22-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Maswaarif Za Zakaah (Wastahiki Wa Kupewa Zakaah)
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Zakaah
22-Maswaarif Za Zakaah (Wastahiki Wa Kupewa Zakaah)
Maswaarif za Zakaah zimeainishwa katika aina nane tu, na aina hizi nane zimetajwa na Al-Qur-aan Al-Kariym katika Kauli Yake Ta’aalaa:
((إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ))
((Hakika Zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia, na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (katika Uislamu) na kuwakomboa mateka, na wenye deni na katika Njia ya Allaah na msafiri (aliyeharibikiwa). Ni faradhi itokayo kwa Allaah. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote)). [At-Tawbah (9:60)]
انما Ambayo imeanziwa kwayo Aayah, ni neno la kudhibiti kitajwa kisiingie kingine, hivyo basi haijuzu kupewa Zakaah yeyote ambaye hayumo ndani ya aina hizi.
Je, Ni Lazima Aina Hizi Nane Wapewe Wote, Au Inajuzu Kupewa Baadhi Yao Tu?
Jumhuri ya ‘Ulamaa (Abu Haniyfah, Maalik, Hanbali na kundi la Masalaf akiwemo ‘Umar na Ibn ‘Abbaas) wanaona si lazima aina hizi nane kupewa wote katika mali ya Zakaah, bali yajuzu kupewa mmoja tu kati yao, na kumpa swadaqah pamoja na kuwepo wengine.
Wametoa hoja kwa yafuatayo:
1- Kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((تاخذ من أغنيائهم فترد على فقرائهم))
((Huchukuliwa toka kwa matajiri wao na hurejeshwa kwa mafakiri wao)). [Muttafaqun ‘Alayhi. Imetajwa nyuma mara nyingi]
Wamesema: Mafakiri ni aina moja kati ya aina za wastahiki nane wa Zakaah.
2- Yaliyosimuliwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwapa watu Zakaah kama Hadiyth ya Qabiyswah bin Makhaariq alipokopa deni kubwa (la kudhamini suluhu kati ya watu) na akamjia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kumwomba Zakaah, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia:
((أقم حتى تأتينا الصدقة فنأمر لك بها))
((Kaa mpaka itujie Zakaah, kisha tuamuru upewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1044)]
Kuna matukio mengine ambayo baadhi yake yametajwa nyuma.
Lakini Ash-Shaafi’iy na kundi jingine wanasema kuwa ni lazima mgawo wa Zakaah uwaenee wote wa aina hizi nane. Abu Thawr na Abu ‘Ubayd wamesema: Ikiwa kiongozi mhusika atagawa Zakaah, basi ni lazima agawe kwa aina zote, lakini mmiliki wa mali akitoa, basi inajuzu kuitoa kwa aina moja tu. [Al-Majmuw’u (6/185), Al-Mughniy (2/668) na Al-Amwaal cha Abu ‘Ubayd (uk. 692)]
[1,2] Mafukara na masikini
Mafukara na masikini ni watu wahitaji wasiopata cha kuwatosheleza. Linapotajwa neno mafukara peke yake, basi huingia pamoja nao masikini, na pia kinyume chake. Na kama yatatajwa yote mawili katika sentensi moja kama katika Aayah ya wastahiki, basi kila moja litakuwa na maana tofauti na mwenzake.
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu nani kati ya wawili ni mhitaji zaidi kuliko mwingine. Ash-Shaafi’iy na Hanbali wanasema kuwa fakiri ni mhitaji zaidi kuliko masikini. Dalili yao wanasema kuwa Allaah Amewataja kwanza wao katika Aayah, na hii ni dalili kuwa wao ndio muhimu zaidi. Pia kwa Neno Lake Ta’aalaa:
((أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ))
((Ama jahazi, ilikuwa ya masikini wanaofanya kazi baharini)). [Al-Kahf (18:79)]
Hapa Amewathibitishia sifa ya umasikini pamoja na kuwa wanamiliki jahazi na wanapata nauli.
Kadhalika, wamejiridhisha na hilo pia kutokana na mnyambuliko (wa neno). “Al-Faqiyr” (الفقير)katika lugha liko katika wazni wa “Fa’iyl” (فعيل) kwa maana ya mtendwa, naye ni mtu aliyeondolewa baadhi ya pingili za uti wake wa mgongo, na mgongo wake ukakatika. Na “Al-Miskiyn” (المسكين) liko katika wazni wa “Mif-‘iyl” (مفعيل) kutokana na neno “As-Sukuwn” (السكون) [kutulia]. Na mtu ambaye uti wake wa mgongo umevunjika anakuwa mhitaji zaidi kuliko “As-Saakin” (aliyetulia).
Lakini Hanafiy na Maalik wanaona kuwa masikini ni mhitaji zaidi kuliko fakiri. Dalili yao wanasema kuwa Allaah Mtukufu Anasema:
(( أَوْ مِسْكِينًا ذَا مَتْرَبَةٍ))
((Au maskini aliye hohehahe)). [Al-Balad (90:16]
Huyu ni masikini aliyetupwa juu ya udongo kutokana na njaa kali. Pia wanasema vigogo wa lugha wamesema hilo akiwemo Al-Farraai, Tha-‘alab na Ibn Qutaybah. Aidha, kutokana pia na mnyambuliko, kwani masikini linatokana na neno “As-Sukuwn” (kutulia) kana kwamba ameshindwa kusogea na kubakia pale alipo. Ad-Dusuwqiy amenukulu kauli isemayo kuwa fakiri na masikini ni mtu huyo huyo mmoja, naye ni ambaye hana chakula cha mwaka wake, sawasawa akiwa hana kitu kabisa, au ana chakula kidogo cha kumtosheleza mwaka mzima.
Fuqahaa wamekhitalifiana kuhusu mpaka (wa kipato) kwa masikini na fakiri
[Al-Mawsuw-’at Al-Fiqhiyyat (23/312)]
Ash-Shaafi’iy na Hanbali wanasema kuwa fakiri ni mtu asiye na mali wala kipato kinachokidhi mahitaji yake. Ni kama mtu ambaye anahitajia kumi na hapati chochote kabisa, au yule ambaye kwa mali yake, kipato chake na anachokipata kutokana na ardhi yake na kinginecho, anaweza kupata chini ya nusu ya mahitaji yake. Na ikiwa anapata nusu au zaidi lakini hapati kumi kamili, basi huyo ni masikini.
