17-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Nguzo Ya Pili Ya Hajj: Twawaaf “Kutufu” (Twawaaful Ifaadhwah)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

17-Nguzo Ya Pili Ya Hajj: Twawaaf “Kutufu” (Twawaaful Ifaadhwah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Twawaaf ni nini?

 

Kilugha, Twawaaf ni kukizunguka kitu kwa pembeni. Ama kisharia, ni kuizunguka Nyumba Tukufu [Al-Ka’abah] kwa namna itakavyoelezewa baadaye.

 

Aina za Twawaaf

 

Twawaaf za kisharia katika Hajj ni tatu:

 

1- Twawaaf Al-Quduwm:

 

Inaitwa pia Twawaaf Al-Wuruwd (ya kuja) na Twawaaf At-Tahiyyah (maamkizi), kwa kuwa imewekwa kwa mjaji asiye mkazi wa Makkah ili kuisalimia Nyumba. Imesuniwa kwa mjaji anayetoka nje ya mipaka ya Makkah kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa –kinyume na Fuqahaa wa Kimaalik ambao wamewajibisha

Twawaaf Al-Quduwm na kusema: Mwenye kuiacha ni lazima achinje kwa ajili ya kuisalimia Nyumba Kongwe.

 

Na asili ya hili ni kitendo chake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Katika Hadiyth ya Jaabir: ((Mpaka tulipoifikia Nyumba pamoja naye, aliigusa nguzo kwa mkono [kama anaisalimia], akaenda kasi kidogo mara tatu (mizunguko mitatu ya kwanza) na akatembea kawaida mara nne [mizunguko minne ya mwisho])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1218)]

 

Na toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa): ((Jambo la kwanza aliloanza nalo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wakati alipowasili Makkah ni kutawadha, kisha alitufu…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1615) na Muslim (1245)]

 

‘Ulamaa wa Kimaalik wametolea dalili ulazima wa hilo kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((خذوا عني مناسككم))

((Jifunzeni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj)). [Imekharijiwa na Muslim (1297), An-Nasaaiy (3062) na Abu Daawuwd (1970]

 

Jumhuri wamesema: “Kiashirio kimethibiti kuwa si waajib, kwa kuwa makusudio ni kusalimia. Ni sawa na Swalaah ya Maamkizi ya Msikiti ambayo ni Sunnah”.

 

Kauli hii ni imara zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi wa yote.

 

Faida

 

Aliyekwenda moja kwa moja Minaa au ‘Arafaat akitokea Miyqaat na hakuwahi kuingia Makkah kabla ya hapo, basi si vizuri kwake –wala kwa mwenye kufanya Tamattu’u- kutufu Twawaaf Al-Quduwm baada ya kusimama ‘Arafah, kwa kuwa Twawaaf Al-Quduwm inapotea kwa kusimama ‘Arafah.

 

 

2- Twawaaf Al-Ifaadhwah (Twawaaf Ar-Ruknu)

 

Inaitwa pia Twawaaf ya Ziara. Nayo ni nguzo kati ya nguzo za Hajj kwa makubaliano ya Fuqahaa wote. Na Hujaji hawezi kufanya tahalluli kubwa bila ya kuifanya Twawaaf hii, na hakuna kabisa chochote cha badali yake. Qur-aan, Sunnah na Ijma’a zimethibitisha kuwa ni nguzo ya Hajj. [Al-Mughniy (3/440), Al-Badaai’u (1/128) na At-Tamhiyd (6/133- Fat-hul Maalik]

Allaah Amesema:

((ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ))

((Kisha wamalize ‘ibaadah zao; wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)).  [Al-Hajj (22:29)]

 

‘Ulamaa wameafikiana wote kuwa Aayah hii inahusu Twawaaf Al-Ifaadhwah.

 

Na katika Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) ni kuwa Swafiyyah bint Huyayy (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alihiji pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na akapata hedhi. Rasuli akasema: ((Je, yeye katuzuia?)). Wakasema: Yeye ameshatufu Twawaaf Al-Ifaadhwah”. Akasema: ((Basi kama hivyo, hawezi kutuzuia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1733) na Muslim (1211)]

 

Hivyo, haya yanadulisha kuwa Twawaaf Al-Ifaadhwah ni faradhi ya lazima. Na kama isingekuwa faradhi, basi asingelizuiliwa kusafiri ambaye hakuifanya.

