06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Ni Vipi Vigezo Vya Uwezo Wa Kuhiji?

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

06-Ni Vipi Vigezo Vya Uwezo Wa Kuhiji?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Uwezo wa kuwajibisha Hajj ni lazima uwe na vigezo vifuatavyo:

 

1- Afya ya mwili na kusalimika na magonjwa yanayoweza kumzuia asiweze kutekeleza ‘amali za Hajj.

 

Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: ((Kwamba mwanamke mmoja toka Khath-’am alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika baba yangu imemkuta Faradhi ya Allaah katika Hajj akiwa mzee kikongwe, hawezi kukaa sawa juu ya mnyama, basi je naweza kumhijia? Akamwambia:

((حجي عنه))

((Mhijie)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1855) na Muslim (1334)]

 

Basi yeyote atakayetimiza shuruti nyinginezo lakini akawa mgonjwa wa maradhi sugu, au mgonjwa hawezi kusimama, basi si wajibu kutekeleza faradhi ya Hajj yeye mwenyewe binafsi kwa itifaki ya ‘Ulamaa wote. Lakini wamekhitalifiana kama ni lazima atafute mtu wa kumhijia au la. Fuqahaa wa Kishaafi’iy, Kihanbali na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah wamesema ni lazima atafute, kwa hoja kwamba afya ya mwili ni sharti ya mtu kujifanyia mwenyewe na si sharti ya wajibu. Ama Abu Haniyfah na Maalik, wao wanasema haimlazimu. [Nihaayatul Muhtaaj (2/385), Al-Kaafiy (1/214) na Fat-hul Qadiyr (2/125)]

 

Ninasema: “Lililo bayana zaidi ni kuwa inamlazimu atafute mtu kutokana na udulisho wa Hadiyth iliyotangulia ya Ibn ‘Abbaas. Katika baadhi ya riwaya zake, Hadiyth inasema:

 

((أرأيت إن كان على أبيك دين، أكنت قاضيته؟)) قالت: نعم، قال: ((فدين الله أحق أن يقضى))

((Nieleze, kama baba yako alikuwa anadaiwa deni, je ungelilipa)). Akasema: Na’am. Akasema: ((Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5699) na An-Nasaaiy (5/116). Angalia Al-Muhallaa (7/57)]

 

2- Amiliki chenye kumtosha katika safari yake, ukaazi wake, na kurudi kwake ambacho kimezidi mahitaji yake ya kimsingi katika masarifu ya watoto wake na wote ambao ni jukumu lake kuwakimu, na asiwe na deni. Hii ni kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa kinyume na walivyosema Fuqahaa wa Kimaalik. [Al-Majmuw’u (7/56) na Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (17/31)]

 

Kwa kuwa masarifu ni haki ya wanadamu, na haki hii inawekwa mbele, na kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((كفى بالمرء إثما أن يضيّع من يقوت))

((Inamtosha mtu kuwa anapata madhambi kwa kutowajali anaowalisha)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1676). Angalia Al-Irwaa (989)]

 

Inaingia katika hili kumiliki fedha za matumizi na kipando (usafiri). Neno السبيل katika Kauli Yake Ta’aalaa:

((مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا))

Kwa mwenye uwezo kuiendea

 

.. ni kwa maana ya masurufu (fedha za matumizi) na kipando. Tafsiyr hii imesimuliwa kwa njia Marfuw’u, na si swahiyh. [Tafsiyr At-Twabariy (4/15)]

 

3- Usalama wa njia ya usafiri

 

Unajumuisha usalama wa roho na mali wakati watu wanaposafiri kwenda (Makkah) kuhiji, kwa kuwa uwezo haupo bila usalama.

 

Mahram ni sharti kwa mwanamke ili awajibikiwe na Hajj

 

Ili Hajj iwe waajib kwa mwanamke, ni lazima awe na masharti matano yaliyotangulia. Masharti haya huongezewa jingine juu yake, nalo ni kuandamana na mume wake au mahram yake. Na kama hakumpata, basi Hajj si waajib juu kwake. [Taarifu ya mahram itakuja katika mlango wa ndoa kwenye kitabu hiki In Shaa Allaah]

 

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema:

 

((لا يخلون رجل بامرأة إلا ومعها ذو محرم، ولا تسافر المرأة إلا مع ذي محرم))، فقام رجل فقال: يا رسول الله، إن امرأتي خرجت حاجة، وإني اكتتبت في غزوة كذا وكذا، فقال: ((انطلق فحج مع امرأتك))

((Asikae kabisa mwanamume faragha na mwanamke isipokuwa awe pamoja naye mahram wake, na asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja na mahram wake)). Mtu mmoja akasimama akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mke wangu ametoka kwenda kuhiji, na mimi nimesajiliwa katika Vita kadha wa kadha. Akamwambia: ((Chomoka haraka ukahiji na mkeo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (3006) na Muslim (1341)]

 

Haya ni madhehebu ya Hanafiy na Hanbal. [Al-Badaai’u (3/1089), Al-Mughniy (3/230), Bidaayatul Mujtahid (1/348), na Al-Majmuw’u (7/68)]

 

Lakini Maalik na Ash-Shaafi’iy wanasema kuwa mahram si sharti katika Hajj, lakini wameshurutisha usalama wa safari na kuandamana na watu wenye kuaminika. Na hii ni katika Hajj ya faradhi, ama Hajj ya Sunnah, haijuzu kutoka mwanamke ila pamoja na mahram yake kwa itifaki ya ‘Ulamaa wote.