Hanafy na Maalik kwa upande wao wanasema masikini ni yule ambaye hana kitu asilani akahitajia kuomba, na huyu kuomba ni halali kwake. Lakini kwa upande wa fakiri wametofautiana. Hanafiy anasema: Fakiri ni yule mwenye kitu kidogo ambacho hakifikii kiwango (cha Zakaah). Ikiwa atamiliki kiwango kutoka mali yoyote ya Zakaah, basi huyo ni tajiri hastahiki kupewa chochote katika Zakaah. Na akimiliki chini kidogo ya kiwango, basi si mstahiki. Vile vile akimiliki kiwango ambacho hakiongezeki, nailhali ametingwa na mahitaji ya kimsingi (atapewa), na kama hakutingwa atazuiliwa. Ni kama mwenye nguo zenye thamani sawa na kiwango (cha Zakaah) ambazo hazihitajii, basi Zakaah ni haramu kupewa. Na ikiwa thamani ya anavyovimiliki itafikia kiwango, basi hilo halizuii yeye kuwa katika wastahiki wa Zakaah ikiwa thamani itatosheleza mahitaji asili. Ni kama mwenye vitabu anavyovihitaji kufundishia, au zana za kazi na mfano wa hivyo.
Maalik amesema: Fakiri ni yule ambaye anamiliki kitu ambacho hakimtoshi kwa chakula chake cha mwaka.
Utajiri unaozuia kupewa Zakaah kwa mujibu wa picha ya ufakiri na umasikini:
Haijuzu kiasli tajiri kupewa Zakaah. Hii ni itifaki ya ‘Ulamaa kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((لا حظ فيها لغني))
((Hakuna fungu ndani yake kwa tajiri)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1633) na An-Nasaaiy (2598)]
Lakini wamekhitalifiana kwa upande wa utajiri wenye kuzuia mtu kuchukua Zakaah. Jumhuri ya ‘Ulamaa wa madhehebu ya Maalik na Ash-Shaafi’iy, na riwaya ya Ahmad ambayo maswahibu zake waliofuatia baadaye waliikadimisha, wamesema: “Jambo linazingatiwa kwa kujitosha. Atakayepata pesa au kinginecho kinachomtosha na kuwatosha anaowakimu, basi huyo ni tajiri ambaye Zakaah si halali kwake. Na kama hakupata hilo, Zakaah itakuwa ni halali kwake hata kama alichonacho kitafikia viwango vya Zakaah. Na juu ya msingi wa haya, haizuii kuwepo mtu ambaye anawajibika kutoa Zakaah na wakati huo huo akawa mstahiki wa kupewa Zakaah”.
Mahanafiy wamesema: “Huo ni utajiri wenye kuwajibisha Zakaah. Hivyo, anayewajibikiwa Zakaah, si halali kwake achukue Zakaah kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam): ((Hakika Allaah Amewafaradhia Zakaah, inachukuliwa toka kwa matajiri wao ikarudishwa kwa mafukara wao)).
Na mwenye kumiliki kiwango katika mali yoyote ya kutolewa Zakaah, basi huyo ni tajiri, haijuzu kupewa Zakaah hata kama alichonacho hakimtoshi kwa mwaka. Na ambaye hamiliki kiwango kamili, basi huyo ni fakiri au masikini inajuzu kumpa Zakaah kama ilivyotangulia”.
Na katika riwaya nyingine ya Mahanbali ambayo ina nguvu zaidi katika madhehebu yao ni kuwa akipata cha kumtosha, basi huyo ni tajiri, na kama hakupata na akawa na dirhamu 50, au thamani yake katika dhahabu, basi huyo ni tajiri hata kama haimtoshi. Na hii ni kwa Hadiyth isemayo:
((من سأل الناس وله ما يغنيه جاء يوم القيامة ومسألته في وجهه خموش أو خدوش أو كدوح. قالوا يا رسول الله وما يغنيه؟ قال: خمسون درهما أو قيمتها من الذهب))
((Mwenye kuomba watu naye anacho kinachomtosheleza, atakuja Siku ya Qiyaamah na (athari ya) ombaomba zake. Katika uso wake makovu, au mikwaruzo au mabaka”. Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni kipi kinamtosheleza? Akasema: Dirhamu 50 au thamani yake ya dhahabu)) [Kuna mvutano katika Sanad yake. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (650) na Ibn Maajah (1840)]
Na bila shaka wamepambanua kati ya thamani na vinginevyo kufuata Hadiyth.
Je, inajuzu kumpa Zakaah fakiri au masikini mwenye uwezo wa kufanya kazi na kulipwa?
Mtu yeyote fakiri au masikini mwenye kuweza kupata kipato cha kumtosha yeye na kuwatosha anaowakimu, au kuwatosheleza na kuzidi, basi si halali kwake kuchukua Zakaah. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
(( لا حظ فيها لغني ولا لقوي مكتسب))
((Hakuna fungu ndani yake kwa tajiri wala kwa mwenye nguvu mwenye kuweza kupata kipato)). [Abu Daawuwd (1617) na An-Nasaaiy (5/99). Al-Albaaniy kasema Swahiyh]
Na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
(( لا تحل الصدقة لغني ولا لذي مرة سوي))
((Si halali Zakaah kwa tajiri wala kwa mwenye nguvu mzima wa afya)). [At-Tirmidhiy (647) na Abu Daawuwd (1618). Angalia Swahiyh Al-Jaami’i (7251)]
Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali, nayo ndiyo yenye nguvu.
