19-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Mali na Bidhaa Za Biashara
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Zakaah
19-Zakaah Ya Mali na Bidhaa Za Biashara
Mali na bidhaa za biashara ni bidhaa zote isipokuwa dhahabu na fedha (silver). Ni kama mizigo, ardhi, viwanja na majumba (real estate), wanyama wa aina tofauti, mazao, mavazi, vyombo, vito vya thamani na mfano wake ambazo ni kwa ajili ya biashara.
Wengine wamezifasili bidhaa kama ni kila kilichotayarishwa kwa ajili ya kuuza na kununua kwa lengo la kupata faida.
Hukmu Ya Zakaah Katika Mali Na Bidhaa Za Biashara
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu Zakaah hii katika kauli mbili: [Angalia Fiqhu Az Zakaah (1/340) na baada yake, na vitabu vingine vilivyoashiriwa baadaye]
Kauli ya kwanza:
Ni lazima zitolewe Zakaah. Ni kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. Na wengine wameeleza kuwa ni Ijma’a ya Swahaba na Taabi’iyna kama tutakavyokuja kueleza mbeleni. Wametolea dalili Qur-aan, As-Sunnah, Athari za Swahaba na Taabi’iyna pamoja na Qiyaas.
(a) Kutoka kwenye Qur-aan ni Kauli Yake Ta’aalaa:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ))
((Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi)). [Al-Baqarah (2:267)]
Al-Bukhaariy amelihusishia suala hili mlango maalum katika Kitaab Az Zakaah katika Swahiyh yake akisema: (Mlango Wa Zakaah Ya Chumo Na Biashara). Na maana ya Kauli Yake (مَا كَسَبْتُمْ) ni biashara. [Angalia Tafsiyr At-Twabariy (5/555), Ahkaamul Qur-aan cha Ibn ‘Arabiy (1/235) na wengineo]
(b) Na kutoka kwenye As-Sunnah:
Ni Hadiyth ya Samrah bin Jundub aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akituamuru tutoe Zakaah ya vitu tunavyoviandaa kwa kuuza)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Abu Daawuud (1562), na kutoka kwake Al-Bayhaqiy (1/97), Ad-Daaraqutwniy (uk. 214) na wengineo kwa Sanad Dhwa’iyf. Angalia Al-Irwaa (827)]
Na kwa Hadiyth Marfuw’u ya Abu Dharri:
((في الإبل صدقتها، وفي الغنم صدقتها، وفي البز صدقته))
((Katika ngamia kuna Zakaah yake, katika mbuzi na kondoo kuna Zakaah yake, na katika nguo kuna Zakaah yake)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ahmad (5/179), Al-Bayhaqiy (4/147) na Ad-Daaraqutwniy. Angalia Adh-Dhwa’iyfah (1178)]
Nguo hapa ni pamoja na vitambaa, mashuka, matandiko, vyombo na mfano wake. Na vitu hivi vikiwa vya matumizi binafsi, basi havina Zakaah bila mvutano wowote. Hivyo, muradi wa kutolewa Zakaah ni kuwa tu viwe vinatumika kwa faida na biashara.
Tatizo hapa ni kuwa Hadiyth hizi mbili ni Dhwa’iyf. Lakini dalili ya kupasa kutoa Zakaah kwa mali na bidhaa za biashara inapatikana katika ujumuisho wa maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa Mu’aadh:
((أعلمهم أن الله افترض عليهم صدقة من أموالهم))
((Wajulishe kuwa Allaah Amewafaradhishia Zakaah kutokana na mali zao..)). [Takhriyj yake ishadokezwa nyuma]
Bidhaa za biashara ni mali bila shaka yoyote, na hii ni kwa kuingia ndani ya mjumuisho wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam): ((Hakika amali ni kwa niya….)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1), na Muslim (1907)]
Kwani hakika, mfanyibiashara akiulizwa: “Unataka nini kwa biashara?” Atasema: “Dhahabu na fedha (silver)?!” [Imenukuliwa toka Ash-Sharhu Al-Mumti’u (6/141)]
Na hili linatolewa dalili vile vile na Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusiana na Khaalid bin Al-Waliyd kukataa kutoa Zakaah na watu kulilalamikia hilo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
((وأما خالد، فإنكم تظلمون خالدا، قد احتبس أدراعه وأعتده في سبيل الله...))
