28-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah:

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

28-Al-Hady Wanyama Wa Kuchinja

 

الهدي

Alhidaaya.com

 

 

"الهدي" Ni kinachopelekwa Al-Haram kati ya wanyama na vinginevyo. Na muradi hapa ni wanyama maalum wanaopelekwa Al-Haram kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah. Allaah Amesema:

((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ))

((Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi)). [Al-Hajj (22:36)]

 

Amesema tena:

 

((لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))

((Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Älivyowatiisha kwenu ili mpate kumtukuza Allaah; “Allaahu Akbar, kwa yale Aliyokuongozeni; na wabashirie wafanyao ihsaan)). [Al-Hajj (22:37)]

 

 

Aina ya wanyama

 

‘Ulamaa wamekubaliana wote kuwa mnyama wa kuchinjwa ni lazima awe katika zile jozi nane Alizoziainisha Allaah Subhaanah (katika Aayah ya 143 ya Suwrat Al- An’aam), na mnyama bora kabisa ni ngamia, kisha ng’ombe, halafu kondoo na mbuzi. [Bidaayatul Mujtahid (2/559) na Al-Majmuw’u (8/368)]

 

Na kila mnyama anavyokuwa ghali, basi inakuwa ni bora zaidi, kwani Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipoulizwa kuhusu watumwa: Ni yupi bora zaidi [kwa kuachwa huru?] alisema:

((أغلاها ثمنا، وأنفسها عند أهلها))

((Ni mwenye bei ghali zaidi, na mwenye kuthaminiwa zaidi na watu wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2515), Muslim (136) na wengineo]

 

 

Yaliyoshurutishwa kwa mnyama wa kuchinjwa

 

1- Awe ni katika  "بهيمة الأنعام"

[wanyama wa mifugo] ambao ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo.

 

2- Kondoo awe amekomaa vizuri kwa kutimiza mwaka mmoja na zaidi, wa chini ya hapo hatoshelezi. Ngamia wa chini ya miaka mitano hatoshelezi, wala ng’ombe wa chini ya miaka miwili, wala mbuzi wa chini ya mwaka.

 

Toka kwa Jaabir kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:   

((لا تذبحوا إلا مسنة، إلا أن تعسر عليكم فتذبحوا جذعة من الضأن))

((Msichinje isipokuwa Musinnah [ngamia aliyetimiza miaka mitano au ng’ombe aliyetimiza miaka mitatu], ila kama itakuwa vigumu kwenu, hapo mtachinja kondoo aliyetimiza mwaka)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslmi (1963), Abu Daawuwd (2797), An-Nasaaiy (7/218) na Ibn Maajah (3141)]

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia Abu Burdah kuhusiana na mbuzi mwenye miezi sita:

((تجزئ عنك، ولا تجزئ عن أحد بعدك))

((Anakutosheleza wewe [tu], na hamtoshelezi mwingine yeyote baada yako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5556) na Muslim (1961)]

 

3- Asiwe na kasoro yoyote kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((أربع لا تجزئ في الأضاحي: العوراء البين عورها، والمريضة البين مرضها، والعرجاء البين ظلعها والكسيرة التي لا تنقي))

((Wanne hawafai katika wanyama wa kudhwahi: Mwenye chongo linaloonekana bayana, mwenye ugonjwa wa dhahiri, kiwete asiyeweza kutembea, na dhaifu [gofu] asiye na mifupa imara)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2785), At-Tirmidhiy (1530), An-Nasaaiy (7/214) na Ibn Maajah (3144)]

 

Kasoro za wanyama zinaweza kugawanywa vigawanyo vitatu: [Ash-Sharhul Mumti’u ‘Alaa Zaadil Mustanqa’i (7/467-477)]

 

(a) Ziwe kasoro nne zilizoainishwa kwenye Hadiyth iliyotangulia. Kasoro hizi zinabatilisha utoshelezo.

 

(b) Ziwe zimetangaziwa katazo lakini zinaweza kutosheleza. Na hawa ni wanyama wenye kasoro kwenye masikio yao, pembe zao na mfano wa hivyo. Ni kama Hadiyth ya ‘Aliyy bin Abiy Twaalib:

 

((أَمَرَنَا رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم أَنْ نَسْتَشْرِفَ الْعَيْنَ وَالْأُذُنَ، وألا نُضَحِّي بِمُقَابَلَةٍ، ولا مُدَابَرَةٍ، ولا خَرْقَاءَ))

((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ametuamuru tukague macho na masikio [tunaponunua wanyama], na tusidhwahi aliyekatwa sikio kwa mbele likaachwa likining’inia, wala aliyekatwa sikio kwa nyuma, wala aliyepasuliwa sikio kwa urefu, wala aliyetobolewa sikio)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2804), At-Tirmidhiy (1543), An-Nasaaiy (7/217) na Ibn Maajah (3142)]

 

Wanyama wenye kasoro hizi ni makruhu kudhwahi lakini wanakidhi lengo.

(c) Ziwe kasoro ambazo hazikukatazwa lakini zinaharibu kidogo ukamilifu wa mnyama. Hizi hazina athari, lakini ni makruhu, na si haramu. Ni kama aliyevunjika meno na mfano wa hivyo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Wanyama ni wa aina mbili

 

‘Ulamaa wamekubaliana wote kuwa mnyama anayeswagwa kwenye ‘ibaadah hii, yuko wa Waajib na yuko wa Sunnah.