 

 

Wakati wa Twawaaf Al-Ifaadhwah  

 

(a) Wakati wake wa mwanzo:

 

Twawaaf hii haiswihi kabla ya wakati wake ainishwa wa kisharia. Ni wakati mpana unaoanzia tokea jua linapochomoza Siku ya Kuchinja [Yawm An-Nahr tarehe 10]. Hii ni kwa mujibu wa Maalik na Hanafiy.

 

Ama Ash-Shaafi’iy na Hanbal, wao wanasema wakati wake unaanzia baada ya usiku wa manane wa kuamkia Siku ya Kuchinja kwa aliyesimama ‘Arafah kabla yake.

 

(b) Wakati wa mwisho wake:

 

Mahanafi wanasema mwisho wa wakati wake ni Siku ya Mwisho ya Tashriyq. Na Fuqahaa wa Kimaalik wanasema wakati wake ni Mwezi wa Dhul Hijjah, na kama atachelewesha ukapita, basi ni lazima achinje mnyama fidia.

 

Ama Fuqahaa wa Kishaafiíy, Kihanbali na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah, wao wanasema: Asili ni kutoweka wakati maalum wa hilo, na hakuna linalowajibisha kufanyika Twawaaf hii katika Masiku ya Kuchinja, na wala mtu halazimikiwi kutoa fidia kama ataichelewesha baada ya Masiku ya Kuchinja au baada ya Mwezi wa Dhul Hijjah. Na Twawaaf hii haisameheki kwa mtu milele, na hata fidia pia haiwezi kuziba kitu, kwa kuwa ni nguzo, na mtu ataendelea kuzuiwa asijimai mpaka arudi aifanye.

 

 

Ninasema: “Kauli inayosema kuwa haijuzu kuichelewesha Twawaaf hii baada ya Mwezi wa Dhul Hijjah ni elekevu zaidi, kwa kuwa katika Mwezi huu, ndimo ‘amali za Hijjah hufanywa ingawa kiakiba zaidi ni Hujaji asiicheleweshe mpaka baada ya Masiku ya Kuchinja ili atoke ndani ya mvutano. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema katika Kitabu chake cha Mansak: “Ataingia Makkah na atatufu Twawaaf Al-Ifaadhwah –kama ataweza hilo Siku ya Kuchinja (tarehe 10)- na kama hakuweza, basi ataifanya baada ya hapo, lakini inatakikana iwe katika Masiku ya At-Tashriyq, kwa kuwa kuichelewesha baada ya Masiku hayo, kuna mgogoro”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/138). Ibn Hazm (7/172) anasema akiichelewesha baada ya Mwezi wa Dhul Hijjah, basi Hajj yake inabatilika.

 

 

(c) Wakati wake bora zaidi

 

Imesuniwa Twawaafu hii ifanywe Siku ya Kuchinja (Siku ya ‘Iyd) kwa kuwa Rasuli alifanya siku hiyo kwa mujibu wa Hadiyth ndefu ya Jaabir na nyinginezo.

 

Imeshurutishwa katika Twawaaf hii mahsusi itanguliwe na Kisimamo cha ‘Arafah. Kama atatufu kabla ya Kusimama ‘Arafah, basi faradhi hiyo ya Twawaaf haimwondokei kwa mujibu wa Ijma’a ya ‘Ulamaa.

 

Mwanamke akipata hedhi kabla ya Twawaaf Al-Ifaadhwah

 

Kama ataweza –ikiwa hakuna uzito- kusubiri hadi atwaharike kisha atufu, basi itamlazimu afanye hivyo. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kumwambia ‘Aaishah alipopata hedhi:

 

((افعَلي ما يفعَلُ الحاجُّ، غير ألَّا تطوفي بالبيتِ حتى تطهُرِي))

((Fanya anayoyafanya Hujaji, ila usitufu Nyumba mpaka utwaharike)). [Hadiyth Swahiyh. Takhriyj yake imetajwa nyuma]

 

Sheikh wa Uislamu amesema: “Ama ambalo silijui lenye mzozo ni kuwa haifai mwanamke kutufu akiwa na hedhi kama anaweza kutufu pamoja na utwahara. Simjui mpingaji yeyote asemaye kuwa hilo ni haramu kwake na anapata madhambi kwa kulifanya. Na wao wamevutana kwa upande wa kutoshelezwa na hilo. Madhehebu ya Abu Haniyfah yanasema hilo linamtosheleza, nayo ni kauli katika madhehebu ya Ahmad..” [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/205-206)]

 

Lakini, ikiwa mwanamke huyo hawezi kusubiri mpaka atwaharike ili atufu kwa sababu ameshaweka tarehe ya safari ya kurudi au mfano wa hilo –na hii ndio hali halisi katika nyakati zetu za sasa- basi hatokosa moja kati ya vigawanyo vinane:

 

[Muhtasari wa utafiti murua wa Al-‘Allaamah Ibn Al-Qayyim katika I-‘ilaam Al-Muwaqqi’iyna (3/19) na zinazofuatia].