Lakini Hanafiy na Maalik, wao wanasema kuwa inajuzu kupewa madhali ni fakiri na masikini. Wametoa dalili kutoka kwenye mnasaba wa kisa cha Hadiyth tuliyoitaja. ((Ni kuwa watu wawili walimwomba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) Zakaah, naye akawapindulia macho yake kuwakagua, akawaona mashupavu. Akasema: Mkitaka nitawapeni, na hakuna fungu ndani yake kwa tajiri wala kwa mwenye nguvu mwenye kipato)). [Imekharijiwa nyuma kidogo]
Wamesema: Hapa amejuzisha kuwapa. Na neno lake (..hakuna fungu..) maana yake ni: “Hakuna haki wala fungu kwenu katika kuomba”. [Fat-hul Qadiyr (2/28), Al-Mughniy (6/423), Al-Majmuw’u (6/190) na Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/316)]
Ninasema: “Hayafichikani yaliyomo ndani ya taawiyl hii. Lenye kuonekana bayana ni kuwa neno lake “Mkitaka nitawapeni” halimaanishi kujuzisha kupewa Zakaah, bali ni tahadharisho. Ni kama Kauli Yake Ta’aalaa:
((فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ))
((Basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru)). [Al-Kahf (18:29)]
Kiasi anachopewa fakiri na masikini katika Zakaah
Kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa, fakiri na masikini hupewa Zakaah ya kumtosha au iliyokamili kwake yeye na anaowakimu kwa muda wa mwaka mzima, na haiongezwi zaidi ya hapo.
Wameweka mpaka wa mwaka mmoja kwa kuwa Zakaah hukariri aghlabu kila mwaka, na kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam): ((Alikuwa anahifadhi kwa wakeze chakula cha mwaka mzima)). [Al-Bukhaariy (5357) na Muslim (1757)]
Baadhi yao wamesema: “Kama ni mtu wa kazi za mikono, basi atapewa cha kununulia vifaa vya kazi yake kwa namna ya kuweza kupata faida ya kumtosheleza takriban mahitaji yake”. [Al-Majmuw’u (6/194)]
[3] Wenye kuitumikia Zakaah (Wakusanyaji)
Inajuzu kuwapa Zakaah wenye kuitumikia (wakusanyaji). Mkusanyaji anayepewa Zakaah ni lazima awe na masharti yaliyofafanuliwa nyuma, na mwenye kupewa katika wakusanyaji hao si lazima awe fakiri, kwa kuwa anapewa kutokana na kazi yake, na si kutokana na ufakiri. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((لا تحل الصدقة لغني إلا لخمسة.. قذكر منهم العامل عليها))
((Si halali Zakaah kwa tajiri ila kwa watano…Akataja miongoni mwao mwenye kuitumikia Zakaah)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1635) na Ibn Maajah (184)]
Hanafiy amesema: “Mkusanyaji atalipwa kwa mujibu wa kazi yake. Atapewa cha kumtosheleza yeye na kuwatosheleza wasaidizi wake bila kukadiriwa kwa thamani, wala haongezewi zaidi ya nusu ya alichokusanya hata kama kazi yake ni kubwa zaidi”.
Ash-Shaafi’iy na Hanbali wamesema: “Kiongozi anatakiwa amwajiri mkusanyaji ajira rasmi kwa malipo maalumu, ima kwa muda maalumu au kwa kazi maalum”.
Kisha Ash-Shaafi’iy akasema: “Mkusanyaji hapewi kutoka kwenye (mali jumla ya) Zakaah zaidi ya thumni, na ikiwa malipo yake yatapindukia zaidi ya thumni, basi atakamilishiwa toka Baytul Maal”.
Wengine wamesema atakamilishiwa toka fungu lililobaki. Kadhalika, kiongozi anaweza kumpa malipo yake toka Baytul Maal, na anaweza kumtuma kama kibarua kisha akaja kumlipa malipo sawa na kazi aliyoifanya. Na ikiwa kiongozi atabeba jukumu la kukusanya Zakaah na ugawaji wake, au Mkuu wa Jimbo, au Kadhi au mfano wao ambao wameteuliwa na kiongozi, basi haitojuzu wachukue chochote toka kwenye Zakaah, kwa kuwa wanachukua mishahara yao toka Baytul Maal. Kazi za hawa hazina mpaka maalum.
[4] Wenye kuzoeshwa nyoyo
Wenye kuzoeshwa nyoyo wako aina mbili: Makafiri na Waislamu, na hawa wote ni vigogo waheshimiwa wenye kutiiwa na kusikilizwa na watu wao na koo zao.
Waislamu katika hawa wako aina nne:
1- Waheshimiwa wenye sauti mbele ya watu wao ambao wamesilimu lakini nyoyo zao bado dhaifu. Hawa hupewa ili kuwaweka imara ki-iymaan.
2- Watu watukufu wenye madaraka ambao wamesilimu. Hawa hupewa kwa ajili ya kuwaraghibisha wenzao katika makafiri ili wasilimu.
3- Wanaopewa kwa lengo la kuwazoesha huko kuwe kwa ajili ya kupambana na makafiri walio jirani nao, na kuwahami Waislamu walio karibu nao.
4- Wanaopewa kwa lengo la kuwashajiisha wasiotoa Zakaah wapate kutoa.
Ama makafiri, wao wako aina mbili:
1- Anayetarajiwa kusilimu. Huyu hupewa ili nafsi yake ipondokee kwenye Uislamu.
2- Anayehofiwa shari yake, na kwa kumpa hutarajiwa kuzuia shari yake na kuwazuia wengine pamoja naye. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (2/498)]
Je, fungu la wenye kuzoeshwa nyoyo limekatika baada ya kufariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) au bado lipo?
‘Ulamaa wamekhitalifiana katika suala hili katika kauli mbili: [Sharhu Fat-hil Qadiyr]
Ya kwanza:
Fungu la wenye kuzoeshwa nyoyo bado lipo kama zilivyo aina nyinginezo zilizotajwa katika Kitabu cha Allaah. Haya ni madhehebu ya Ahmad, na ni kauli inayotegemewa kwa Maalik na Ash-Shaafi’iy. Pia ni kauli ya Al-Hasan na Az-Zuhriy.