 

1- Wa Waajib

 

Hawa wako katika vigawanyo vifuatavyo:

 

(a) Mnyama wa Tamattu’u na Qiraan. Huyu ni yule aliye waajib kwa Hujaji aliyefanya ‘Umrah kwanza kisha Hajj (Tamattu’u), au aliyefanya Hajj na ‘Umrah kwa pamoja (Qiraan). Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa: 

 

((فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ))

((Basi mwenye kufanya Tamattu’u kwa kutekeleza ‘Umrah kwanza kisha Hajj, achinje mnyama aliye mwepesi. Na asiyepata afunge Swiyaam siku tatu katika Hajj na saba mtakaporejea)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Mnyama huyu ni waajib kwa mwenye kufanya Tamattu’u kwa Ijma’a, na kwa mwenye kufanya Qiraan kwa kauli ya Jumhuri.

 

 

(b) Mnyama wa fidia. Huyu ni yule aliye waajib kwa Hujaji akinyoa nywele zake kutokana na ugonjwa au wadudu wanaomsumbua. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِّن رَّأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِّن صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ))

((Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake (ikambidi anyoe); basi atoe fidia kwa kufunga Swiyaam au kutoa swadaqah au kuchinja mnyama)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Hujaji huyu atakhiyarishwa baina ya kuchinja, au kulisha, au kufunga kama ilivyotangulia.

 

Jumhuri wameunganisha aina hii kuwajibisha kuchinja kwa mwenye kuacha waajib katika waajibaat za Hajj, na kwa mwenye kufanya katazo lolote kati ya makatazo ya Ihraam.

 

(c) Mnyama wa malipo. Ni yule ambaye ni waajib kwa Muhrim aliyeua mnyama wa kuwindwa wa nchi kavu, na hili lishaelezwa nyuma. Wamelifanyia hili Qiyaas kuchinja kwa mwenye kufanya marufuku yoyote kati ya marufuku katika Al-Haram kama kukata mti na mfano wake.

 

(d) Mnyama wa kuzuilika. Ni yule aliye waajib kwa aliyezuilika asiweze kukamilisha ‘amali za Hajj kutokana na ugonjwa au adui au mfano wa hayo, na hakuwa ameweka shuruti wakati wa kuhirimia –kama tulivyoeleza nyuma- kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((Na kama mkizuilika basi chinjeni wanyama walio wepesi kupatikana)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

(e) Mnyama wa kumwingilia mke. Ni yule aliye waajib kwa Hujaji anapomwingilia mkewe wakati wa Hajj. Na hili lishaelezwa nyuma.

 

(f) Mnyama wa nadhiri. Huyu ni waajib kwa aliyemwekea nadhiri.

 

 

2- Wa Kujitolea

 

Ni yule ambaye Hujaji mwenye kufanya Ifraad anajitolea tu (kama swadaqah) zaidi ya mnyama wa waajib.

 

 

Kumpeleka mnyama Haram kwa asiyetaka kwenda mwenyewe

 

Atakayekuwa kwenye mji wake na hakutaka kwenda Haram, basi imestahabiwa ampe mtu mwingine mnyama huyo ampelekee huko. Imestahabiwa pia amvishe vigwe na amtie alama kama tutakavyokuja kuona mbeleni.  Na akimpeleka, hawi kwa kufanya hivyo Muhrim, na wala hakatazwi kufanya lolote katika mambo yaliyokatazwa kwa Muhrim. Hii ni kauli ya Jumhuri.

Toka kwa ‘Aaishah amesema:

 

((فَتَلْتُ قَلائِدَ بدن رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم بيدي ثُمَّ أَشْعَرْتُهَا وَقَلَّدَهَا - أَوْ قَلَّدْتُهَا - ثُمَّ بَعَثَ بِهَا إلَى الْبَيْتِ . وَأَقَامَ بِالْمَدِينَةِ , فَمَا حَرُمَ عَلَيْهِ شَيْءٌ كَانَ لَهُ حِلاُّ))

((Nilivisuka vigwe vya ngamia wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa mikono yangu miwili, kisha nikamtia alama na yeye akamvisha vigwe –au nilimvisha mimi vigwe- halafu akamtuma [mtu pamoja naye) kumpeleka kwenye Nyumba, naye akakaa Madiynah, na halikuwa katazo kwake jambo lolote lililokuwa ni halali)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1696) na Muslim (1321)]

 

 

Ni wanyama wangapi wanatosheleza?

 

Hakuna mpaka maalum wa wingi wa wanyama wa kuchinja. Wanyama aliochinja Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) walikuwa ni mia moja. Toka kwa ‘Aliyy: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alichinja ngamia mia..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1718)]

 

Idadi ya chini kabisa inayomtosha mtu mmoja ni mbuzi mmoja. Toka kwa Abu Ayuuwb Al-Answaariyy: ((Mtu katika enzi ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anajichinjia mbuzi mwenyewe na kwa watu wa nyumba yake, wanakula na wanalisha. Kisha watu wakajifaharisha, na wakawa kama unavyoona)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1541) na Ibn Maajah. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

Na katika Hadiyth ya ‘Aaishah, ni kuwa: ((Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimchukua kondoo dume akamlaza chini, kisha akasema:

((اللهم تقبل من محمد وآل محمد))

((Ee Allaah! Taqabal kutoka kwa Muhammad na ukoo wa Muhammad)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1967)]

 

Na hii ni kwa mnyama wa kudhwahi.

