23-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Sunnah Za Kutoka Kwenda Minaa

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

23-Sunnah Za Kutoka Kwenda Minaa

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Hujaji [mwenye kufanya Ifraad katika wakazi wa Makkah au aliyefanya Tamattu’u] ahirimie toka nyumbani kwake Siku ya At-Tarwiyah (Tarehe nane Dhul Hijjah).

 

2- Mahujaji wote waelekee Minaa Siku ya At-Tarwiyah kabla ya Adhuhuri.

 

3- Waswali Adhuhuri na Alasiri, na Magharibi na ‘Ishaa Siku ya At-Tarwiyah.

 

4- Walale Minaa ili waswalie Alfajiri huko na jua la Arafah liwachomozee huko.

 

5- Wahame katika maeneo haya kwa kutumia kipando (gari n.k), na kupanda ni bora kuliko kutembea.

 

6- Afunge Hujaji kijihema kidogo Namirah kama atataka kumwiga Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).

 

Dalili ya Sunan hizi ni yaliyoelezewa katika Hadiyth ya Jaabir: ((..Na ilipokuwa Siku ya At-Tarwiyah, walielekea Minaa, wakahirimia Hajj. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipanda [mnyama], akaswalia huko Adhuhuri, ‘Alasiri, Magharibi, ‘Ishaa na Alfajiri. Halafu alikaa kidogo mpaka jua likachomoza, akaamuru ajengewe kijihema cha manyoya Namirah, na Rasuli wa Allaah akaenda mpaka akafika ‘Arafah..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1218] 

 

7- Alete Talbiyah au Takbiyr wakati anapotoka Minaa kuelekea ‘Arafah. Ni kwa Hadiyth ya Muhammad bin Abiy Bakr Ath-Thaqafiy kuwa alimuuliza Anas bin Maalik –nao wakirauka asubuhi kwenda ‘Arafah toka Minaa-: Vipi mlikuwa mnafanya katika siku hii pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)? Akasema: Alikuwa mmoja wetu analeta Tahliyl naye hamkatazi, na mwenye kuleta Takbiyr naye hamkatazi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1659) na Muslim (1284)]

 

Na toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Tulirauka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) toka Minaa kwenda ‘Arafah, baadhi yetu wakileta Talbiyah na wengine wakileta Takbiyr)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1284)]

 

8- Imamu awahutubie na awabainishie Manaasik za Hajj, na awahimize wakithirishe du’aa na kujinyenyekeza kwa Allaah. Awabainishie mambo muhimu ya lazima ya dini yao na utengemao wa hali zao kama ilivyo katika Hadiyth ya Jaabir. Khutbah hii ni Sunnah kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote, na imesuniwa iwe khutbah moja badala ya mbili ya kukaa kati yake. Ni mashuhuri katika vitabu vya sharia za kivitendo.

 

 

9- Aswali Adhuhuri na ‘Alasiri kwa kukusanya na kupunguza pamoja na imamu huko Namirah (Siku ya ‘Arafah), na asiswali kati ya Swalaah hizi mbili Swalaah nyingine yoyote. [Aliyekosa kuziswali pamoja na imamu, anaruhusiwa kuziswali peke yake kwa kuzikusanya kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Abu Haniyfah amesema haijuzu]

 

 

 

Share