Ya pili:
Fungu lao limekatika baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Abu Haniyfah. Hoja yao ni kuwa Allaah Ameshautia Uislamu nguvu na uimara na Ameutosheleza na suala la watu kuzoeshewa. Wamelitolea hili dalili kwa kusema kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab hakutoa fungu hili kwa watu waliokuwa wanapewa, na akasema: ((Ni kitu ambacho Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anawapeni ili awazoeshe, na sasa Allaah Ameshautia nguvu Uislamu na Hawahitajieni..)). [Sunan Al-Bayhaqiy (7/20)]
“Kiukweli ni kuwa ‘Umar hakulifuta fungu hili, bali hakuwapa kwa kuwa hawakuwa tena na sifa inayowafanya kuitwa (wazoeshwa nyoyo). Na hii ni kwa upande wa kufanya ijtihaad kwa kuwepo vigezo vya kuitumia matini, na si kwa upande wa kufuta hukmu ya matini, na hili liko wazi. Na kwa msingi huu, ikiwa itatokea haja ya kuwapa wenye maana na sifa ya (wazoeshwa nyoyo), basi hapo mtawala atawapa kutoka fungu hili kwa mujibu wa maslaha ya Waislamu, na hususan nguvu ya Waislamu ikiwa imepinduka na kuwa udhalili, na maadui zao kuwa juu yao.” [Al-Mafswal cha ‘Abdul Kariym Zaydaan (1/433-434) kwa mabadilisho kidogo]
[5] Watumwa
Hawa wako makundi matatu:
La kwanza.
Ni watumwa Waislamu walioandikishiana mkataba na mabwana zao. Hawa inajuzu kuwapa Zakaah kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa kwa ajili ya kuwasaidia wajikomboe. Maalik hakujuzisha hilo, na pia hakujuzisha kutoa chochote katika Zakaah katika kumkomboa mtumwa ambaye ana njia ya kuachiliwa bila kuandikishiana mkataba kama kuwepo mkakati (wa kukomboka), kutwaa (mamlaka) na kuwa sehemu (ya bwana mmiliki).
Na kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa ni kuwa aliyeandikishiana mkataba husaidiwa kama hawezi kulipa sehemu ya malipo ya mkataba wake. Na kama hana kitu kabisa, basi atalipiwa malipo yote anayohitaji kumaliza mkataba.
La pili.
Kumkomboa Muislamu. Maalik na Ahmad katika riwaya yake wamejuzisha kutolewa Zakaah kwa ajili ya hili. Na kwa msingi huu, ikiwa Zakaah iko mkononi mwa mtawala au mkusanyaji Zakaah, basi itajuzu wao kumnunua mtumwa au watumwa na kisha kuwaacha huru, na muamana wao utakuwa kwa Waislamu. Na hivyo hivyo, ikiwa Zakaah iko mkononi mwa mwenye mali na akataka kumwacha huru mtumwa kikamilifu kutokana na Zakaah hiyo, basi hilo litajuzu kutokana na ujumuishi wa Aayah ((وفي الرقاب)) na muamana wake utakuwa kwa Waislamu kwa mujibu wa Maalik.
Hanafiy, Ash-Shaafi’iy na Ahmad katika riwaya nyingine wanasema hakombolewi kutokana na Zakaah, kwa kuwa hilo linakuwa kama kutoa Zakaah kwa mtumwa hohehahe, na mtumwa hapewi Zakaah, na kiuhalisia, bwana wake ndiye atakayeihodhi. Hanafiy anasema kukomboa ni kufuta umiliki, na si kumilikisha, lakini ikiwa Zakaah yake itasaidia kukomboa mtumwa, basi hilo litajuzu kwa mujibu wa Mahanbali wenye kauli hii.
La tatu:
Kumkomboa mateka wa Kiislamu anayeshikiliwa na Mapagani. Mahanbali, Ibn Habiyb na Ibn Al-Hakam wamesema hili linajuzu, kwa kuwa ni kumkomboa mtu matekani, na hili linaingia kwenye ujumuishi wa Aayah, bali ni muhimu zaidi kuliko kumwacha huru mateka tunayemshikilia. Maalik amelikataa hilo.
[6] Wenye madeni
Wadaiwa wenye kustahiki Zakaah ni wa aina tatu:
Aina ya kwanza:
Anayedaiwa deni la kibinafsi. Huyu ‘Ulamaa wote kiujumla wamekubaliana kuwa anastahiki. Masharti ya kumpa Zakaah mdaiwa huyu ni haya yafuatayo:
1- Awe Muislamu.
2- Asiwe wa kutoka Aalil Bayt (ukoo wa Rasuli). Lakini Hanbali anasema inajuzu kumpa Aalil Bayt Zakaah kama anadaiwa.
3- ‘Ulamaa wa Kimaalik wameshurutisha asiwe amekopa ili apewe Zakaah. Ni kama mtu kuwa na cha kumtosha, halafu akatanua matumizi katika fedha za deni ili achukue Zakaah kinyume na fakiri aliyekopa kwa dharura kwa nia ya kuchukua toka kwenye Zakaah.
4- Pia wameshurutisha deni liwe la mdaiwa ambaye mali yake inaweza kushikiliwa. Linaingia hapa deni analomdai mtoto baba yake na deni analodaiwa mtu mwenye hali ngumu. Haliingii hapa deni la kafara na Zakaah.
5- Kwa sharti la Mashaafi’iy, deni liwe la kulipwa wakati uliopo. Wamesema: Ikiwa deni ni la kulipwa mbeleni, basi kuna kauli tatu katika suala hili, ya tatu yake ni kuwa ikiwa muda wa mbeleni wa kulipwa ni mwaka huo huo, basi atapewa, na kama si hivyo hatopewa Zakaah za mwaka huo.
6- Asiweze kulipa kutokana na mali aliyonayo ya Zakaah au isiyo ya Zakaah iliyozidi toshelezo lake. Ikiwa thamani ya nyumba anayoishi ni sawa na mia, naye anadaiwa mia, ilhali nyumba ya hamsini inamtosha, basi hatopewa mpaka iuzwe, na kinachozidi kitalipwa kwenye deni lake kwa mujibu wa kauli ya Maalik. Na kama atapata cha kujazilia sehemu ya deni lake, basi atapewa kilichobakia tu. Na ikiwa ataweza kulipa deni kamili baada ya muda kwa kufanya kazi, basi itajuzu kumpa Zakaah kwa mujibu wa kauli mbili za Ash-Shaafi’iy.