 

‘Ulamaa wote wamekubaliana kuwa kondoo mmoja hatoshelezi isipokuwa kwa mtu mmoja tu, tofauti na yaliyosimuliwa toka kwa Maalik kuwa anatosheleza ikiwa mtu atajichinjia mwenyewe na watu wa nyumba yake, lakini si kwa ushirika, bali akimnunua peke yake. [Bidaayatul Mujtahid (1/655)]

 

Watu saba wakishirikiana ngamia au ng’ombe mmoja itawatosheleza. Hii ni kauli mashuhuri ya Ash-Shaafi’iy toka kwa Ahmad. Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema: ((Tulichinja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) Mwaka wa Al-Hudaybiyyah ngamia jike kwa watu saba, na ng’ombe kwa watu saba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1318)].  

 

Na toka kwa Jaabir tena: ((Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) tukihirimia Hajj…na akatuamuru tushirikiane katika ngamia na ng’ombe, kila watu saba kati yetu ngamia mmoja)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1318)]

 

Ibn Rushd amenukuu Ijma’a ya kuwa haijuzu kushirikiana watu zaidi ya saba katika kuchinja mnyama. [Bidaayatul Mujtahid (1/656]

 

Ninasema: “Bali Is-Haaq ameelekea kusema kuwa ngamia mmoja na ng’ombe mmoja wanatosheleza watu kumi. Katika Hadiyth ya ‘Aaishah: ((..tulipokuwa Minaa, nililetewa nyama ya ng’ombe, nikasema: Hii ya nini? Wakasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amechinja ng’ombe kwa niaba ya wakeze)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1623) na Muslim (1211)]

 

Na wakeze ni tisa.

 

Na imeelezewa katika baadhi ya riwaya kuwa alikuwa ng’ombe mmoja baina yao. [Hadiyth Mursal. Imekharijiwa na Maalik (2/486-487]

 

Na imethibiti kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aligawa ghanima (ngawira) na akamlinganisha ngamia mmoja sawa na mbuzi kumi. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2507), Muslim (1968) na wengineo]

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas: ((Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika safari, ikawadia [siku ya] Adhwhaa, tukashirikiana watu kumi ngamia, na watu saba ng’ombe)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (907), An-Nasaaiy (7/222) na Ibn Maajah (3131)]

 

Na Hadiyth hizi zinabambanuliwa (zinakharijiwa) katika moja ya njia tatu: [Zaad Al-Ma’aad cha Ibn Al-Qayyim (2/266-267)]

 

1- Ima isemwe: Hadiyth zinazosema watu saba washirikiane ngamia mmoja au ng’ombe mmoja ndizo nyingi zaidi na Swahiyh zaidi.

 

2- Au isemwe: Kumsawazisha ngamia mmoja na kondoo kumi, ni tathmini ya kuleta uwiano sawa katika mgawo wa ghanima. Ama kuwa kwa watu saba katika wanyama wa kuchinja kwenye Hajj, hayo ni makadirio ya kisharia.

 

3- Na ima isemwe: Kuwa hilo linatofautiana kwa kutofautiana zama, mahala na ngamia. Katika baadhi ya nyakati, ngamia mmoja alikuwa sawa na mbuzi kumi, akamfanya kwa watu kumi, na nyakati nyingine alikuwa sawa na mbuzi saba, akamfanya kwa watu saba. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Wakati wa kuchinja

 

Imestahabiwa kuchinja Yawm An-Nahr (10 Dhul Hijjah) baada ya kutupia Jamaratul ‘Aqabah, na kabla ya kunyoa na kutufu kama ilivyotangulia. Ama wakati wa kujuzu, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kwa kauli mbalimbali: [Al-Mabsuwtw (12/9), Al-Ummu (2/217), Al-Inswaaf (4/87), Al-Majmuw’u (8/390) na Az-Zaad (2/318)]

 

1- Inajuzu kuchinja Yawm An-Nahr na siku tatu baada yake. Hii ni kauli ya ‘Aliyy bin Abiy Twaalib, na madhehebu ya Al-Hasan Al-Baswriy, ‘Atwaa, Al-Awzaa’iy na Ash-Shaafi’iy. Ni chaguo la Ibn Al-Mundhir, Ibn Taymiyah na Ibn Al-Qayyim. Hoja yao ni Hadiyth:

 

((كل أيام التشريق ذبح))

((Masiku yote ya Tashriyq ni kuchinja)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ahmad (4/82) na Ibn Hibaan (1008) kwa Sanad Munqatwi’u]

 

Na kwa kuwa siku tatu ni mahususi kama Siku za Minaa, Siku za Kutupia, Siku za Tashriyq, na ni haramu kuzifunga, hivyo siku hizi ni ndugu katika hukmu hizi, haziwezi kutenganishwa katika kujuzu kuchinja bila Aayah au Hadiyth au Ijma’a.