((.. ama Khaalid, hakika nyinyi mnamdhulumu Khaalid, hakika yeye amezifungia ngao zake na zana zake za vita katika Njia ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1468) na Muslim (983)]
Ni kana kwamba walidhani kuwa ngao na zana hizo ni kwa ajili ya biashara, wakamtaka atoe Zakaah kwa thamani zake. Na Rasuli (‘alayhis Swalaat was salaam) akawajulisha kuwa hakuna Zakaah kwa Khaalid kwa kile alichokifungia. [Angalia Fat-hul Baariy (3/392). Na amesema: Na hii inahitaji nukuu maalum ili iwe na hujja]
(c) Na kutoka kwenye aathaar za Swahaba na Watangu Wema:
1- Ibnu ‘Abdil Qaariy amesema: ((Nilikuwa mweka hazina wa Baytul Maal enzi za ‘Umar bin Al-Khattwaab. Alikuwa unapowadia wakati wa watu kutoa Zakaah, anakusanya mali za wafanyibiashara na kuzipiga hesabu; mali taslimu na mali zisizo taslimu [mifugo, mashamba n.k]. Kisha anachukua Zakaah ya mali taslimu na mali isiyo taslimu)). [Al-Amwaal, Muswannaf Ibn Abiy Shaybah na Al-Muhallaa. Ibn Hazm kasema ni Swahiyh na ameiawilisha]
2- Ibn ‘Umar kasema: ((Hakuna Zakaah katika vitu isipokuwa kwa vile vya biashara)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Ash-Shaafi’iy ameikhariji katika Al-Ummu (2/68), ‘Abdur Raaziq (4/97), na Al-Bayhaqiy (4/147) kwa Sanad Swahiyh]
3- Ibn ‘Abbaas amesema: ((Hakuna ubaya kufuatilia na kusubiri mpaka amalize mauzo, na Zakaah ni waajibu ndani yake)). [Al-Amwaal (uk. 426), na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (5/234). Isnaad Yake kasema ni Swahiyh lakini kaiawilisha]
4- ‘Atwaa amesema: ((Hakuna Zakaah katika lulu, wala zubarjad (aquamarine), wala yakuti (ruby), wala vistoni vya vito, wala bidhaa, wala kitu kisichofanyiwa biashara. Na ikiwa kuna chochote katika hivyo kinafanyiwa biashara, basi kuna Zakaah ndani yake katika thamani yake wakati kinapouzwa)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abdur Razzaaq (7061) na Ibn Abiy Shaybah (3/144) kwa Sanad Swahiyh]
5- ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz alimwandikia Zurayq akimwambia: ((Angalia waliopita kwako kati ya Waislamu. Chukua kinachoonekana katika mali zao katika vitu wanavyovifanyia biashara dinari moja katika kila dinari 40..)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (594) na Ash-Shaafi’iy katika Al-Ummu (2/68)]
Na hakikunukuliwa kutoka kwa yeyote katika Swahaba chochote chenye kukhalifiana na kauli ya ‘Umar, mwanaye na Ibn ‘Abbaas, bali kazi na fatwaa ziliendelea juu ya hilo katika enzi ya Taabi’iyna na enzi ya ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz. Aidha, Fuqahaa wa Taabi’iyna na waliofuatia baada yao, wameitafikiana juu ya kauli inayowajibisha Zakaah katika mali za biashara.
Hata Ibn Al-Mundhir na Abu ‘Ubaydah wamenukuu Ijma’a juu ya hilo isipokuwa kauli moja tu ambayo Abu ‘Ubaydah ameitaja na hakuinasibisha kwa msemaji yeyote. Kisha ‘Uqbah akasema: “Ama kauli nyingine, si katika madhehebu ya ‘Ulamaa kwetu sisi”.
(d) Ama Qiyaas:
Ni kuwa bidhaa zenye kufanyiwa biashara, ni mali zinazokusudiwa kuzalisha faida. Hivyo zinafanana na aina tatu ambazo ni lazima zitolewe Zakaah (dhahabu na fedha, mifugo na mazao).
