A-Majina Ya Swahaba: Maana, Wasifu Wao Kwa Mukhtasari: Abu Bakr Asw-Swiddiyq
A-Majina Ya Swahaba: Maana, Wasifu Wao Kwa Mukhtasari
Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)
Jina Lake: Abu Bakr Asw-Swiddiyq
(Al-Qurayshiyy)
ابو بكر الصّدّيق
Maana Yake: Abu ni baba na Bakr ni ngamia mchanga (mtoto).
Wasifu Wake:
Jina halisi la Abu Bakr ni ‘Abdullaah ibn Abi Quhaafah.
Abu Bakr alijulikana kama Asw-Swiddiyq (msema kweli). Heshima yake ilikua kubwa sana baina ya ma-Quraysh.
Abu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alikua mtu mwenye elimu kubwa ya kuhifadhi nasaba za makabila na mataifa ya kiarabu.
Abu Bakr aliishi kama mfanya biashara hapo Makkah. Inasemekana kwamba alitoa mali nyingi fiy SabiliLlaah (njia ya Allaah) kuliko yeyote mwengine.
Abu Bakr ni Swahaba wa kwanza aliyebashiriwa Jannah.
Alizaliwa miaka miwili baada ya kuzaliwa Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).
Upendo wa Abu Bakr kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba alikuwa tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya kumlinda na kumfariji Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).
Alikua Swahaba mnyenyekevu na mkarimu ambaye aliaminiwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika kila kitu kwa kiwango ambacho aliitwa As-Swiddiyq na Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).
Utu wake mkubwa na utumishi wake kwa Uislamu na Waislamu ulimpatia upendo na heshima ya Waislamu wote, alichaguliwa na Waislamu wote kama Khalifa wa kwanza baada ya kifo cha Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).
Kufariki Kwake:
Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alifariki akiwa na umri wa miaka 63 mwaka wa 13 wa Hijri.