Aina ya pili:
Aliyekopa kwa sababu ya kusuluhisha watu. Asili ya hili ni Hadiyth ya Qubayswah aliyesema: ((Nilikopa fedha nikazitumia kusuluhishia watu, kisha nikamwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kumwomba anisaidie akaniambia: ((Kaa mpaka itujie Zakaah, tuamuru upewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1044), Abu Daawuwd (1624) na An-Nasaaiy (5/96)]
Ash-Shaafi’iy na Maalik wanasema mdaiwa wa aina hii hupewa Zakaah ni sawa akiwa tajiri au fakiri, kwa kuwa lau ingeshurutishwa mtu awe fukara (ndio apewe), basi utashi ungepungua katika kazi hii ya kutukuka na kuthaminiwa. Na picha yake ni kuwepo mzozo kati ya makabila mawili au mitaa miwili na watu wakawa wanauana au kuharibiana mali, hapo akakopa fedha kwa ajili ya kusuluhisha kati yao. Huyu atapewa Zakaah ili alipe deni lake hilo.
Mahanafiy wamesema: “Mwenye deni hilo hapewi Zakaah isipokuwa tu kama hamiliki kiwango cha ziada ya deni lake kama wadaiwa wengineo”.
Maalik katika kumpekua kwetu, hakuzungumza lolote kuhusu hukmu ya kundi hili.
Aina ya tatu:
Anayedaiwa kwa sababu ya deni la kudhamini. Ash-Shaafi’iy kaielezea aina hii. Lenye kuzingatiwa hapa ni kuwepo hali ngumu ya kipesa kwa mdhamini na mdhaminiwa. Ikiwa mmoja wa wawili hao anajiweza kifedha, basi kuna makhitalifiano na uchambuzi kati yao kuhusu kupewa mdhamini Zakaah. [Al-Mawsuw’atu Al-Fiqhiyyah (23/322)].
Maiti Mdaiwa
Akifa mtu anayedaiwa na hakuna cha kulipa deni lake katika alichokiwacha, basi haijuzu kulipa deni lake kwa Zakaah kwa mujibu wa rai ya Jumhuri.
Lakini Maalik amesema deni lake litalipwa kutoka kwenye Zakaah hata kama amekufa. Wengine wamesema: Ana haki zaidi ya kulipiwa kwa vile hakuna kabisa tamaa ya yeye kulilipa, nayo ni moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy.
[7] Fiy Sabiylil Laah
Kundi hili lina aina tatu:
Aina ya kwanza:
Ni wapiganaji katika Njia ya Allaah Ta’aalaa ambao hawana fungu lolote kwenye hazina ya dola, bali wanajitolea tu kushiriki katika Jihaad. Fuqahaa wote kiujumla wamekubaliana kuwa inajuzu kundi hili kupewa Zakaah kiasi cha kuwawezesha kujiandaa kwa vita kwa kupata kipando, silaha, matumizi na yote anayoyahitajia mpiganaji katika kipindi chote cha vita hata kama vita vitachukua muda mrefu. Na si sharti mpiganaji awe masikini, bali inajuzu kumpa tajiri kwa mujibu wa rai ya Jumhuri, kwa kuwa hachukui Zakaah hiyo kujinufaisha nafsi yake, bali ni kwa maslaha ya Waislamu wote.
Hanafiy kasema: Ikiwa mpiganaji ni tajiri, naye ni yule anayemiliki dirhamu 50 au thamani yake kwa dhahabu kama ilivyotangulia katika kundi la mafakiri, basi hapewi Zakaah. Na kama hana, basi atapewa hata kama ana kazi ya kumpatia kipato, kwa kuwa kazi itamzuia asishiriki Jihaad. Na kwa mujibu wa Muhammad, yeye anasema الغازي ni mtu aliyeshindwa kufuatana na Mahujaji (kwenda kuhiji) na si yule aliyeshindwa kuungana na wapiganaji (kwenda Jihaad).
Maalik ameeleza kuwa ni sharti mpiganaji awe mwenye kuwajibikiwa na Jihaad kama kuwa Muislamu, mwanamume, aliyebaleghe, mwenye uwezo na asiwe katika Aalul Bayt.
Ama askari jeshi wenye mishahara toka hazina ya dola, hawa hawapewi Zakaah. Ash-Shaafi’iy anasema katika moja ya kauli zake mbili kuwa ikiwa itashindikana kupatiwa mishahara toka Baytul Maal kutokana na ukata wa fedha, basi itajuzu kuwapa Zakaah.
Aina ya pili:
Ni miundo mbinu ya vita. Wanachuoni wa Kimaalik wameitaja aina hii. Sahihi kwao ni kuwa inajuzu kutumia mali ya Zakaah kwa maslahi mengine ya Jihaad kando na malipo ya wapiganaji kama kujenga ngome za kuhami mji (nchi) usivamiwe na maadui, au kutengenezea vipando vya kivita, au kumlipa jasusi wa kupeleleza habari za adui akiwa Muislamu au kafiri.
Baadhi ya Wanachuoni wa Kishaafi’iy wamejuzisha kununua silaha na zana za vita kwa mali ya Zakaah, na silaha hizo zifanywe waqf ambapo wapiganaji watazitumia kisha watazirejesha. Mahanbali hawakulijuzisha hili, na ndilo lililofanywa na Fuqahaa wengine ambapo wamelihusisha fungu la Fiy Sabiylil Laah kwa wapiganaji tu, au wapiganaji na Mahujaji tu. Fuqahaa hao wamesema kuwa haijuzu kutolewa Zakaah katika aina hii, kwa kuwa hakuna umilikishaji, au upo lakini si kwa wastahiki wa Zakaat. Au kama alivyosema Ahmad kuwa hakuna aliyepewa Zakaat, na Zakaah imeamuriwa itolewe.
Aina ya tatu:
Mahujaji. Jumhuri ya ‘Ulamaa (Hanafiy, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ath-Thawriy, Abu Thawr na Ibn Al-Mundhir, nayo ni riwaya toka kwa Ahmad, na Ibn Qudaamah kasema ni swahiyh) wanaona kuwa haijuzu kutoa Zakaah kwa ajili ya Hijjah, kwa kuwa Sabiylil Laah katika Aayah ni mutwlaq, na itwlaaq imelenga kwenye “Jihaad tu” Fiy Sabiylil Laah Ta’aalaa (na si vinginevyo). Kwa kuwa mengi yaliyotajwa katika Kitabu cha Allaah Ta’aalaa yamekusudiwa Jihaad.