 

1- Aambiwe: Bakia Makkah mpaka utwaharike na utufu hata kama wanaume watasafiri na kuondoka.

 

Katika hili kuna ufisadi kwa kumwacha abaki peke yake ugenini ambapo anaweza kupata madhara mengi.

 

2- Aambiwe: Twawaaf Al-Ifaadhwah inapomoka kwa kushindikana sharti yake.

 

Hili hakuna wa kulisema, kwa kuwa Twawaaf hii ni nguzo kuu ya Hajj, nayo ndio makusudio yake hasa. Kusimama ‘Arafah na yanayofuatia ni utangulizi wa nguzo hii.

 

3- Aambiwe: Ukihofia hedhi kukujia wakati wa kutufu, basi inajuzu kuifanya kabla ya wakati wake. Na hili hakuna aliyelisema. Ni kama kutanguliza kusimama ‘Arafah kabla ya Siku yake.

 

4- Isemwe: Ikiwa anajua kwa mazoea kuwa siku zake zinamjia katika masiku ya Hajj, basi atasameheka na faradhi ya Hajj mpaka afikie umri wa kutotokwa na damu ya hedhi na ikatike kabisa.

 

Hili litalazimisha kuondosha ufaradhi wa Hajj kwa wanawake wengi, nalo ni batili.

 

5- Isemwe: Arudi kwenye Ihraam yake kwa kujizuia jimai na nikaah mpaka arudi kwenye Al-Ka’abah, atufu akiwa twahara hata baada ya miaka. Na hili ndilo ambalo linarejeshwa na Usuwl ya sharia na yaliyomo ndani yake kati ya rahmah, hikmah na maslaha. Na bila shaka uzito ulioko ndani ya hili haufichiki.

 

6- Isemwe: Atavua Ihraam mpaka atwaharike kama anavyovua Ihraam aliyezuilika asiweze kufanya Hajj pamoja na kusalia Hajj katika dhima yake. Na wakati wowote atakapokuwa na uwezo, basi itamlazimu, na atatufu akiwa twahara. Na hili ni dhaifu kwa kuwa kuzuilika mtu asiweze kufanya Hajj ni jambo linalotokea bila kutarajiwa ambalo linamzuilia Hujaji kufika Makkah katika wakati wa Hajj. Lakini mwanamke huyu ashafika kwenye Al-Ka’abah, kisha udhuru wake haupomoshi faradhi yake ya Hajj. Hivyo kutokewa ghafla na hali hiyo hakumuwajibishii kuvua Ihraam kama inavyofanyika kwa jambo lenye kumzuia asiweze kufika Makkah.

 

7- Isemwe: Ni lazima amtafute mtu wa kumhijia mfano wa mwenye kuugua maradhi sugu yasiyopona na asiyeweza kuhiji. Hili hakuna mwenye kulisema. Halafu, mwenye maradhi sugu, hana tena matumaini ya udhuru wake huo kuondoka, lakini mwanamke huyo hakati tamaa ya kuondoka udhuru wake kwa kuwezekana kukatika kabisa damu yake katika umri wa kufunga damu ya hedhi au kabla yake. Yeye si kama mgonjwa wa maradhi sugu.

 

Makadirio haya yote saba hayafai, ni batili. Hivyo imebidi lipatikane la nane ambalo ni:

 

8- Isemwe: Atatufu Al-Ka’abah –akiwa na hedhi- kwa dharura. Na hili linaendana na roho samehevu ya sharia, na kwa ajili ya kuondosha uzito kwa umma.

 

Ama yaliyosemwa na ‘Ulamaa na Fatwa walizotoa kuhusu kushurutisha mwanamke awe twahara kutokana na hadathi kubwa wakati wa kutufu, haya bila shaka ni katika hali ya kuwa na uwezo na wasaa na si katika hali ya dharura na kushindwa. Kufutu hivi hakupingani na sharia wala kauli za ‘Ulamaa.