(e) Ama kwa upande wa kinadhari na kimazingatio:
- Ni kuwa bidhaa za biashara zinazoingia kwenye mzunguko wa soko kwa ajili ya kuuzwa, zinakuwa ni pesa kimaana. Hakuna tofauti kati yake na dirhamu na dinari ambazo ni thamani zake, isipokuwa katika kuwa kiwango kinapanda na kushuka na kubadilika kati ya thamani ambayo ni pesa na kinachotiwa thamani ambacho ni bidhaa. Na lau kama Zakaah si waajib katika mali za biashara, basi matajiri wote au wengi wao wangeliweza kufanya biashara kwa kutumia pesa zao, na wangelipania kiwango cha dhahabu na fedha kisipitiwe kamwe na mwaka, na hivyo Zakaah ingelikwama kwao katika viwili hivyo. [Tafsiyr Al-Manaar ya Rashiyd Ridhwaa (10/591)]
- Watu wanaohitajia zaidi kujitakasa wenyewe pamoja na mali zao na kuzisafisha, ni wafanyibiashara, kwani njia zao za uchumaji mali hazisalimiki na ghushi na ufisadi.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:
(( يا معشر التجار، إن البيع يحضره اللغو والحلف، فشوبوه بالصدقة))
((Enyi jumuiya ya wafanyabiashara! Hakika biashara inaingiliwa na upuuzi na uapaji, basi yachanganyeni hayo kwa Zakaah)). [Abu Daawuwd (3326), At-Tirmidhiy (1208), An-Nasaaiy (3797) na Ibn Maajah (2145). Ni Hadiyth Swahiyh]
Faida
Ibn Al-Mundhir, Abu ‘Ubayd, na kundi la ‘Ulamaa wamenukuu Ijma’a juu ya uwajibu wa Zakaah kwa bidhaa za biashara. Hili linahitajia kuhakikiwa upya, kwa kuwa mvutano katika suala hili ni wa kale –kama alivyoeleza Ash-Shaafi’iy na wengineo- lakini Adh-Dhwaahiriyyah wamesema kinyume na hayo kama itakavyokuja kuelezwa mbeleni. [Al-Ijma’a (14) na Al-Amwaal (429). Angalia pia Al-Majmuw’u (6/47), Bidaayatul Mujtahid (1/254), Ar-Rawdhwatu An Naddiyyah (1/286) na Muswannaf Ibn Abiy Shaybah (3/36,44) chapa ya Al-Fikr]
Kauli ya pili:
Si lazima zitolewe Zakaah. Ni madhehebu ya Adh-Dhwaahiriyyah na walioungana nao kama Ash-Shawkaaniy, Swiddiyq Khaan, kisha Al-Albaaniy. Ibn Hazm katika kitabu chake cha Al-Muhalla ameienzi kauli yao na kuwatetea, na akakamia katika kutengua madhehebu ya Jumhuri.
Kati ya dalili zao ni:
1- Hadiyth
(( ليس على مسلم في عبده ولا فرسه صدقة))
((Hakuna Zakaah kwa Muislamu katika mtumwa wake wala farasi wake)). [Al-Bukhaariy (1464) na Muslim (628)]
Udhahiri wake ni kuwa hakuna uwajibu wa Zakaah sawasawa ikiwa ni kwa biashara au kwa jinginelo.
Jumhuri wamewajibu wakisema kuwa kusudio ni kukanusha Zakaah kwa mtumwa wake anayemtumikia na farasi wake anayempanda, na hao wawili ni katika mahitajio ya asili yanayosamehewa Zakaah kwa Ijma’a.
2- Mali ya Muislamu kiasili haibebeshwi wala kufungamanishwa na makalifisho yoyote, na uasili huu unabakia kama ulivyo ikiwa hakuna dalili ya kuubadilisha. Na nyuma tushasema kuwa Ijma’a ya Swahaba imethibitisha uwajibu wa Zakaah kwa bidhaa za biashara.