Ahmad anaona Hajji ni katika Njia ya Allaah (Sabiylil Laah), hivyo hutolewa Zakaah, na hii ni kutokana na simulizi isemayo: “Mtu mmoja alimtoa ngamia wake katika Njia ya Allaah, na mkewe akataka kuhiji. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ama hakika wewe, lau utamhijisha kwa kumpandisha ngamia huyu, itakuwa ni katika Njia ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1974), Al-Haakim (1838) na Al-Bayhaqiy (6/164)]
Kwa msingi wa kauli hii, hapewi Zakaah mwenye mali ya kumtosha kuhijia, na asiye na mali ya kumtosha hupewa kwa Hajji ya faradhi tu. Mahanbali wanasema: Inajuzu hata kwa Hajji ya Sunnah.
Imenukuliwa toka kwa baadhi ya Fuqahaa wa Kihanafiy kuwa mstahiki wa kupewa katika (Fiy Sabiyli Laah) ni yule aliyeshindwa kwenda na Mahujaji (kwa kuwa hana kitu). Isipokuwa anayetaka kuhiji kwa mujibu wa Fuqahaa wa Kishaafi’iy hupewa Zakaah kwa mazingatio kuwa ni msafiri kama itakayobainishwa mbeleni.
[8] Ibnus Sabiyl (Msafiri)
Ameitwa “Ibnus Sabiyl” kwa kutoachana kwake na njia, na kutokuwepo nchini kwake kupata hifadhi ya makazi.
Ibn As Sabiyl ni wa aina mbili:
Wa kwanza:
Aliyeko ughaibuni mbali na nchi yake na hana nauli ya kumrejesha. Huyu bila makhitalifiano ni katika watu wa kupewa Zakaah, atapewa cha kumfikisha kwao. Kauli dhwa’iyf ya Ash-Shaafi’iy inasema hapewi, kwa kuwa hilo linakuwa katika hukmu ya kuhamisha Zakaah toka nchi yake (ya asili).
Mghaibu huyu hapewi Zakaah isipokuwa kwa masharti yafuatayo:
La kwanza: Awe Muislamu lakini si Aalul Bayt.
La pili: Asiwe na mali wakati huo ya kumwezesha kurudi kwao hata kama ni tajiri nchini kwake. Na kama ana fedha ambazo atazipata baadaye, au zipo kwa mtu ambaye hayupo, au mwenye hali ngumu ya kifedha, au mwenye kukanusha deni, basi hayo hayazuii kupewa Zakaah kwa kauli ya Hanafiy.
La tatu: Safari yake isiwe ya maasia. Sharti hili limetolewa na Maalik, Ash-Shaafi’iy na Hanbali. Inajuzu kumpa ikiwa safari yake ni kwa ajili ya twa’a ya waajib kama Hajji ya faradhi, kuwatendea wema wazazi, au ya twa’a ya sunnah kama kuwazuru ‘Ulamaa na watu wema, au ya mubaaha kama kutafuta maisha na kufanya biashara. Na kama safari yake ni ya maasi’a, basi haijuzu kumpa Zakaah kwa kuwa itakuwa ni kumsaidia maasi’a yake ila tu kama atatubu. Ama ikiwa safari ni ya matembezi tu, hapa Hanbali ana miono miwili: na wenye nguvu zaidi ni kuwa haijuzu kupewa kwa kuwa safari hii hakuwa na ulazima nayo.
La nne: Asipate wa kumkopesha (ughaibuni) kama ni tajiri kwao. Sharti hili limetolewa na Maalik peke yake.
Watu wa fungu hili hawapewi Zakaah zaidi ya kinachowatosha kurejea makwao. Hanbali amesema: Kama ana nia ya kwenda nchi nyingine, basi atapewa cha kumfikisha huko, kisha na cha kumrejesha nchini kwake.
Maalik amesema: Kama atakaa nchi ya ughaibuni baada ya kupewa Zakaah, basi atapokonywa kama si fakiri nchini kwake. Na ikiwa kitabaki cha kubaki baada ya kurejea nchini kwake, basi kitachukuliwa kwa mujibu wa kauli ya Hanbali. Kisha Hanbali amesema: (Msafiri) mwenye uwezo wa kulipa deni, basi ni bora akope badala ya kuchukua Zakaah.
Wa pili:
Aliyeko nchini kwake na anataka kufanya safari. Jumhuri ya ‘Ulamaa wamekataza kupewa Zakaah watu wa aina hii, lakini Ash-Shaafi’iy amejuzisha kupewa kundi hili kwa sharti msafiri huyo asiwe na masurufu ya safari, na safari isiwe ya ma’asia.
Kwa msingi huu, inajuzu kumpa Zakaah anayetaka kuhiji kama hana fedha za kuhijia katika mji wake anakoanzia safari ya Hajji.
Mahanafiy hawaoni kuwa inajuzu kupewa Zakaah aina hii, lakini wanaona kuwa mtu aliyeko mjini kwake na hana fedha zozote za matumizi lakini anazo fedha mji mwingine ambao hawezi kwenda, basi atazingatiwa ni Ibn As Sabiyl. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/324)]
Je, inajuzu mtoto au baba kupewa Zakaah?
Inajuzu mtu kuwapa Zakaah wazazi wake, au wanawe -ambao hawamtegemei kwa matumizi ya maisha– kama wana madeni, au wameandikishiana mkataba wa kujikomboa, au wapiganaji. [Majmu’u Al-Fataawaa cha Ibn Taymiyyah (25/90-92) na Al-Muhallaa (6/151-152)]
Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (6/229]
Lakini kama ni mafukara na yeye hana uwezo wa kuwakimu kimaisha, Jumhuri wanasema ni marufuku kuwapa Zakaah. Sheikh wa Uislamu –Allaah Amrehemu- amekhitari kujuzu kuwapa Zakaah akishindwa mtu kuwakimu. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/90-92)].
Hili ndilo lenye nguvu zaidi, kwa kuwa Jumhuri kuzuia mtu kuwapa Zakaah anaowakimu kimaisha kumetokana na sababu mbili. Ya kwanza, kwa kuwakimu, yeye anakuwa ni mwenye kujitosheleza. Ya pili, kwa kumpa Zakaah, yeye mwenyewe anajinufaisha, na manufaa hayo ni kuzuia uwajibu wa kuwakimu.