 

 

2- Wakati wake ni Yawm An-Nahr na siku mbili baada yake. Ni madhehebu ya Ahmad. Maalik na Abu Haniyfah. Pia ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na Swahaba zaidi ya mmoja. Hoja yao ni kuwa imekatazwa kuzivundika nyama za Adhwaahiy kwa zaidi ya siku tatu.

Wamesema hii ni dalili kuwa siku za kuchinja ni tatu tu. Lakini kauli hii ina walakini, kwa kuwa katazo la kuvundika zaidi ya siku tatu, halizuii kuchinja baada ya siku tatu.

 

3- Wakati wa kuchinja ni siku moja tu, kwa kuwa siku imeambatika na jina lenyewe, na hivyo hukmu yake imeambatanishwa nayo. Ni kauli ya Ibn Siyriyna.

 

4- Ni siku moja tu kwa mijini na siku tatu kwa Minaa. Ni kauli ya Sa’iyd bin Jubayr na Jaabir bin Zayd. Kwa kuwa Minaa kuna matendo ya Manaasik kama kutupia Jamaraat, Kutufu na kunyoa. Hivyo yamekuwa ni siku za kuchinja kinyume na watu wa mijini.

 

5- Ni kuanzia Yawm An-Nahr hadi mwisho wa Dhul Hijjah. Kauli hii imesimuliwa toka kwa Abu Salamah bin ‘Abdur Rahmaan na An-Nakha’iy.

 

6- Hakuna wakati maalum. Ni mwono wa Ash-Shaafi’iy, na An-Nawawiy ameudhoofisha. [Al-Majmuw’u (8/348-349)]

 

Ninasema: “Inaonekana wazi kuwa siku za kuchinja ni nne: Yawm An-Nahr na siku tatu baada yake za At-Tashriyq. Hili limepitishwa kwa wingi na Baraza la Bodi ya ‘Ulamaa Wakuu wa Saudia (azimio no. 43 la tarehe 13/4/1396 Hijriyyah)”. [Tawdhwiyhul Ahkaam cha Bassaam (3/374)]

 

 

Mahala pa kuchinjia

 

Allaah Mtukufu Amesema:

((ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ))

((Kisha [mahala pa] kuhalalika kwake kuchinjwa ni kwenye Nyumba ya Kale)). [Al-Hajj (22:33)]

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alichinja mahala pake pa kuchinjia Mina, na akasema:

((نحَرْتُ هَا هُنَا، وَمِنًى كُلهَا مَنْحَرٌ، فَانْحَرُوا فِي رِحَالِكُمْ))

((Nilichinja hapa, na Mina yote ni mahala pa kuchinjia, basi chinjeni majumbani mwenu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1218) toka kwa Jaabir]

 

Na katika tamko jingine:

((وكل منى منحر، وكل المزدلفة موقف، وكل فجاج مكة طريق ومنحر))

((Na Mina yote ni mahala pa kuchinjia, na Muzdalifah yote ni sehemu ya kisimamo, na barabara zote za Makkah ni njia na mahala pa kuchinjia)). [Isnaad Yake ni Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1937), Ibn Maajah (3048) na Ahmad (3/326)]

 

Hivyo basi, mnyama hachinjwi isipokuwa katika Al-Haram. Atakayechinja mahala popote ndani ya Al-Haram, -ndani ya Makkah au penginepo- basi itamtosheleza kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Lakini Maalik amesema haitoshelezi katika Al-Haram isipokuwa Makkah tu akishikimana na udhahiri wa Kauli Yake Ta’aalaa:

((هَدْيًا بَالِغَ الْكَعْبَةِ))

((Mnyama huyo afikishwe Ka’bah)).

 

Na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ni hujja dhidi yake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Je, inajuzu kuhamisha nyama za adhwaahi nje ya Al-Haram?

 

Baraza la Bodi ya ‘Ulamaa wa Saudia katika azimio lake (nambari 77) tarehe 21/10/1400 Hijria limesema:

 

Wanyama anaochinja Hujaji ni wa aina tatu:

 

1- Mnyama wa kufanya Tamattu’u au Qiraan. Huyu inajuzu kuhamisha nyama yake nje ya Al-Haram. Swahaba (Ridhwaanu Allaah ‘alayhim) walichukua sehemu ya nyama za wanyama wao waliowachinja kwenda nazo Madiynah. Katika Swahiyh Al-Bukhaariy toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah amesema: ((Tulikuwa hatuli nyama za ngamia wetu zaidi ya siku tatu Minaa, na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaturuhusu akituambia:

((كلوا وتزودوا، فأكلنا وتزودنا))

((Kuleni na chukueni masurufu ya safari, tukala na tukabeba masurufu ya safari)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1719) na Muslim (1972)]

 

2- Mnyama anayemchinja Hujaji ndani ya Al-Haram kama malipo ya kuwinda, au fidia ya kuondosha adha, au kufanya lililokatazwa, au kuacha la waajib. Aina hii haijuzu kabisa kuhamisha nyama yake kupeleka kwengine, kwa kuwa nyama yote ni kwa masikini wa Al-Haram.

