Hazina Miongoni Mwa Hazina Za Jannah: لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بالله
Hazina Miongoni Mwa Hazina Za Jannah:
لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بالله
Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa Sallam):
Hadiyth Ya Kwanza:
حَدَّثَنَا سُلَيْمَانُ بْنُ حَرْبٍ، حَدَّثَنَا حَمَّادُ بْنُ زَيْدٍ، عَنْ أَيُّوبَ، عَنْ أَبِي عُثْمَانَ، عَنْ أَبِي مُوسَى رضى الله عنه قَالَ كُنَّا مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فِي سَفَرٍ فَكُنَّا إِذَا عَلَوْنَا كَبَّرْنَا فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم " أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ، فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ وَلاَ غَائِبًا، وَلَكِنْ تَدْعُونَ سَمِيعًا بَصِيرًا ". ثُمَّ أَتَى عَلَىَّ وَأَنَا أَقُولُ فِي نَفْسِي لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ. فَقَالَ " يَا عَبْدَ اللَّهِ بْنَ قَيْسٍ قُلْ لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ فَإِنَّهَا. كَنْزٌ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ ". أَوْ قَالَ " أَلاَ أَدُلُّكَ عَلَى كَلِمَةٍ هِيَ كَنْزٌ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ، لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ ".
Amesimulia Abi ‘Uthmaan kuwa Abu Muwsaa Al-Ash‘ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari, nasi tulikuwa tukipanda sehemu yenye mwinuko, tukileta Takbiyr (kusema Allaahu Akbar – Allaah ni Mkubwa kwa sauti kubwa). Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alyahi wa aalihi wa sallam) akasema: “Enyi watu! Jioneeni huruma nafsi zenu, kwani hakika yenu nyinyi hamumuombi kiziwi wala asiyekuwepo, lakini mnamuomba Mwenye kusikia na Mwenye kuona”. Kisha akanijia mimi nilipokuwa nasoma kwa taratibu:
لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ
Laa hawla wa laa quwwata illa biLLaah (Hapana hila wala nguvu ila za Allaah) Akasema: “Ee ‘Abdullaah bin Qays! Sema:
لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ
kwani hiyo ni hazina miongoni mwa hazina za Jannah.”
Au alisema: “Je, sikuelekezi wewe kwa neno ambalo ni hazina miongoni mwa hazina za Jannah? Ni
لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ
[Al-Bukhaariy Kitabu Cha Kuomba Du’aa]
Hadiyth Ya Pili:
حَدَّثَنَا مُوسَى بْنُ إِسْمَاعِيلَ، حَدَّثَنَا عَبْدُ الْوَاحِدِ، عَنْ عَاصِمٍ، عَنْ أَبِي عُثْمَانَ، عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ لَمَّا غَزَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم خَيْبَرَ ـ أَوْ قَالَ لَمَّا تَوَجَّهَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ـ أَشْرَفَ النَّاسُ عَلَى وَادٍ، فَرَفَعُوا أَصْوَاتَهُمْ بِالتَّكْبِيرِ اللَّهُ أَكْبَرُ اللَّهُ أَكْبَرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ، إِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ وَلاَ غَائِبًا، إِنَّكُمْ تَدْعُونَ سَمِيعًا قَرِيبًا وَهْوَ مَعَكُمْ ". وَأَنَا خَلْفَ دَابَّةِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَسَمِعَنِي وَأَنَا أَقُولُ لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ، فَقَالَ لِي " يَا عَبْدَ اللَّهِ بْنَ قَيْسٍ ". قُلْتُ لَبَّيْكَ رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ " أَلاَ أَدُلُّكَ عَلَى كَلِمَةٍ مِنْ كَنْزٍ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ ". قُلْتُ بَلَى يَا رَسُولَ اللَّهِ فِدَاكَ أَبِي وَأُمِّي. قَالَ " لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ ".
Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy (Radhwiya 'anhu) . Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipopigana vita vya Khaybar, au Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoelekea huko na watu waliliona bonde, wakapaza sauti zao kuleta Takbiyr wakisema:
اللَّهُ أَكْبَرُ اللَّهُ أَكْبَرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ
"Allaahu Akbar! Allaahu Akbar!
(Allaah ni Mkubwa)
laa ilaaha illa Allaah (hakuna mwabudiwa wa haki ila Allaah).
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia, "Shusheni sauti zenu, kwani mnayemwita si kiziwi au aliye mbali, bali mnayemwita ni Mwenye kusikia. Ambaye yuko karibu na yuko pamoja nanyi.” Nilikuwa nyuma yake akiendesha mnyama wake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanisikia nikisema:
لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إِلا باللَّهِ
Laa hawla walaa quwwata illa biLLaah
Akaniambia: “Yaa ‘Abdallaah bin Qays!” Nikasema: Labbayak ee Rasuli wa Allaah! Akasema: "Je, nisikujulishe neno katika hazina ya Jannah?” Nikajibu: Ndiyo, Ee Rasuli wa Allaah, Baba yangu na mama wafidiwe kwa ajili yako. Akasema:
لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إِلا باللَّهِ،
"Laa hawla wa la quwwata illa biLLaah." [Al-Bukhaariy Kitabu Cha Maghazi]
Hadiyth Ya 3
حَدَّثَنَا أَبُو كُرَيْبٍ، حَدَّثَنَا أَبُو خَالِدٍ الأَحْمَرُ، عَنْ هِشَامِ بْنِ الْغَازِ، عَنْ مَكْحُولٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، قَالَ قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " أَكْثِرْ مِنْ قَوْلِ لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ فَإِنَّهَا كَنْزٌ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ " .
Amesimulia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kithirisheni kusema
لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ
Laa hawla walaa quwwata illa biLLaah
Kwani hiyo ni hazina katika hazina za Jannah (Peponi). [At-Tirmidhiy]
Tafsiyr Ya:
لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بالله كَنْزٌ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ
Amesema Imaam An-Nawawiy (Rahimahu-Allaah) katika Sharh ya Hadiyth ya kwanza.
لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بالله كَنْزٌ مِنْ كُنُوزِ الْجَنَّةِ
'Ulamaa wanasema: Ni kwa sababu hilo ni neno la kujisalimisha na kumuachia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kukiri Kwake na kujisalimisha Kwake na kukiri kuwa hakuna mtengenezaji au mjengaji zaidi yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kamba hakuna yeyote mwenye uwezo wa kurejesha Analolipanga Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ya kuwa mja hamiliki chochote katika jambo lake.
Ama maana ya hazina hapa ni: Thawabu tele zilizowekwa Jannah (Peponi) nazo ni thawabu zenye thamani kubwa kama vile ambavyo hazina ni mali zenu za thamani zaidi. Watu wa lugha wamesema:
الحول
Al-Hawl ni harakati na hila, Yaani: hakuna uwezo wala hila isipokuwa ni kutokana na uwezo wa Allaah ('Azzaa wa Jaal). Na imesemwa vile vile maana yake
لا حَوْلَ
Yaani: Hatuna uwezo wa kuondosha shari wala nguvu za kupata kheri isipokuwa ni kutoka kwa Allaah ('Azza wa Jaal). Na imesemwa vile vile hatuna uwezo wa kumuasi Allaah ('Azza wa Jaal) isipokuwa kwa msaada Wake wa kutuepusha na maasi. Na hakuna uwezo wa kumtii Yeye isipokuwa ni kwa msaada Wake.
Na hivyo amesema pia Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu). Na wengineo wamekaribiana kufasiri hivyo.
[Sharh Swahiyh Muslim (9/28)]
Kisa Cha Swahabi ‘Awf bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) Na Du’aa Ya Wazazi Wake
Imaam Al-Qurtwuby [Al-Jaami’ Li-Ahkaam Al-Qur-aan (18: 160 – 161] na Wafasiri wa Qur-aan wengineo wamesema kuwa Aayah zifuatazo ziliteremshwa kumhusu ‘Awf bin Maalik Al-Ashja’iyy (Radhwiya Allaahu 'anhu)
مَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا﴿٢﴾ وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani). Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza kusudio Lake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu makadirio. [Atw-Twalaaq: 2 – 3]
Ingawa baadhi ya ‘Ulamaa wamedhoofisha kisa hiki, ila baadhi yao wamekisimulia kwamba 'Awf Ibn Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) mtoto wa Maalik Ibn Abu ‘Awf Al-Ashjaa’iy alitekwa na majeshi ya maadui kipindi cha Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Khabari hii ilipowafikia wazazi wa 'Awf, walisikitishwa sana kiasi kwamba mama wa 'Awf alihuzunika na kula mno, kiasi cha kukaribia kukata tamaa. Wakati huo, Maalik (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alienda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: "Mwanangu ametekwa na mama yake amepata kiwewe, je unaniamrisha nini? Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Mche Allaah na vuteni subra na amrisha ahli wako wakithirishe kusema.
لا حول ولا قوة إلا بالله
"Laa hawla walaa quwwata illa bi-LLaahi"
Akarudi nyumbani kwake akamwambia mkewe: Hakika Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) menimarisha pamoja nawewe tukithirishe kauli ya ya
لا حول ولا قوة إلا بالله
"Laa hawla walaa quwwata illa bi-LLaahi"
(Mama yake ‘Awf) akasema: “Uzuri ulioje kwa aliyotuamirisha.” Wakawa wanaitamka kauli hiyo ya
لا حول ولا قوة إلا بالله
"Laa hawla walaa quwwata illa bi-LLaahi"
Basi kwa du’aa hiyo ya mara kwa mara Allaah ('Azza wa Jaal) Akajaalia minyororo ya ‘Awf kuvunjika gerezani na maadui zake wakaghafilika naye, hapo 'Awf aliweza kuwatoroka maadui akarudi kwa wazazi wake pamoja na kujaaliwa kupata mali ya Wanyama aliowapata akiwa njiani.
Mafunzo Na Mwongozo:
Nasaha Kwa Wazazi Na Watoto Wa Kiislaam! Tambueni Kudura Na Adhama Ya Du’aa Ya Wazazi!
Nasaha kwa Wazazi wapendelee kuwaombea Watoto wao du’aa nzuri na wajiepushe kuwaombea du’aa mbaya khasa wanapokuwa wameghadhibika kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha hivyo katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لاَ تَدْعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ ولاَ تَدْعُوا عَلَى أَولاَدِكُمْ))
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msijiombee dhidi ya nafsi zenu wala msiombe dhidi ya watoto wenu.)) [Muslim (3009), Abuu Daawuwd, taz. Swahiyh Abiy Daawuwd (1532) na Swahiyh Al-Jaami’ (7267)]
Na pia Hadiyth ifuatayo inathibitisha kuwa du’aa ya mzazi hutaqabaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
عّنْ أَنسْ بِنْ ماَلِكْ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ): ((ثَلاَثُ دَعْواتِ لاَ تُرَدُّ: دَعْوَةُ الْوَالِدِ لِوَلَدِهِ، وَدَعْوَةُ الصَّائِم، وَدَعْوَةُ الْمُسَافَرَ))
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): ((Du’aa za watatu hazirudishwi; du’aa ya mzazi kwa mwanawe, na du’aa ya mwenye kufunga Swawm, na du’aa ya msafiri.))[Al-Bayhaqiy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3032) na katika Asw-Swahiyhah (1797)]