Na ikiwa mtu hawezi toka mwanzoni kuwakimu, au hakuwa akilazimika kuwakimu, basi sababu mbili zitakuwa hazipo tena pamoja na uwepo wa muktadha. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
[Ninasema: “Huenda kujuzu kunatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mu’an bin Yaziyd aliyesema: ((…na baba yangu –Yaziyd- alikuwa ametoa dinari kadhaa za swadaqah (Zakaah). Akaziweka kwa mtu msikitini, nami nikaenda, nikazichukua, halafu nikaenda nazo kwake. Akasema: Wallaah, si wewe niliyekusudia kumpa, nikaenda kumshtakia kwa Rasuli. Rasuli akasema: Umepata uliyoyakusudia ee Yaziyd, na ni haki yako uliyochukua ee Mu’an)). [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy (1422)]
Na hapa iko ihtimali kuwa Mu’an baba yake Yaziyd alikuwa akimkimu kimaisha. Hivyo inakuwa ni hoja ya kujuzu kuwapa watoto Zakaah bila pingamizi, au anaweza kuwa anajitegemea mwenyewe na hahitaji matumizi toka kwa baba yake, na hii inakuwa hoja ya kujuzu kuwapa Zakaah watoto ambao baba hawakimu kimaisha. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Je, inajuzu mke kumpa Zakaah yake mumewe kama ni mstahiki wa Zakaah?
‘Ulamaa wamekhitalifiana katika suala hili katika kauli mbili:
Ya kwanza: Haijuzu kumpa. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Mudawwanah (1/298), Sharhu Fat-hil Qadiyr (2/209) na Al-Mughniy (2/484)]
Hoja yao katika hili ni:
- Mume ni jozi ya wanandoa wawili. Haifai mmoja wao kumpa mwenzake Zakaah yake kama mtu wa kando.
- Mke atanufaika na Zakaah hiyo hiyo kwa kumpa mumewe.
Ya pili: Inajuzu kumpa. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na riwaya nyingine toka kwa Ahmad. [Al-Majmuw’u (6/138) na Al-Mughniy (2/484)]
Ni kauli yenye nguvu zaidi kwa kuwa inawafikiana na dalili.
Ni kwa Hadiyth ya Abu Sa’iyd isemayo kuwa Zaynab mke wa Ibn Mas-‘uwd alisema: ((Ee Nabiy wa Allaah! Hakika wewe umeamuru leo swadaqah (Zakaah). Na mimi nilikuwa na mapambo yangu nikataka kuyatoa Zakaah. Ibn Mas-‘uwd akadai kuwa yeye na mwanaye wana haki zaidi ya kupewa Zakaah hiyo nami. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:
((صدق ابن مسعود، زوجك وولدك أحق من تصدقت به عليهم))
((Amesema kweli Ibn Mas-‘uwd. Mumeo na mwanao wana haki zaidi wewe kuwapa Zakaah kuliko wengine)). [Al-Bukhaariy (1462), Muslim (1000) na Ibn Maajah (1834)]
Na kwa vile mke si waajib wake kutoa matumizi kwa mumewe, basi hazuiliwi kumpa mumewe Zakaah kama mtu wa kando.
Ama mume, yeye Zakaah yake haijuzu kumpa mke wake, kwa kuwa pesa za matumizi ya mke wake yako juu yake. Pesa hizo zitamkidhi na kuzuia asichukue Zakaah. Ibn Al-Mundhir amenukulu Ijma’a juu ya hili. [Al-Mughniy (6/649) na Al-Badaai’u (2/49)]
Je, ndugu akraba wa damu hupewa Zakaah?
Ndugu akraba ikiwa wanastahiki Zakaah inajuzu kuwapa. Wao ni bora zaidi kupewa kuliko wengineo. Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
(( صدقتك على ذي الرحم صدقة وصلة))
((Swadaqah [Zakaah] yako kwa ndugu wa damu, ni swadaqah na ni kuunga [udugu])). [Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (658), An-Nasaaiy (2582) na Ibn Maajah (1844). Kuna udhwa’iyf ndani yake]
Linalototewa ushuhuda ni yaliyomo kwenye Hadiyth ya Zaynab: “Je, Zakaat inawatosheleza wao wawili kwa waume zao na kwa mayatima walio chini ya ulezi wao?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((نعم، ولها أجران: أجر القرابة، وأجر الصدقة))
((Na’am, na yeye ana ajri mbili: ajri ya ukaraba, na ajri ya Zakaat)). [Al-Bukhaariy (1466) na Muslim (998)]
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia Abu Twalha alipomjia na swadaqah yake:
((وإني أرى أن تجعلها في الأقربين...))
((..na hakika mimi naona uitoe kwa akraba zako…..)). [Al-Bukhaariy (1461) na Muslim (998)]
Je, inajuzu kupewa Zakaah mtu faasiq, mtu wa bid-’a, au mtu atakayeitumia kufanyia maasia?
Picha ya wenye kunasibishwa na Uislamu –na ambao wanaweza kuwa ni wenye kustahiki Zakaah -haikosi hali tatu:
1- Waislamu watiifu wenye kusimamisha shariy’ah. Hawa hupewa Zakaah -ikiwa wanastahiki- bila makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa.
2- Waislamu wa bid’a za kuwakufurisha. Hawa watazuiliwa Zakaah bila makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa. Kwa kuwa kwa bid’a zao hizi, wanakuwa wametoka nje ya Diyn, na makafiri hawapewi Zakaah kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa.
3- Waislamu wa bid’a na maasia. Hawa, ikiwa dhana ya mtoaji itatopea kuwa wataitumia katika maasia, basi haijuzu kuwapa Zakaah. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na Hanbal.