 

Adh-Dhwaahiriyyah wamejuzisha mwanamke asiye na mume wala mahram au baba mkwe wake, ahiji bila mahram. [Al-Muhallaa (7/47)]

 

Wote wametoa dalili kwa yaliyosimuliwa kuhusiana na tafsiyr ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa uwezo ni masurufu na kipando, na tafsiyr hii ni dhwa’iyf kama ilivyotangulia. Na pia kwa neno lake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)

 

((يوشك أن تخرج الظعينة من الحيرة تؤم البيت لا جوار معها، لا تخاف إلا الله))

((Imekurubia mwanamke kusafiri peke yake ndani ya hawdaj toka Hiyrah akiikusudia Nyumba, haogopi chochote isipokuwa Allaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (3595) na wengineo]

 

 “Hawdaj” ni kibanda kidogo kinachopachikwa juu ya mgongo wa ngamia ambapo msafiri hukaa ndani yake.

 

Hili linajibiwa kwa kusema hii ni habari kuhusiana na yatakayotokea kwa upande wa amani na usalama, na halina uhusiano na hukmu ya kusafiri mwanamke bila mahram.

 

Na ikiwa mwanamke atahiji bila mahram, basi Hajj yake ni sahihi lakini atapata madhambi kwa kutoka peke yake.

 

Mke atamtaka idhini mumewe kwenda Hajj, na mume hana haki ya kumzuia

[Al-Mughniy (3/240), Al-Ummu (2/117), Fat-hul Qadiyr (2/130) na Al-Muhallaa (7/52)]

 

1- Zikipatikana shuruti zilizotangulia za uwajibu wa Hajj kwa mwanamke –katika Hajj ya faradhi- basi inastahabiwa kwake amwombe ruksa mumewe. Akimruhusu vyema, na kama hakumruhusu basi atatoka bila ruksa, kwa sababu, kwa mujibu wa rai ya Jumhuri ya ‘Ulamaa, mume hana haki ya kumzuia mke kwenda kufanya Hajj ya faradhi, kwa kuwa haki ya mume haitangulizwi juu ya Fardhi ‘Ayn kama kufunga Ramadhwaan na mfano wake.

 

2- Ikiwa Hajj yake ni Hajj ya nadhiri, na nadhiri aliiweka kwa idhini ya mumewe, au aliiweka kabla ya kuoana kisha akamweleza naye akaikubali, basi mume hana haki ya kumzuia. Ama kama ataiweka kinyume na utashi wa mumewe, basi mume ana haki ya kumzuia. ‘Ulamaa wengine wamesema hana haki ya kumzuia vile vile, kwa kuwa ni waajib kama ilivyo Hajj ya faradhi.

 

3- Ikiwa Hajj yake ni ya Sunnah, au ya kumhijia mtu, hapo kwa mujibu wa Ijma’a, ni lazima aombe ruksa, na inajuzu mume kumzuia.

 

Je, mwanamke mwenye eda anaweza kwenda kuhiji?

 

Mwanamke mwenye eda ya talaka au ya kufiwa na mume ya muda wa kuweza kwenda Hijjah, si waajib kuhiji kwa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa, kwa kuwa Allaah Amewakataza wanawake wenye eda kutokana na Neno Lake:

((لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ))

((Msiwatowe katika nyumba zao, na wala wao wasitoke)). [At-Twalaaq (65:1)]

 

..na kwa vile pia Hajj inaweza kutekelezwa wakati mwingine. Lakini eda ni lazima iwe katika wakati maalum.

 

Fuqahaa wa Kihanbali wametofautisha kati ya kutoka kwake kwenda Hijja katika eda ya kuachwa (kutalikiwa), na eda ya kufiwa na mume wake. Wamezuia asiende kuhiji katika eda ya kufiwa na mumewe, kwa sababu kubaki nyumbani katika eda hii ni waajib, na wamejuzisha katika eda ya talaka ya kutorejelewa tena (talaka tatu), kwa sababu si waajib kubakia nyumbani.

 

Ninasema: “Sioni mantiki yoyote ya utofautishaji huu -kuhusu wajibu wa kubakia nyumbani- kati ya eda ya kufiwa na mume na eda ya kuachwa. Kimsingi, Aayah inahusiana na wanawake waliotalikiwa. Na mwanamke mwenye eda ya kufiwa na mume anafanyiwa qiyaas –kwa moja ya kauli mbili-. Na kauli ya pili inasema kuwa mwenye eda ya kufiwa na mumewe atakalia eda yake popote pale anapotaka. Na hili litakuja kuchambuliwa katika mlango wake. Basi si vyema wakageuza kinyume utofautishaji huu!!” 

 

Share