01-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Miujiza Yake: Ni Mingi Muujiza Mkubwa Kabisa Ni Qur-aan

 

Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

01-Miujiza Yake: Ni Mingi Muujiza Mkubwa Kabisa Ni Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

Miujiza ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika Siyrah yake ni mingi mno kama itakavyobainishwa katika makala zijazo na Muujiza mkubwa kabisa ni Qur-aan ambayo Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) Anasema:

 

 وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ﴿٤١﴾ لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾

Na hakika hicho ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti. Hakitokifikia ubatili mbele yake, na wala nyuma yake; ni uteremsho kutoka kwa Mwenye hikmah wa yote, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Fusw-Swilat: 41 – 42]

 

Na katika Hadiyth amethibitisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ مَا مِنَ الأَنْبِيَاءِ نَبِيٌّ إِلاَّ أُعْطِيَ مَا مِثْلُهُ آمَنَ عَلَيْهِ الْبَشَرُ، وَإِنَّمَا كَانَ الَّذِي أُوتِيتُ وَحْيًا أَوْحَاهُ اللَّهُ إِلَىَّ فَأَرْجُو أَنْ أَكُونَ أَكْثَرَهُمْ تَابِعًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ‏"‏‏.‏

AmesimuliaAbuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna Nabiy katika Manabii ila alipewa miujiza ambayo watu wanaiamini. Kwa hakika nilichopewa mimi ni Wahyi aliouleta Allaah kwangu. Kwa hiyo, ninataraji nitawapiku kwa wingi wa wafuasi Siku ya Qiyaamah.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Bila shaka Qur-aan Tukufu ni muujiza mkubwa kabisa ambao wana-Aadam ulimwenguni wameujua kwani ndio muujiza pekee uliobakia na utaendelea kubakia hadi Siku ya Qiyaamah kwa sababu Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ndiye Nabiy wa mwisho na Risala yake ni Risala ya mwisho na ya kudumu hadi Siku ya Qiyaamah wala hakuna atakayeweza kudai anayo mfano wa Qur-aan, wala hata kuleta Aayah au kidogo tu kulikoni Aayah, Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) Anahakikisha hivyo pindi Anavosema:

 

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨﴾

Sema: Ikiwa watajumuika wana Aadam na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan; hawatoweza kuleta mfano wake na japokuwa watasaidiana wao kwa wao. [Al-Israa: 88]

 

Bali Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) Anatoa changamoto ya mustahili ambayo kuanzia mwanzo wake hadi Siku ya Qiyaamah hakuna atakayeweza kuleta Suwrah moja au zaidi yake; Anasema Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى):

 

وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٣﴾

Na ikiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi leteni Suwrah mfano wake, na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli. [Al-Baqarah: 23]

 

Na pia Anasema Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى):

 

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِّثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿١٣﴾

Je, wanasema Ameitunga (hii Qur-aan)? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Leteni Suwrah kumi mfano wake zilizotungwa, na iteni muwawezao (wakusaidieni) pasina Allaah mkiwa ni wakweli. [Huwd: 13]

 

Na pia Kauli Yake Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى):

 

أَمْ يَقُولُونَ تَقَوَّلَهُ ۚ بَل لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٣﴾ فَلْيَأْتُوا بِحَدِيثٍ مِّثْلِهِ إِن كَانُوا صَادِقِينَ ﴿٣٤﴾

 

Au wanasema ameibuni (Qur-aan)? Bali hawaamini. Basi walete kauli mfano wake wakiwa ni wakweli. [Atw-Twuwr: 33 – 34]

 

 

Kwanini Qur-aan Ni Muujiza Mkubwa:

 

  • Kwanini Qur-aan isiwe ni muujiza mkubwa kabisa ilhali ni maneno ya Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى), Muumba wa mbingu na ardhi na yaliyomo ndani yake?

 

  • Kwanini Qur-aan isiwe muujiza mkubwa ilhali Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) Ameiteremsha Qur-aan kwa mja Wake ambaye hakuwa akijua kusoma wala kuandika; lakini Qur-aan ilithibitika kifuani mwake akafahamu kabisa hukmu zake, tafsiri yake na ufahamu wa ndani wa kila upande, na akawasomea na kuwafundisha Swahaba?

 

  • Kwanini Qur-aan isiwe muujiza ilhali Maneno Yake ni muujiza katika Suwrah zake, Aayah zake, herufi zake, ufasaha wa lugha yake na maneno yake yenye maana pana ambayo hakuna lugha yoyote nyengine inaweza kulingana nayo, mpangilio wake (Qur-aan), hukmu zake za ki-Shariy’ah na za kilimwengu?

 

  • Kwanini Qur-aan isiwe muujiza mkubwa ilhali ina khabari za kale, khabari za ghayb, pia bayana za sayansi za ulimwengu na yaliomo ndani yake na biologia ya viumbe vyote wakiwemo wana-Aadam na kila kiumbe kinachoishi kwa amri Yake Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى).

 

  • Kwanini Qur-aan isiwe muujiza mkubwa ilhali ilikuwa ikiteremshwa kidogokidogo kwa matukio yaliyokuwa yakitokea ikawa Qur-aan inathibitisha matukio hayo kupinga au kuwafikina na tukio au kutoa hukmu kutokana na tukio na mengineyo, hadi kwamba watu wakawa wanakhofia kuteremshwa kwa Aayah pindi wanapofanya au kusema jambo fulani au linapotokea tukio fulani. Na uteremsho wa Qur-aan ulikuwa katika kipindi cha kuanzia Unabii wake (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hadi kufariki kwake.

 

Basi makafiri wangapi wameingia Uislamu kwa kutambua miujiza iliyomo ndani ya Qur-aan na itaendelea Qur-aan kuwashangaza wana-Aadam na kuwabainikia wenye kutaka kuongoka hadi Siku ya Qiyaamah mijuza ya Aayaat za Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) kama Anavyosema Mwenyewe Allaah (عَزَّ وَجَلَّ):

 

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾

Tutawaonyesha Aayaat (ishara, dalili) Zetu katika peo za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba hiyo ni haki! Je, haitoshelezi Rabb wako kuwa Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu? [Fusw-Swilat: 53]

 

 

Miujiza ndani ya Qu-raan pekee inaweza kupindukia maelfu na inahitaji mijalada na mijalada ya Vitabu kuitaja na kuibainisha miujiza hiyo iliyomo ndani ya Muujiza huo mkubwa wa Qur-aan.

 

 

Share