Hili kaligusia Sheikh wa Uislamu katika Kitabu cha Al-Fataawaa (25/87) akisema:
“Inatakikana mtu awahakiki wastahiki wa Zakaah yake miongoni mwa mafakiri, masikini, wenye madeni na wengineo kati ya Waislamu wenye kufuata shariy’ah. Na mwenye kudhihirisha bid-’a au fujuwr (ufasiki wa kupinga haki), basi huyo anastahiki adhabu ya kutengwa na jamii au nyingineyo na kutubishwa. Basi vipi asaidiwe kwa hilo? Aidha, haijuzu kupewa Zakaah mtu ambaye haimsaidii katika kumtii Allaah, kwani Allaah Ameifaradhisha ili iwe msaada wa kumtii Yeye. Asiyeswali hapewi mpaka atubie na awajibike kutekeleza Swalaah. Na atakayekuwa katika hawa ni mnafiki, au anadhihirisha bid-’a inayokhalifiana na Qur-aan na Sunnah katika bid-’a za masuala ya kiitikadi na ki’ibaadah, basi huyo anastahiki adhabu. Na kati ya adhabu hizo ni kunyimwa Zakaah mpaka atubie”.
Ama ikiwa hawaitumii mali ya Zakaah katika kumwasi Allaah, Sheikh wa Uislamu anaona pia kuwa wasipewe. Lakini wengine wanaona kuwa watapewa kwa kuwa wanaingia kwenye ujumuishi wa Aayah ya kundi la wanaopewa Zakaah ambayo haikubagua kati ya mtendaji maasia au mtiifu wa maamrisho.
Alaa kulli haal, lililo bora ni kutangulizwa watu walioshika Diyn na waliolingamana sawa katika itikadi na utendaji kabla ya wengine wakati wa kugawa Zakaah. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Ninasema: Kati ya yaliyosimuliwa katika mlango huu:
1- Toka kwa Qaz’ah amesema: ((Nilimwambia Ibn ‘Umar: Mimi nina mali, nani nimpe Zakaah yake? Akasema: Itoe kwa watu hawa –yaani Maamiyr- Nikasema: Basi watanunulia kwayo nguo na manukato. Akasema: Hata wakinunulia kwayo nguo na manukato, lakini katika mali yako kuna haki (nyingine) zaidi ya Zakaah)). [Al-Amwaal cha Abu ‘Ubayd (1798) kwa Sanad Swahiyh na mfanowe Ibn Abiy Shaybah (4/28)]
2- Toka kwa Suhayl bin Abiy Swaaleh toka kwa baba yake amesema: ((Nilimwendea Sa’ad bin Abiy Waqqaasw nikamwambia: Nina mali nataka kuitolea Zakaah yake, na watu hawa hali yao kama unavyoiona. Akasema: Wape hiyo Zakaah. Nikawaendea Ibn ‘Umar, Abu Hurayrah na Abu Sa’iyd, nao wakasema hivyo hivyo)). [Al-Amwaal (1789) na Al-Bayhaqiy (4/115) kwa Sanad Swahiyh.
Linaloonekana kutokana na konteksi ya athar hizi ni kuwa muradi wa watu –ambao hupewa Zakaah pamoja na maasia yao- ni Maamiri na viongozi ambao ni lazima kuwatii. Hivyo hakuna ukinzani katika yale tuliyoyatilia nguvu katika madhehebu ya Sheikh wa Uislamu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Je, Baniy Haashim wanapewa Zakaah?
Baniy Haashim kwa kauli yenye nguvu, ni ukoo wa ‘Aliyy, ukoo wa ‘Aqiyl, ukoo wa Ja-’afar, ukoo wa ‘Abbaas, ukoo wa Al-Haarith na pia ukoo wa Al-Muttwalib. [Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) -kama ilivyo kwa Al-Bukhaariy (3/40) na wengineo-:
((إنا وبني المطلب لا نفنرق في جاهلية ولا إسلام، وإنما نحن وهم شيء واحد)) وشبك بين أصابعه
((Hakika sisi na Baniy Al-Muttwalib, hatutengani katika ujahilia wala katika Uislamu, bali hakika sisi na wao ni kitu kimoja)). Akapachanisha kati ya vidole vyake]
Hawa, si halali kwao kuchukua Zakaah ya faradhi bila makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((إن الصدقة لا تنبغي لآل محمد، وإنما هي أوساخ الناس))
((Hakika Zakaah haifai kwa ukoo wa Muhammad. Hakika si jinginelo, Zakaah ni takataka za watu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1072) na An-Nasaaiy (1609)]
Maana ya (takataka za watu) ni kuwa Zakaah ni utwaharisho wa mali zao na nafsi zao. Zakaah ni mashine ya kusugua na kuondosha uchafu. Na kwa neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((إنا لا تحل لنا الصدقة))
((Hakika sisi si halali kwetu swadaqah [Zakaah])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1069) na Abu Daawuwd (1650)]
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia Al-Hasan bin ‘Aliyy alipochukua tende moja kati ya tende za swadaqah:
((كخ كخ (ليطرحها) أما شعرت أنا لا نأكل الصدقة))
((Wacha hii, wacha hii! (tema): Je hujui kuwa sisi hatuli swadaqah [Zakaah])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1491) na Muslim (1069)]
Sheikh wa Uislamu amekhitari kuwa inajuzu kwa Baniy Haashim kuchukua Zakaah ya Mahaashim na si Zakaah ya watu wengineo. Haya yamesimuliwa toka kwa Abu Haniyfah na Abu Yuwsuf. [Fat-hul Qadiyr cha Ibn Al-Hamaam (2/272). Angalia Al-Jaami’u Lil-Ikhtibaaraat Al-Fiqhiyyah cha Ibn Taymiyyah. Dk. Ahmad Muwaafiy (1/400)]
Kupelekwa Zakaah Mji Mwingine
Asli ya mambo ni kuwa, Zakaah huchukuliwa toka kwa matajiri wa mji na kurejeshwa kwa mafakiri wao, haihamishwi ikapelekwa mji mwingine. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hadiyth ya Mu’aadh:
((أخبرهم أن الله قد فرض عليهم صدقة تؤخذ من أغنيائهم وترد إلى فقرائهم))
((Waeleze kuwa Allaah Amewafaradhia Zakaah, huchukuliwa toka kwa matajiri wao na kurejeshwa kwa mafukara wao)). [Imeripotiwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Lakini kama wakazi wa mji wa mtoaji Zakaah si wahitaji wa Zakaah, au watu wa eneo jingine wakawa wanaihitajia zaidi, au wakawa ni akraba wa mtoaji Zakaah wenye kustahiki Zakaah, au mengineyo kati ya manufaiko yenye uzito, basi hakuna ubaya kuihamisha Zakaah na kuipeleka mji mwingine. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.