 

3- Mnyama aliyechinjwa nje ya mipaka ya Al-Haram kama wa fidia ya malipo, au wa kuzuilika, au mwingine wa kuwezekana kuchinjwa nje ya Al-Haram. Huyu nyama yake hugawiwa pale alipochinjwa, na pia haikatazwi kuihamisha toka mahala alipochinjwa kupelekwa kwengine. [Tawdhwiyhul Ahkaam (3/311-312)]

 

 

Kuwaswaga wanyama

 

Inajuzu kwa Hujaji amnunue mnyama wake katika eneo la Al-Haram. Pia inajuzu amlete (amswage) toka nje ya Al-Haram. Na akimswaga, imestahabiwa amfunge vigwe na amtie alama –kama ni ngamia au ng’ombe- bila makhitalifiano yoyote. Vigwe ni kamba au kipande cha ngozi ambacho hufungwa shingoni ili ajulikane kuwa ni mnyama wa kudhwahi. Ama kutiwa alama, ni kupasuliwa upande mmoja wa nundu ya ngamia au ng’ombe damu ikachuruzika, na hiyo inakuwa ni alama ya kuwa ni mnyama wa kudhwahi. Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamestahabisha apasuliwe upande wa kulia.  

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema:

 

صَلَّى رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم الظهْرَ بِذِي الْحُلَيْفَةِ، ثُمَّ دَعَا بِبدنة فَأَشْعَرَهَا من صَفْحَةِ سَنَامِهَا الأَيْمَنِ، وَسَلَتَ الدَّمَ عنها، وَقَلَّدَهَا بنَعْلَيْنِ، ثُمَّ رَكِبَ رَاحِلَتَهُ، فَلَمَّا اسْتَوَتْ بِهِ عَلَى الْبَيْدَاءِ، أَهَلَّ بِالْحَجَّ

((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliswali Adhuhuri Dhul Hulayfah, kisha akaitisha ngamia wake, akamtia alama upande wa kulia wa nundu yake, akampangusa damu yake, na akamfungia viatu viwili. Kisha alimpanda ngamia wake, na alipokaa sawa naye juu ya Al-Baydaa, alinyanyua sauti yake kuleta Talbiyah kwa ajili ya Hajj)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1234), Abu Daawuwd (1752) na An-Nasaaiy (5/170-171)]

 

 

Je. mbuzi na kondoo huvishwa vigwe?

 

Maalik na Abu Haniyfah wamesema mbuzi na kondoo hawavishwi vigwe. Na Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Abu Thawr na Daawuwd wamesema wanavishwa kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipeleka mara moja kondoo wa kudhwahi, akamvisha vigwe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1701) na Muslim (1331)]

 

 

Kuwasimamisha wanyama wa kudhwahi ‘Arafah (na kuwatambulisha)

[Al-Muhallaa (7/166/167) na Bidaayatul Mujtahid 1/561-562)]

 

Maalik anaona kuwa mnyama wa kudhwahi anayenunuliwa Haram hatoshelezi mpaka asimamishwe ‘Arafah. Na kama atanunuliwa sehemu ambayo marufuku za Ihraam zinaruhusika kisha akaingizwa Haram basi itatosha hata kama hakusimamishwa ‘Arafah.

 

Allayth kasema: Hawi mnyama wa kudhwahi ila aliyevikwa njuga, aliyepasuliwa alama na akasimamishwa ‘Arafah. Na huja yake ni Hadiyth ya Twaawuws: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimtia alama ngamia)). Lakini Hadiyth si Swahiyh. [Hadiyth Dhwa’iyf. Angalia Al-Muhallaa (7/166)]

 

Ash-Shaafi’iy, Ath-Thawriy na Abu Thawr wamesema kuwa kusimama mnyama wa kudhwahi ‘Arafah ni Sunnah, na hakuna ubaya kumwacha, ni sawa akiwa ni mwenye kuingia toka sehemu iliyohalalishwa marufuku au hakuwa.

Abu Haniyfah kasema: Kumtia alama mnyama si Sunnah.

 

Ninasema: “La sawa ni kuwa akisimama na mnyama wa kudhwahi (‘Arafah) basi ni jambo jema, na kama hakusimama naye, basi hapana ubaya.  Ibn Hazm kasema: “Haikuja amri yoyote ya kutia alama katika hilo kutoka kwenye Qur-aan au Sunnah. Na haliwi waajib ila Aliloliwajibisha Allaah katika moja ya mawili, na hakuna pia Qiyaas kinachowajibisha hilo, kwa kuwa Manaasik za Hajj ndizo zenye kuwawajibikia watu na si ngamia”.

