07-Rajab: Mafunzo Katika Miezi Ya Hijri: Ya Kutekeleza Na Ya Kujiepusha
07-Rajab
Mafunzo Katika Miezi Ya Hijri: Ya Kutekeleza Na Ya Kujiepusha
'Amali Za Kutenda Na Mambo Ya Kujiepusha Nayo Katika Miezi Mitukufu
'Amali Za Kutenda Na Mambo Ya Kujiepusha Nayo Katika Miezi Mitukufu
AlhamduliLLaah. Inapasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kutujaalia uhai hadi kutufikisha katika mwezi mwengine mtukufu. Ni fursa nyingine ya kutenda mema tuchume thawabu nyingi. Mema ambayo hatuna budi kuyatenda kwa ajili ya kujenga Aakhirah yetu kabla haijafika siku ya kuaga kwetu dunia.
Utukufu wa miezi hiyo mitukufu imetajwa katika Qur-aan na Sunnah: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ﴿٣٦﴾
Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukmu ya makadirio ya Allaah, (tangu) siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo, (iko miezi) minne mitukufu. Hivyo ndiyo Dini iliyo nyoofu. Basi msijidhulumu humo nafsi zenu (kwa kufanya maasi), na piganeni vita na washirikina wote kama wao wanavyokupigeni vita nyote. Na jueni kwamba Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa. [At-Tawbah: 36]
Na miezi hiyo minne mitukufu imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أبي بَكْرَةَ رضي الله عنه عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أنه قَالَ: ((إن الزَّمَانَ قَدْ اسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْمَ خَلَقَ اللَّهُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضَ السَّنَةُ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ثَلاثٌ مُتَوَالِيَاتٌ ذُو الْقَعْدَةِ وَذُو الْحِجَّةِ وَالْمُحَرَّمُ وَرَجَبُ مُضَرَ الَّذِي بَيْنَ جُمَادَى وَشَعْبَانَ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mgawano wa zama umerudi katika hali yake ya asili siku Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili; minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram, mwengine ni Rajab wa (kabila la) Mudhwarr ambao uko baina ya Jumaadaa na Sha'baan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Imaam Atw-Twabariy amesema: “Katika miezi yote kumi na mbili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameichagua hii minne na Ameifanya kuwa ni mitukufu na kusisitiza kuitakasa, na kwamba dhambi zitakazofanyika humo ni zaidi na hali kadhalika thawabu za ‘amali njema zinakuwa maradufu na zaidi. [Atw-Twabariy 14: 238]
Qataadah amesema kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):