08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Mawaaqiyt (Nyakati Na Mahala Pa Kuhirimia)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

08-Mawaaqiyt (Nyakati Na Mahala Pa Kuhirimia)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

المواقيت  ni wingi (plural) wa ميقات , nayo ni ya wakati na ya mahala.

 

 

(a) Mawaaqiyt Za Nyakati

 

Nazo ni nyakati ambazo haijuzu ‘amali yoyote ya Hajj isipokuwa ndani yake. Allaah Ta’aalaa Amezitaja nyakati hizi katika Kauli Yake:

 

((الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ ۚ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ))

((Hajj ni miezi maalumu. Na atakayekusudia kuhiji (akahirimia), basi asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala mabishano katika Hajj)). [Al-Baqarah (2:197)]

 

Aayah hii inatuhabarisha kuwa Hajj ina nyakati maalum zilizotajwa, hivyo haijuzu kuihirimia isipokuwa katika miezi ya Hajj. Allaah Ta’aalaa Amesema:

((وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ))

((Na yeyote atakayevuka Mipaka ya Allaah, basi kwa yakini amedhulumu nafsi yake)). [At-Twalaaq (62:1)]

 

Ikiwa mtu atahirimia Hajj kabla ya miezi yake, basi haitoswihi. Haya ni madhehebu ya Swahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum). [Al-Muhallaa (7/65-66) na Al-Majmuw’u (7/128) na kurasa zinazofuatia].

 

Imepokewa pia toka kwa Ash-Sha-‘abiyy na ‘Atwaa ya kuwa inaswihi kuhirimia.

 

Al-Awzaa’iy na Ash-Shaafi’iy wamesema: Inakuwa ni ‘Umrah na hapana budi.

 

Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad wamesema kuwa hilo ni makruhu, na Hajj itamlazimu kama amehirimia kabla ya miezi ya Hajj.

 

Lililo sahihi ni kuwa Hajj yake haiswihi kutokana na Aayah ilivyoeleza. Ama kusema kuwa itakuwa ni ‘Umrah, hapa ni lazima tuhoji. Vipi tubatilishe ‘amali yake ambayo ameingia kwa kuwa tu amekhalifu la sawa? Kisha vipi tumlazimishe kwa kitendo hicho ‘Umrah ambayo hakuitaka asilani, wala hakuikusudia wala hajainuwia? Bali:

 

((إنما الاعمال بالنيات وإنما لكل امرئ ما نوى))

((Hakika si jinginelo, ‘amali ni kwa mujibu wa niya, na hakika kila mtu ni kwa lile alilolinuwia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy, Muslim (1907) na wengineo]

 

Huyu ni kama mtu aliyehirimia Swalaah kabla ya wakati wake, Swalaah hii ni batili, na mwenye kunuwia kufunga kabla ya wakati wake, basi Swawm yake ni batili.

 

 

Miezi ya Hajj

 

Ni Shawwaal (Mfungo Mosi), Dhul-Qa-‘adah (Mfungo Pili) na siku tisa za Dhul-Hijjah (Mfungo Tatu) kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote. Kisha kumetokea mvutano kati yao kuhusu Yawm An-Nahr (Siku ya kuchinja) na baki ya siku za Dhul-Hijjah, na zikawa kauli zao kuhusu miezi ya Hajj ni tatu:

 

1-  Ni Shawwaal, Dhul-Qa-‘adah na siku tisa za Dhul-Hijjah.

 

Ni madhehebu ya Mahanafiy na Mahanbali, na ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Ibn Mas-‘uwd, Ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar, Ibn Az-Zubayr na kundi la Masalaf. [Sharhu Fat-hil Qadiyr (2/220) na Al-Mughniy (3/275)]

 

2- Ni Shawwaal, Dhul-Qa-‘adah na siku tisa za Dhul-Hijjah lakini Yawm An-Nahr (tarehe 10) haiingii katika miezi hii ya Hajj.

Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy. [Al-Majmuw-‘u 7/135) na Nihaayatul Muhtaaj (3/256)]

Hoja yao ni Kauli Yake Ta’aalaa:

((فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجّ))

((Na atakayekusudia kuhiji (akahirimia) katika miezi hiyo)). [Al-Baqarah (2:197)

 

Hivyo, haiwezekani kuihirimia Hajj baada ya usiku wa An-Nahr.

 

3- Ni Shawwaal, Dhul-Qa-‘adah na Dhul-Hijjah yote.

 

Ni madhehebu ya Maalik na Ibn Hazm. Ni kauli iliyosimuliwa pia toka kwa ‘Umar na mwanawe pamoja na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhum). [Bidaayatul Mujtahid (1/351), Al-Kaafiy Fiy Madh-habi Ahlil Madiynah (1/357) na Al-Muhallaa (7/69)]

 

 

Hoja yao wanasema uchache wa wingi (plural) ni tatu, na kwamba Kutupia Mawe (Jamaraat) -nayo ni katika ‘amali za Hajj-, hufanywa tarehe kumi na tatu, na Twawaaf Al-Ifaadhwah –nayo ni nguzo ya Hajj- hufanywa katika Dhul Hijjah yote bila makhitalifiano yoyote.

 

Ninasema: “Yenye nguvu zaidi ni kauli ya tatu. Hivyo miezi ya Hajj inakuwa ni Shawwaal, Dhul-Qa-‘adah na Dhul-Hijjah yote. Na hii ni kwa maana kwamba ni lazima kisifanyike chochote katika ‘amali za Hajj kabla au baada ya miezi hii, na hailazimu kuwa Hajj inajuzu katika siku zote katika masiku ya miezi hii, bali ni lazima kuchunga hili lifuatalo:

 

Kwamba aliyepitwa na kisimamo cha ‘Arafah katika sehemu ya Usiku wa An-Nahr, basi kaikosa Hajj. Na hili ndilo ambalo Ash-Shaafi’iy ameling’amua alipoitoa Siku ya An-Nahr (Tarehe kumi ya Dhul-Hijjah) nje ya miezi ya Hajj. Naye anajibiwa akiambiwa kuwa Allaah Ta’aalaa Ameiita Siku ya An-Nahr “Yawmu Al-Hajj Al-Akbar” (Siku ya Hajj Kuu) katika Kauli Yake:

((وَأَذَانٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ))

((Na ni tangazo kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake kwa watu siku ya Hajj Kuu)). [At-Tawbah (9:3)]

 

(b) Mawaaqiyt Za Mwahala

 

Nazo ni sehemu ambazo zimeainishwa na kuwekewa mpaka na Shariy’ah ili ahirimie kutoka hapo mwenye kunuwia Hajj au ‘Umrah, na haijuzu kwake kuvuka au kutoka nje ya mipaka bila ya kuhirimia. Mahala hapa panamhusu kila anayepita hapo akikusudia Hajj au ‘Umrah sawasawa akiwa ni mkazi wa maeneo hayo au si mkazi. Maeneo hayo ni:

 

1- Dhul-Hulayfah: Ni kwa watu wa Madiynah. Kwa sasa panajulikana kama Aabaar ‘Aliy.

 

2- Al-Juhfah: Ni kwa watu wa Sham, Misri na Morocco. Ni karibu na Raabigh [mkoa magharibi mwa Saudia] ambao kwa sasa umefanywa kuwa Miyqaat.

 

3- Qarnul Manaazil: Ni kwa watu wa Najd. Kwa sasa inajulikana kama Waad As-Sayl.

 

4- Yalamlam: Ni kwa watu wa Yemen.

