07-Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan? (كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن): Kuithibitisha Qur-aan Baada Ya Kuihifadhi
Vipi Uweze Kuhifadhi Qur-aan?
كَيْفَ تَحْفَظُ الْقُرآن؟
07-Kuithibitisha Qur-aan Baada Ya Kuihifadhi
07-Kuithibitisha Qur-aan Baada Ya Kuihifadhi
Kuhifadhi Qur-aan si jambo gumu sana kama kuithibitisha kwake, kwa sababu mtu anaweza kuhifadhi ukurasa mmoja chini ya nusu saa, lakini ikiwa hakuifanyia juhudi kukariri kuisoma hadi ithibitike vyema moyoni, basi hapo hatobakia katika kumbukumbu, na hivyo basi itakuwa ni khasara kubwa kwa kuwa mtu amepoteza juhudi kubwa na muda wingi kwa jambo ambalo mwishowe halikuthibiti lengo lake.
Nasaha zifuatazo zitakusaidia kuithibitisha hifdhw yako In Shaa Allaah:
i-Dumisha kusoma Qur-aan
Inakupasa ndugu uliyeihifadhi Qur-aan uendelee kuisoma Qur-aan kila siku, kila mara bila ya kuiacha. Kila siku uweke muda maalumu uwe khasa kwa ajili ya kuisoma Qur-aan na isiwe chini ya nusu juzuu kila siku! Na ukiweza kuisoma zaidi ndivyo utakavyoweza kuithibitisha zaidi. Ipe ratiba hii kiupambele katika kila siku ya maisha yako. Zingatia kauli zifautazo za Nabiy ﷺ:
Hadiyth ifuatayo Nabiy ﷺ ameapa kupotea kwa Qur-aan pindi mtu asiposhikamana nayo:
عَنْ أَبِي مُوسَى عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((تَعَاهَدُوا هَذَا الْقُرْآنَ فَوَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَهُوَ أَشَدُّ تَفَلُّتًا مِنْ الْإِبِلِ فِي عُقُلِهَا))
Imepokelewa toka kwa Abu Muwsaa (رضي الله عنه) : Amesema Nabiy ﷺ: ((Dumisheni kuisoma Qur-aan. Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad imo Mikononi Mwake, hiyo (Qur-aan) ni wepesi kukimbia kuliko ngamia anavyochopoka katika kamba yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na pia,
عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّمَا مَثَلُ صَاحِبِ الْقُرْآنِ كَمَثَلِ صَاحِبِ الْإِبِلِ الْمُعَقَّلَةِ إِنْ عَاهَدَ عَلَيْهَا أَمْسَكَهَا وَإِنْ أَطْلَقَهَا ذَهَبَتْ))
Imepokelewa toka kwa ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah ﷺ amesema: ((Hakika mfano wa aliyehifadhi Qur-aan ni kama ngamia aliyefungwa, akimfunga atamzuia, na akimuacha ataenda zake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
ii-Kabla Ya Kulala Rudia Aayah Ulizozihifadhi
Imejaribiwa na kuonekana kwamba pindi mtu akirudia alichohifadhi katika Qur-aan kabla ya kulala, inasaidia kuthibitisha hifdhw yake. Bali ni amali bora kabisa kwamba unasoma Qur-aan kabla ya kulala kwani huenda ikawa ndio amali yako ya mwisho pindi umeandikiwa kufariki usingizini ukajaaliwa husnul-khaatimah (mwisho mwema) na hivyo ndivyo itakavyokuwa hali ya kufufuliwa kwako.
iii-Zisome Aayah Ulizozihifadhi katika Swalaah Za Sunnah.
Hii ni njia bora kabisa ya kuthibitisha hifdhw yako. Zitumie kwanza Aayah zilizothibitika vizuri moyoni kwenye Swalaah za Sunnah, kisha pole pole ongezea nyinginezo. Inaruhusiwa kutumia Mswahafu katika Swalaah za Sunnah, kwa hiyo weka Mswahafu katika rafu ndefu inayofikia urefu wa kiasi cha kuweza kuangaza Aayah, usome kwa hifdh lakini pale unapotatizwa na Aayah, upige jicho kuhakikisha au kurekebisha ulichokosea.
iv-Sikiliza Suwrah ulizozihifadhi.
Pia hii ni njia nyingineyo muwafaka kabisa ya kuithibitisha hifdhw ya Qur-aan. Isikilize kila wakati kila mahali, kila unapopata fursa. Sikiliza hata unapokuwa unafanya kazi zako nyinginezo ingawa inalotakiwa ni kuisikiliza kwa umakini. Imesemekana kwamba baadhi ya watu wameweza kuihifadhi Qur-aan kwa kuisikiliza tu.
Kuisikiliza Qur-aan itakusaidia pia kujirekebisha makosa yako na pia utakapomchagua Qaariu mwenye sauti nzuri inayekupendezea, utaweza nawe kuisoma kwa sauti hiyo hiyo.
v-Ifundishe Qur-aan
Kazi hii humsaidia sana mtu kuithibitsha hifdhw yake. Je, kuna kazi bora zaidi ya kujifunza na kufundisha Qur-aan? Amesema Rasuli wa Allaah ﷺ katika Hadiyth ya 'Uthmaan bin 'Affaan (رضي الله عنه) :
((خَيرُكُم مَنْ تعَلَّمَ القُرآنَ وعَلَّمَه))
((Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Qur-aan kisha akaifundisha)) [Al-Bukhaariy]