02-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kutaqabaliwa 'Amali
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
02-Kutaqabaliwa ‘Amali
"رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ"
“Rabbi wetu Tutakabalie, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa Yote”. [Al-Baqarah: 127)]
Haya ni maombi ya kwanza kati ya maombi ya Imamu wa waliojiengua na shirki na kushikamana na tawhiyd, kiigizo cha wenye kumpwekesha Allaah na Khaliyl wa Ar Rahmaan Nabii Ibraahiym ‘Alayhis Salaam ambaye Allaah Ta’aalaa Amemsifu kwamba ni mwenye kukusanya mambo yote ya kheri Aliposema:
"إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِلَّهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ"
“Hakika Ibraahiym alikuwa mwenye akhlaaq na maadili yote mema, mtiifu kwa Allaah, aliyeelemea haki, na hakuwa miongoni mwa washirikina”. [An Nahl (120)].
Du’aa hii ya kuomba kukubaliwa ‘amali za vitendo na maneno, ni du’aa muhimu kabisa kwetu. Angalia Nabii huyu Baba wa Manabii akiwa katika kazi ya ujenzi huu muhimu wa Al-Ka’abah ambayo ndiyo Qiblah cha Waumini wanachokielekea katika Swalaah zao zote, akiwa pamoja na mwanaye Ismaa’iyl ‘Alayhis Salaam, anavyomwomba Allaah Awataqabalie kazi yao hii pamoja na cheo chake kikubwa alichonacho mbele ya Allaah. Basi vipi mimi na wewe?
Hebu litaamuli jambo lao hili. Wanaifanya kazi hii waliyopewa na Mola wao huku wakimwomba: “Ee Rabbi wetu! Tutakabalie”. Angalia vipi ilikuwa hali yao ya khofu ya kutokukubaliwa ‘amali yao hiyo!
Msingi muhimu wa kukubaliwa mtu ‘amali yake ni ikhlasi pamoja na kumwomba Allaah Amtakabalie.
Hali hii ya Nabiy Ibraahiym ‘Alayhis Salaam na mwanaye Ismaa’iyl ni kama hali ya Waumini wenye kumtakasia Allaah Aliowaelezea katika Kauli Yake:
"وَالَّذينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ"
“Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zina khofu kwamba hakika watarejea kwa Rabbi wao”. [Al-Muuminuuna (23:60)]
Yaani wanatoa swadaqah, matumizi ya familia zao na mengineyo ya kheri huku wakiwa na khofu ya kutokubaliwa hayo. Bibi ‘Aaishah alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Aayah hii akisema:
"أَهُمْ الَّذِينَ يَشْرَبُونَ الْخَمْرَ وَيَسْرِقُونَ؟ قَالَ: لَا يَا بِنْتَ الصِّدِّيقِ، وَلَكِنَّهُمْ الَّذِينَ يَصُومُونَ، وَيُصَلُّونَ، وَيَتَصَدَّقُونَ، وَهُمْ يَخَافُونَ أَنْ لَا يُقْبَلَ مِنْهُمْ"
“Je hawa ni wale wanaokunywa ulevi na wanaoiba? Akasema: Hapana ee binti As Swiddiyq. Lakini hawa ni wale wanaofunga, wanaoswali na wanaotoa swadaqah nailhali wao wanaogopa wasikubaliwe (‘amali zao hizo)”. [Sunanu At-Tirmidhiy: Kitaabu Tafsiyril Qur-aan ‘An Rasuwlil Laah]
Kutokana na du’aa hii tunajifunza haya yafuatayo:
1- Umuhimu wa kukubaliwa ‘amali pale ambapo mhimili wa ‘amali njema unasimamia juu yake. Na hii ni pamoja na kumtakasia Allaah na kufuata yale yote Aliyokuja nayo Rasuli.
2- Aayah inatufundisha kwamba tunatakiwa tushikamane na kumwomba Allaah nyakati zote Atutakabalie ‘amali zetu baada ya kuzifanya. Na hili ndilo alilokuwa akilifanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akistaghfiri mara tatu baada ya kila Swalaah. Na alikuwa anasema baada ya Swalaah ya Alfajiri:
"اللّهمَّ إنّي أسألك علماً نافعاً، ورزقاً طيباً، وعملاً مُتقبّلاً"
“Ee Allaah! Hakika mimi ninakuomba ‘ilmu nufaishi, riziki safi ya halali, na ‘amali yenye kutaqabaliwa”. [Imesimuliwa na Ummu Salamah]
Na alikuwa anajilinda kwa kusema:
"اللّهمّ إنّي أعوذ بك من علم لا ينفع، ومن عمل لا يُرفع"
“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na ‘ilmu isiyonufaishi, na ‘amali isiyopandishwa”. [Imesimuliwa na Anas bin Maalik]
3- Kutawassali kwa Allaah kwa kutumia Majina Yake na Sifa Zake kwa mujibu wa ombi. Jina la السميع linanasibiana na Allaah kuwa Anaisikia du’aa yao, na العليم linanasibiana na kuwa Allaah Anazijua niya zao, na ukweli wa unyenyekevu wao.
4- Du’aa ni makimbilio ya Manabii na Mitume wote. Mja anaihitajia katika hali zake zote za kisharia na kidunia.
5- Du’aa inaondosha sifa ya mtu kujiona, kwani kujiona kunaharibu ‘amali ya mtu.