Maeneo haya manne yamekubaliwa na ‘Ulamaa wote kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) aliyesema:

 

((وقَّتَ رسولُ اللهِ صلَّى الله عليه وسَلَّم لأهلِ المدينةِ ذا الحُلَيفة، ولأهل الشَّامِ الجُحْفةَ، ولأهل نَجْدٍ قَرْنَ المنازِلِ، ولأهْلِ اليَمَنِ يَلَمْلَمَ، قال: فهُنَّ لهُنَّ، ولِمَن أتى عليهِنَّ مِن غيرِ أهْلِهِنَّ، لِمَن كان يريد الحَجَّ والعُمْرَةَ، فمن كان دونَهنَّ فمُهَلُّه من أهْلِه، وكذاك أهْلُ مكَّةَ يُهِلُّونَ منها))

((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwawekea watu wa Madiynah Dhul Hulayfah kuwa Miyqaat yao , Al-Juhfah kwa watu wa Sham, Qarn Al-Manaazil kwa watu Najd, na Yalamlam kwa watu wa Yemen akasema: Basi [Miyqaat] hizo ni zao na kwa atakayepita humo katika wasio wakazi ambaye amekusudia Hajj au ‘Umrah. Na atakayekuwa nje ya Miyqaat hizo, basi atahirimia mjini kwake alipo, na pia watu wa Makkah watahirimia kutoka ndani ya Makkah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1526) na Muslim (1181)]

 

5- Dhaatu ‘Irqi. Ni kwa watu wa Irak na Al-Mashriq. Mahala hapa pako karibu na Al-‘Uqayq. Pamekhitalifiwa kuhusiana na aliyepafanya kuwa Miyqaat. Kuna wanaosema ni ‘Umar kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Ilipokombolewa miji hii miwili (Yaani Basrah na Kuwfah) walimwendea ‘Umar wakamwambia: Ee Amiyrul Muuminiyn! Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amewawekea watu wa Najd Qarn [Al-Manaazil] kuwa Miyqaat yao, nayo iko mbali na njia yetu, na sisi tukitaka kwenda Qarn tunapata uzito. Akasema: Basi angalieni iliyo mfano wake katika njia yenu, akawahadidia Dhaatu ‘Irqi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1531) na Al-Bayhaqiy (5/27)]

 

Wengine wanasema, bali aliyeweka mpaka ni Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa Hadiyth ya Jaabir:

((مهلّ أهل المدينة ذي الحليفة، والطريق الآخر الجحفة، ومهلّ العراق من ذات عرق، ومهلّ أهل نجد من قرن، ومهلّ أهل اليمن يلملم))

((Mahala pa kuhirimia watu wa Madiynah ni Dhul-Hulayfah, na njia nyingine Al-Juhfah. Mahala pa kuhirimia watu wa Irak ni Dhaatu ‘Irqi. Mahala pa kuhirimia watu wa Najd ni  Qarn. Mahala pa kuhirimia watu wa Yemen ni Yalamlam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuuwd (1183). Za kutilia nguvu umarfuw’u wake ziko kwenye Al-Irwaa (998)].

 

Hadiyth hii ina mvutano kuhusu umarfu’u wake. Lakini kuwa kwake Marfuw’u kunatiliwa nguvu na Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) isemayo: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) aliwahadidia Miyqaat watu wa Iraki Dhaatu ‘Irqi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1739), An-Nasaaiy (2/6) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (999)]

 

Hili linaoanishwa kwa kusema kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ndiye aliyeainisha mpaka huo lakini ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) hakulijua hilo, akajitahidi na akaisadifu Sunnah. Ni mengi sana aliyoyasadifu yakaoana na shariah.

 

Miyqaat ya mkazi wa Makkah ni nyumba za Makkah, na mwenye kuishi kati ya Makkah na kati ya moja ya Miyqaat hizi, basi Miyqaat yake ni nyumbani kwake.

 

Na mtu ambaye njia yake haipiti katika Miyqaat yoyote kati ya hizi, akijua kwamba yuko usambamba na iliyo karibu zaidi naye, basi atahirimia hapo. Na atakayekuwa ndani ya ndege, basi atahirimia atakapokuwa sambamba na Miyqaat akiwa angani, na anakuwa ashajiandaa kabla ya kuhirimia kwa kuvaa nguo za kuhirimia kabla ya kuwa sambamba na Miyqaat. Anapokuwa sambamba nayo, atanuwia Ihraam hapo hapo, si aicheleweshe mpaka atue.

 

 

 

 

Share