuchungwa na kulishwa kwenye malisho halali yasiyo na gharama muda mwingi wa mwaka, na wawe wametayarishwa kwa ajili ya maduhuli na kuzaana. Ni kama Alivyosema Ta’aalaa:

((وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُون))

((na [mnaotesha] miti ambayo mnalishia)). [An-Nahl (16:10)]

 

Hawa wanalazimu kutolewa Zakaah.

 

2- Wenye kulishwa majani yanayogharamikiwa. Hawa hata kama wanafugwa kwa ajili ya maduhuli na kuzaana, lakini mmiliki wake anawanunulia majani au anawakatia, basi hawatolewi Zakaah.

 

3- Wenye kufanyishwa kazi. Ni kama ngamia ambao mmiliki wake anawakodishia watu ili kubeba mizigo au kupandwa, au ng’ombe wa kulima na kunyweshelea maji. Hawa hawana Zakaah kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri kinyume na Maalik. [Sharhu Fat-hil Qadiyr (1/509) na Al-Mughniy (2/576)]

 

4- Wenye kufugwa kwa lengo la biashara. Hawa watatolewa Zakaah kama mali za biashara. Ngamia mmoja anaweza kulazimu kutolewa Zakaah kama thamani yake itafikia kiwango, sawasawa akiwa anakula majani ya bure, au ya kununuliwa, au wa kupandwa.

 

 

 

 

Share