3- Hadiyth ya Qays bin Abiy Gharazah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alitoka kutufuata na sisi tunauza watumwa tukiitwa madalali. Akasema: ((Enyi jumuiya ya wafanyabiashara! Hakika mauzo yenu haya yanachanganyika na upuuzi na uapaji, basi yachanganyeni na Zakaah, au na kitu kidogo cha swadaqah))”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (4/6), An-Nasaaiy (7/14), Abu Daawuud, At-Tirmidhiy (1208), Ibn Maajah (2154) na wengineo]
Ibn Hazm amesema: “Na hii ni swadaqah ya faradhi isiyo na mpaka, lakini kwa ambazo roho zao zimeridhia, na inakuwa ni kafara kwa yale yanayochanganyika ndani yake katika mambo yasiyofaa kama upuuzi na kuapa”.
Na mengineyo kati ya pingamizi na migogoro ambayo Ibn Hazm ameiibua kwenye Al-Muhalla (5/233) na kurasa zinazofuatia. Na kauli ya Jumhuri ndiyo sahihi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Shuruti za Zakaah katika mali ya biashara
Ili mali iliyoandaliwa kwa ajili ya kupata faida na biashara iwajibikiwe na Zakaah, ni lazima iwe na shuruti zifuatazo:
1- Mali isiwe kiasili ni katika zinazolazimu Zakaah kama mifugo, dhahabu, fedha na mfano wake, kwa kuwa kwa mujibu wa Ijma’a, Zakaah mbili hazikusanyiki pamoja. [Angalia Al-Majmuw’u (6/50) na Al-Mughniy (3/34)]
2- Ifikie kiwango, nacho ni thamani ya gramu 85 za dhahabu.
3- Ipitiwe na mwaka.
Ni wakati gani kiwango cha mali ya biashara kinaangaliwa?
Kuna kauli tatu kuhusiana na hili:
1- Mwisho wa mwaka (Ni kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy).
2- Mwaka wote, kwa maana, kiwango kikipungua muda mchache, basi mwaka unakatika (Ni madhehebu ya Jumhuri).
3- Mwanzo wa mwaka na mwisho wake (Ni madhehebu ya Abu Haniyfah).
Vipi mfanyabiashara anaitolea Zakaah mali yake ya biashara?
Unapofika muda wa Zakaah, mfanyabiashara atazikusanya mali zake zote. Mali hizi ni:
1- Mtaji, faida, akiba na thamani ya bidhaa zake.
2- Madeni anayotarajia kulipwa.
Atakokotoa thamani ya bidhaa zilizopo, kisha ataijumlisha na pesa zilizopo pamoja na madeni ambayo ana uhakika mkubwa wa kulipwa, halafu atatoa kando madeni anayodaiwa.
Baada ya kufanya hivi, atatolea vyote hivyo robo ya kumi (2.5%) kwa mujibu wa bei ya wakati wa kutoa Zakaah, na si kwa bei ya kununulia bidhaa.
Hii ndio rai ya Jumhuri ya Fuqahaa. Maalik ameungana nao katika hili kwa mfanyabiashara mwenye kuendesha shughuli za ununuzi na uuzaji.
Lakini amesema kuhusu mfanyabiashara (mlanguzi) ambaye ananunua bidhaa au viwanja, kisha anaziweka, anasubiri na anafuatilia mwenendo wa soko mpaka bei ipande ndipo auze, amesema kwamba huyu hatoi Zakaah isipokuwa kama atauza bidhaa. Bidhaa hiyo ataitolea Zakaah ya mwaka mmoja tu hata kama alibaki nayo kwa miaka mingi.
Je, ni bidhaa zenyewe zinazotolewa kwa Zakaah au thamani yake?
Jumhuri wanasema ni waajib kutoa thamani, na haijuzu kutoa bidhaa yenyewe, kwa kuwa kiwango cha Zakaah hutathminiwa kwa thamani, na Zakaah kutokana na thamani hiyo imekuwa ni kama kitu katika mali nyinginezo.
Lakini Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy –katika moja ya kauli zake- wanaona kuwa mfanyabiashara ana khiyari ya kutoa bidhaa au thamani ya bidhaa. [Al-Badaai (2/21) na Al-Mughniy (3/31)]
Ama Sheikh wa Uislamu, yeye amekhiyari kuwa pande zote mbili ni sawa kwa mujibu wa unafuu kwa mpewa Zakaah. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/80)]