 

Alaa kulli haal, utiaji alama na uvikaji wanyama vigwe katika nyakati zetu za sasa ni jambo lenye uzito na tabu kubwa, hivyo watu wasijibebeshe hilo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Uchinjaji wa wanyama

 

‘Ulamaa wamekubaliana kuwa uchinjaji wa wanyama wa kufugwa ni "نحر" (chinjo la mwenye shingo ndefu kama ngamia) na "ذبح" (chinjo la mwenye shingo fupi kama ng’ombe), na kuwa "ذبح" ni Sunnah kwa mbuzi na kondoo, na "نحر" kwa ngamia. Tofauti kati ya "النحر" na "الذبح" itaelezwa kwa ubayana katika mlango wa wanyama wa kudhwahi. [Bidaayatul Mujtahid (1/670)]

 

 

Sunnah ya kumchinja mwenye shingo ndefu

 

Kati ya Sunnah ya kumchinja mwenye shingo ndefu ni kuchinjwa akiwa amesimamishwa na amefungwa. Allaah Amesema:

((فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ))

Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa). [Al-Hajj: 36]

 

Ibn ‘Abbaas kasema: Yaani wamesimama kwa miguu mitatu. [Al-Hajj (22:36)]

 

Na toka kwa Ziyaad bin Jubayr: ((Kwamba Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alimwendea mtu aliyekuwa anamchinja ngamia wake aliyepiga magoti akamwambia: Msimamishe akiwa amefungwa [mguu wake wa mbele wa kushoto], ni Sunnah ya Nabiy wenu (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1713), Muslim (1320) na Abu Daawuwd (1767)]

 

Na toka kwa Jaabir: ((Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na Swahaba Zake walikuwa wakichinja ngamia akiwa amefungwa mguu wake wa mbele wa kushoto na kusimama kwa iliyobakia)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1767)]

 

 

Ama ng’ombe, mbuzi na kondoo, hawa imestahabiwa kuwachinja kwa kuwalaza kwa ubavu wa kushoto, kuuacha huru mguu wa mbele wa kulia, na miguu mitatu ifungwe kamba kwa namna ambayo itabainishwa kwenye mlango wa wanyama wa kudhwahi.

 

 

Manufaa ambayo mwenye mnyama anaweza kunufaika nayo kutokana na mnyama wake

 

Nufaiko la kwanza: Kula nyama yake anapofika mahala halali pa kuchinjwa. Allaah Mtukufu Amesema:

((فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ))

((Basi kuleni humo, na lisheni mwenye shida fakiri)). [Al-Hajj (22:28)]

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na kula nyama ya mnyama ambaye ni wa waajib. Abu Haniyfah amesema: “Haliwi mnyama wa waajib isipokuwa mnyama wa Tamattu’u na Qiraan”. [Al-Hidaayah (1/186)]

 

Na hii ni kauli ya Fuqahaa wengi wa Kihanbal. [Al-Mubdi’u (3/124), Al-Inswaaf (3/439), na Al-Furuw’u (3/378)]

 

Maalik kasema: “Wanyama wote wa waajib huliwa isipokuwa wa malipo ya kuwinda, nadhiri ya masikini na fidia ya adha”. [Bidaayatul Mujtahid (1/565) na Al-Kharshiy (2/378)]

 

Ash-Shaafi-’iy kasema: “Mnyama wa waajib haliwi wote, bali nyama yake yote ni kwa masikini”. [Rawdhwat At-Twaalibiyna (3/191)]

 

Ninasema: “Mnyama anayefanana na wa kafara, nyama yake hailiwi kwa kuwa ‘Ulamaa wamekubaliana kuwa mwenye kafara hali chochote cha mnyama wake. Na hili liko wazi katika mnyama wa malipo ya kuwinda, fidia ya adha na damu nyingine za kukarabati na kuunga kosa. Ama ambaye ni damu ya Nusuk, basi mnyama huyo kimsingi ni wa ‘ibaadah na si damu ya kukarabati na kuunga kosa, na huyu nyama yake huliwa. Na mnyama wa Tamattu’u na Qiraan, huyo ni wa Nusuk –kwa kauli yenye nguvu- ambaye amewajibishwa na sharia kwa ajili ya kumshukuru Allaah Ta’aalaa kwa neema Aliyomtunuku Hujaji kwa kumwepesishia kufanya Hajj na ‘Umrah katika safari moja. Na linalotilia nguvu hili ni kuwa tokea awali sababu ya kuunga kosa ilikuwa ni marufuku wakati ambapo Tamattu’u imeruhusiwa bila pingamizi yoyote. Na kama damu yake ingekuwa damu ya kuunga kosa, basi Tamattu’u isingelijuzu kabisa. Na haya ni madhehebu ya Mahanafiy na Mahanbali wengi, na chaguo la Ibn Taymiyah”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/82)]

 

‘Ulamaa wa Kishaafi-’iy na Maalik wanasema ni damu ya kukarabati kosa isipokuwa Wamaalik wamejuzisha kula. Mwelekeo wa kwanza una nguvu zaidi, kwani imethibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikula kidogo nyama ya mnyama wake na yeye alikuwa amefanya Qiraan. Na katika Hadiyth ya Jaabir: ((…kisha akaamuru kwa kila ngamia lichukuliwe fungu, nikayatia kwenye chungu, nikayapika, wakala nyama yake na wakanywa supu yake..)). [Al-Majmuw’u (7/176), Ar-Rawdhwah (3/47) na Ash-Sharhul Kabiyr ma’a Haashiyat Ad-Dusuwqiy (2/84)]. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Ama mnyama wa swadaqah, huyu huliwa sehemu ya nyama yake kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa –akifikia mahala pa kuchinjwa- kama baki ya watu wengine.