 

Na hili ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah –Allaah Amrehemu- ambaye amesema katika kaditama ya utafiti wake: “Hili ndilo lenye mwelekeo zaidi kwa upande wangu katika suala hili, na hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa toka kwa Allaah Al-‘Aliyyu Al-‘Adhiwym. Na lau si kudharurika watu na kulihitajia hilo kivitendo na kielimu, basi nisingejitaabisha kuzungumzia hili pale ambapo sikukuta ndani yake maneno ya mtu mwingine zaidi yangu, kwa kuwa ijtihaad wakati wa dharura ni jambo ambalo Allaah Ametuamuru”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/176-241). Sheikh wetu ameitilia nguvu katika Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/572) na zinazofuatia]

 

Ninasema: “Mwanamke akiweza kutumia dawa ya kuzuia hedhi wakati wa Hajj, basi anaweza kutumia –kama haitomfanyia matatizo- ili kuondokana na mvutano. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

 

3- Twawaaful Widaa (Ya Kuaga)

 

Inajulikana pia kama Twawaaf As-Swadr na Twawaaf Aakhir Al-‘Ahd. Twawaaf hii ni wajibu kati ya nyujubu za Hajj kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa –kinyume na Fuqahaa wa Kimaalik ambao wanasema ni Sunnah-. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) aliyesema: ((Watu wameamuriwa iwe ahadi yao ya mwisho na Nyumba, isipokuwa imesamehewa kwa mwanamke mwenye hedhi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1755) na Muslim (1327)]

 

Na katika tamko: ((Watu walikuwa [baada ya kumaliza Hajj yao] wakitawanyika huku na kule, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:

 

((لا بنفرن أحد حتى يكون آخر عهده بالبيت))

((Asiondoke mtu [Makkah] mpaka ahadi yake ya mwisho iwe [Kutufu] Nyumba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1327)]

 

Hadiyth hii ni dalili juu ya wajibu wa Twawaafu ya Kuaga, na kwamba mwanamke kama atapata hedhi baada ya Twawaaful Ifaadhwah, itamlazimu abakie mpaka atwaharike, na kisha atufu Twawaafu ya Kuaga. Lakini anaruhusiwa kuacha Twawaafu ya Kuaga na kusafiri kurudi kwao na si wajibu kwake kuchinja. Dalili ya hili ni yaliyotangulia nyuma kidogo kuwa Swafiyyah alipopata hedhi, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) alisema:

 

((أحابستنا هي؟))

((Je, yeye katuzuia?)).

 

Wakasema: Yeye ameshatufu Twawaaf Al-Ifaadhwah”. Akasema:

((فلتنفر إذن))

((Basi kama hivyo, aondoke)). [Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (2/154)]

 

Angalizo

 

Ikiwa mwanamke atatwaharika kabla hajasafiri, basi ni lazima atufu Twawaaf ya Kuaga kama bado hajatoka nje ya majumba ya Makkah. Kama atatwaharika naye bado yuko ndani ya Makkah, basi ni lazima atufu Twawaaf hii. [Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (2/154)]

 

Mkazi wa Makkah hana Twawaaf ya Kuaga

 

Twawaaf ya Kuaga si wajibu isipokuwa kwa Hujaji toka nje ya Makkah. Ama mkazi wa Makkah, huyo hana Twawaaf kwa mujibu wa Fuqahaa wa Kihanafiy na Kihanbali, na Mahanafiy wanamuhesabu kuwa mkazi wa Makkah mtu ambaye nyumba yake iko ndani ya mipaka ya Miyqaat, kwa kuwa Twawaaf ni wajibu kwa ajili ya kuaga Nyumba, na wakazi wa Makkah hawana hali hii, kwa kuwa wako mjini kwao.

 

Ama kwa upande wa Maalik na Ash-Shaafiíy, Twawaaf ya Kuaga inatakiwa ifanywe na kila aliyekusudia kusafiri toka Makkah hata kama ni mkazi wa Makkah ikiwa atakusudia safari ya umbali wa kumruhusu kupunguza Swalaah kutokana na ujumuishi wa amri ya kuwa agano la mwisho liwe kwa Nyumba (Al-Ka’abah). [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (17/58)]

 

 

Share