 

Na ikiwa mnyama atapata adha hatarishi kwa maisha yake kabla hajafika sehemu ya kuchinjwa, basi atamchinja na atawaachia nyama yake watu wengine wale (na si watu wa msafara wake). Toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Abu Qubayswah alimhadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akimtuma kumpelekea ngamia kisha humwambia:

 

((إن عَطِب منها شيءٌ، فخشيت عليها موتًا، فَانْحَرها، ثم اغْمِس نعلَها في دمِها، ثم اضرب صفحتها، ولا تَطْعَمها أنت ولا أحدٌ من أهل رُفْقَتِك))

((Kama ataumia sehemu yoyote ya mwili wake ukakhofia atakufa, basi mchinje, kisha kitoteshe kigwe chake ndani ya damu yake, halafu pakaza damu ubavuni mwake, na wala usile wewe wala yeyote katika watu wa msafara wako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1326), Ibn Maajah (1036) na Abu Daawuwd (1763)]

 

Sababu ya yeye na watu wa msafara wake kukatazwa kula nyama hiyo ni kuchelea wao kumjeruhi mnyama ili achinjwe wapate kula nyama kabla ya wakati wake.

 

Nufaiko la pili: Kumpanda kwa mwenye kuhitajia hilo

 

Inajuzu kumpanda mnyama wa kudhwahi kama Hujaji atahitajia kumpanda. Atampanda kwa mujibu wa hali inavyoruhusu bila kumuumiza au kumdhuru. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi-’iy kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

((لَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ))

((Katika hao (wanyama) mnapata humo manufaa mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Kisha kuhalalika kwake kuchinjwa ni kwenye Nyumba ya Kale. (Haram ya Makkah)). [Al-Hajj (22:33)]

 

Kati ya manufaa hayo ni kumpanda. Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwona mtu anamswaga ngamia [naye kachoka sana], akamwambia: “Mpande”. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Huyu ni ngamia [wa kuchinjwa Ka’abah]. Akamwambia:

((اركبها ويلك))

((Mpande, we vipi wewe.)) katika mara ya pili au ya tatu. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1689), Muslim (1322) na wengineo]

 

Na toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah –ambaye aliulizwa kuhusu kumpanda mnyama wa kudhwahi- akasema: ((Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:

((اركبها بالمعروف إذا ألجئت إليها حتى تجد ظهراً))

((Mpande bila kumdhuru ukilazimika kwa hilo mpaka upate mgongo [wa mnyama mwingine wa kupanda])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1324), Abu Daawuwd (1761) na An-Nasaaiy (2/147)]

 

Abu Haniyfah, Maalik, Ahmad, Is-Haaq na Adh-Dhwaahiriyyah wanasema kuwa atampanda hata kama hahitajii kupanda. Na Hadiyth ya Jaabir inawarudi. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (4/806)].

 

 

Mchinjaji halipwi kutokana na mnyama

 

Haijuzu mchinjaji kupewa malipo yake ya kuchinja kutokana na mnyama aliyechinjwa, lakini inajuzu kumpa nyama kama swadaqah baada ya kumpa malipo yake. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aliyy (Radhwiya Allaah ‘anhu): ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliniamuru nisimamie ngamia, nigawe ngozi yake na matandiko yake, na akaniamuru nisimpe mchinjaji chochote kutokana na mnyama. Akasema: Sisi tunampa kutoka kwetu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1717), Muslim (1317) na wengineo]

 

 

Kufunga kwa asiyeweza kuchinja

 

Mwenye kufanya Qiraan na Tamattu’u ni lazima achinje kama ilivyotangulia nyuma, na kama hana fedha za kununulia mnyama au hakuweza kumpata, basi atafunga siku tatu akiwa Hajj na siku saba atakaporejea kwao nyumbani kama Alivyosema Ta’alaa:

 

((فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ))

((Basi mwenye kufanya Tamattu’u kwa kutekeleza ‘Umrah kwanza kisha Hajj, achinje mnyama aliye mwepesi. Na asiyepata afunge Swiyaam siku tatu katika Hajj na saba mtakaporejea)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar, Nabiy (Swalla Allaah ‘ alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((فمن لم يجد هديا فليصم ثلاثة أيام في الحج وسبعة إذا رجع إلى أهله))

((Ambaye hakupata mnyama, basi afunge siku tatu katika Hajj na saba akirejea kwa watu wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1691) na Muslim (1227)]

 

Ni wakati gani anafunga siku tatu?

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu siku hizi tatu zinazofungwa katika Hajj kwa kauli nyingi. Mashuhuri zaidi ni kauli mbili:

 

Ya kwanza: Inahalalika kuzifunga tokea anapohirimia ‘Umrah katika miezi ya Hajj, na imestahabiwa ziwe kuanzia tarehe saba Dhul Hijjah, Siku ya Tarwiyah na Siku ya ‘Arafah. Kauli hii imekhitariwa na Ibn Taymiyah, na ni madhehebu ya Mahanafiy na Mahanbali. Ahmad amenukuliwa akisema kuwa lililo bora zaidi ni siku ya mwisho iwe Siku ya Tarwiyah (tarehe nane). [Fat-hul Qadiyr (2/529), Al-Inswaaf (3/512) na Al-Mubdi’u (3/175)]

Na ikiwa mtu atasema, Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

 ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ  

 

((Siku tatu katika Hajj)),

 

ataambiwa na’am, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((دخلت العمرة في الحج))

((‘Umrah imeingia ndani ya Hajj)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]

 

Ya pili: Haijuzu kufunga ila baada ya kuhirimia Hajj. Ni madhehebu ya Maalik, na Ash-Shaafi-iy. [Ash-Sharhul Kabiyr ma’a Haashiyati Ad-Dusuwqiy (2/84) na Al-Majmuw’u (7/186)]

 

Dalili ni Kauli Yake Ta’aalaa:

((ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ))

((Siku tatu katika Hajj)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar.

 

Ninasema: “Kauli zote mbili zina mwelekeo murua unaobeba maana yumkinivu ya Aayah Tukufu. Kauli ya kwanza haina kipingamizi, lakini ni lazima kuzingatia yafuatayo: [Yamedokolewa toka kwenye Kitabu cha Ash-Sharhul Mumti’u (7/208)]

 

(a) Haitakikani kuhirimia Hajj kutangulizwe kabla ya Siku ya Tarwiyah (tarehe nane) kwa ajili ya kufunga, kwani hivi ni kinyume na Sunnah kama tulivyotangulia kuelezea. Na dhana topezi ni kuwa baadhi ya Swahaba waliohirimia na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) Siku ya Tarwiyah, walikuwa ni masikini bila wanyama, na hawakutanguliza Ihraam ya Hajj.

 

(b) Haitakikani Hujaji afunge Siku ya ‘Arafah kwa kuwa ni kinyume na Sunnah kama ilivyoelezwa nyuma. Akitaka anaweza kufunga tarehe sita, saba na Siku ya Tarwiyah kama alivyosema Ahmad na kukhitariwa na Ibn Baaz (Rahimahuma-Allaah).

 

(c)   Linaloonekana ni kuwa Swahaba walikuwa wakizifunga katika Siku za Tashriyq kama linavyofahamika hilo kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar na ‘Aaishah: ((Haikuruhusiwa katika Siku za Tashriyq kuzifunga isipokuwa kwa ambaye hakupata mnyama)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1997)]

 

Hili ndilo la akiba na salama zaidi, na kwalo Hujaji atajinasua toka kwenye mvutano.

 

(d) Haijuzu kuchelewesha kuzifunga siku hizo tatu baada ya Siku za Tashriyq, kwa kuwa siku zinazofuatia baada yake, si siku za Hajj.

 

(e) Akifunga kabla ya Siku za Tashriyq halazimishwi azifunge mfululizo, kwa kuwa Aayah haikuweka mabano ya kufunga mfululizo. Kiilivyo, Aliloliachilia Allaah na Rasuli Wake bila kuliwekea mpaka linaachiliwa kama lilivyo bila kuliwekea mpaka. Lakini kama ataanza kufunga katika Siku ya kwanza ya Tashriyq, hapo itamlazimu kufuatanisha ili Swawm yake iwe ndani ya Siku za Hajj. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Aliyezuilika kama hana mnyama

 

Tumeeleza nyuma kuwa aliyezuilika asiweze kukamilisha Hajj yake –na hakuwa ameweka shuruti katika Ihraam yake- basi huyo ni lazima achinje kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:   

 

 ((فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((Na kama mkizuilika basi chinjeni wanyama walio wepesi kupatikana)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Mnyama huyo atamchinja mahala pale alipozuilika, halafu atanyoa nywele zake. Toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Tulitoka na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwenda kufanya ‘Umrah, na makafiri wa Kiqureshi wakaizuia Nyumba. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamchinja ngamia wake na akanyoa kichwa chake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1997)]

 

Na kama hakuweza au hakumpata, basi la sawa ni kuwa atavua Ihraam, na hatodaiwa chochote, si Swawm wala kingine. Ama mwenye kufanya Qiyaas kwa mnyama wa Tamattu’u, hili tunaweza kulipembua kwa njia hizi:

 

1- Katika ‘Umrah ya Hudaybiyah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa pamoja na Swahaba wake wengi wakiwemo masikini kati yao. Na haikuripotiwa kuwa aliwaamuru kufunga siku kumi wale ambao hawakuweza kupata mnyama. Hao kiasili hawadaiwi lolote.

 

2- Ni kuwa hukmu ya Tamattu’u na kuzuilika ipo kwenye Aayah moja [Al-Baqarah 196]. Allaah Ameitaja badali ya kutokuwa na mnyama wa kuchinja katika Tamattu’u [ambayo ni kufunga siku 10] na Hakuitaja katika kuzuilika, bali Amehamia kwenye hukmu nyingine Akisema

  وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ

((Na wala msinyoe vichwa vyenu)),

 

na hivyo kuonyesha kuwa aliyezuilika ambaye hana mnyama, hadaiwi chochote. Hivyo Qiyaas kinakinzana na Aayah.

 

3- Ni kuwa Qiyaas hiki ni Qiyaas bila urari, kwani tofauti kati ya Tamattu’u na kuzuilika ni kubwa sana. Mwenye kufanya Tamattu’u lengo lake la Hajj anakuwa ashalipata baada ya kujivua na Ihraam ya ‘Umrah wakati mwenye kuzuilika hakukidhi lengo lake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

 

Share