07-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Maghfirah, Kuimarishwa Na Ushindi Dhidi Ya Makafiri

                            

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

                  

07-Maghfirah, Kuimarishwa Miguu Na Ushindi Dhidi Ya Makafiri                  

                  

 

 

"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ "

 

“Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na upindukaji wetu mipaka katika mambo yetu, na Ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri”.  [Aal ‘Imraan: (147)].

 

Du’aa hii adhimu Waumini walikuwa wakiiomba katika uwanja wa vita kabla ya kukabiliana na adui au wakati vita vinapopamba moto.  Na Allaah Ametueleza hili ili tuigize kitendo chao hicho pamoja na du’aa hii wakati tunapokabiliana na makafiri au wakati tunapopitiwa na misukosuko migumu. Vita vya kupigania Uislamu (Jihaad) –hata kabla ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake Al Kiraam- vilifanywa na Manabii wengi mno wakiwa na wafuasi wao Waislamu wakipambana kwa pamoja na makafiri ili kulinyanyua juu kabisa Neno la Allaah la Tawhiyd na Dini Yake.  Allaah Anatuambia:

 

"وَكَأَيِّنْ مِنْ نَبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّه وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا وَاللَّهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ"

 

Na Manabii wangapi walipigana vita wakiwa pamoja nao Waumini wengi waliojaa Imani ya kikweli, basi hawakulegea kwa yaliyowasibu katika Njia ya Allaah, wala hawakudhoofika na wala hawakunyong’onyea. Na Allaah Anapenda wanaosubiri”.  [Aal ‘Imraan: (146)]

 

Hawakunyong’onyea, hawakukata tamaa wala hawakuvunjika moyo hata kama matokeo ya vita hayakuwa mazuri, bali walirudi, wakajipanga upya, wakajiimarisha tena na kuwa tayari kwa raundi zijazo.  Na hii yote ni kutokana na ungangari wao na nguvu ya iymaan yao.  Na wakati huo mgumu wa kuumana vita, hawakuwa na jingine la kuomba isipokuwa kusema:

 

"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ "

 

“Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na upindukaji wetu mipaka katika mambo yetu, na Ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri”.  [Aal ‘Imraan: (147)].

 

Walijiongezea wenyewe ombi hili pamoja na inavyoonesha kwamba wao ni wawajibikaji wazuri wa Maamrisho ya Allaah na katika kuipigania Dini Yake kwa ajili ya kujinyenyekeza na kujikusurisha kwa Allaah.  Na huu ndio ukamilifu wa utumwa kwa Allaah Rabbi wa walimwengu.

 

Walijua kwa yakini kwamba madhambi na kupetuka Mipaka ya Allaah ni katika sababu kubwa za kufeli na kushindwa, na kwamba kuepukana na madhambi ni moja kati ya sababu za ushindi dhidi ya maadui au kupata mafanikio yoyote ya kidunia au ya kiaakhirah.  Hapo ndipo walipomwomba Mola wao Awaghufurie madhambi yao yote.  Na hizi ndizo sifa za Waumini wachaji.  Wao daima wanakuwa katika hali ya kati ya matarajio na khofu hata pale wanapokuwa kwenye misukosuko mikubwa.

Kadhalika, walimwomba Allaah Aithibitishe miguu yao, yaani Azitie nguvu nyoyo zao ili miguu iweze kusimama imara.  Nyoyo zikilegea, basi miguu haiwezi kusimama.  Muislamu anamhitajia Allaah Amthibitishe moyo wake katika hali tatu:

 

1-  Amthibitishe wakati wa kupambana na maadui.  Kama Hakumthibitisha, basi atakimbia vita.  Na kukimbia vita ni katika makosa makubwa sana kwa Muislamu.

 

2-  Amthibitishe kwenye mambo ya shubha.  Kama Hakumthibitisha basi atapotea.

 

3-  Amthibitishe mbele ya matamanio ya nafsi. Asipomthibitisha basi ataangamia.

 

 

Na kwa vile wapiganaji hawa wakiwa na Manabii wao walikusanya matano wakati wa hali hizo ngumu; subra, kutonyong’onyea na kutokata tamaa, kuomba maghfirah, kuomba du’aa kwa adabu na unyenyekevu na kuomba nusura toka Kwake tu Allaah, Allaah Aliwajibu hapo hapo.  Allaah Anasema: 

 

"فَآتَاهُمُ اللَّهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الْآخِرَةِ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ"

 

Basi Allaah Akawalipa malipo ya dunia na thawabu nzuri za Aakhirah. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan”.  [Aal ‘Imraan: (148)]

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-   Muislamu anatakiwa amwombe Allaah kwa du’aa hii na hususan wakati wa kupambana na makafiri.  Si katika vita tu, bali katika pambano lolote la kuitetea  na kuipigania dini.  Ni kama kwenye midahalo au katika kuwanusuru Waislamu wanaonyanyaswa kwa ajili ya dini yao.

 

2-  Mwanadamu anamhitajia Allaah katika hali zake zote.

 

3-  Mwanadamu hakosi kuvuka mipaka juu ya nafsi yake; ima kwa kuzidisha yasiyotakiwa, au katika kukusuru kwa kufanya jambo chini ya kiwango chake kinachotakiwa.  Hivyo anatakiwa akithirishe du’aa hii kwa kuwa inanasibiana na hali yake.

 

 

4-  Kutanua du’aa ni vizuri zaidi kuliko kuifupisha.  Lau wao wangelisema: “Tughufirie” basi ingelitosha.  Lakini wametanua zaidi du’aa yao wakiomba Awaghufirie madhambi yao madogo madogo, na kuvuka kwao mipaka kwa kutenda madhambi makubwa.  Na kila mtu anavyozidi kutanua wigo wa du’aa yake na kuirefusha, basi anazidi kudhihirisha utumwa wake kwa Allaah.  Na huu ndio ukomo wa unyenyekevu kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

5-  Madhambi ndio sababu kuu ya udhaifu na kukosa Msaada wa Allaah.  Na kwa ajili hiyo, walimwomba Allaah Awafutie madhambi yao ili mlango wa Msaada Wake ufunguke kwao waweze kuwashinda maadui zao makafiri.

 

 

6-  Du’aa ni katika sababu kuu za mtu kupata muradi wake na kuondoshewa adha. Baada ya kuomba, Allaah Akawatimizia pale Anaposema:  Basi Allaah Akawalipa malipo ya dunia na thawabu nzuri za Aakhirah”.

 

 

7-  Muislamu anatakiwa asitegemee tu nyenzo alizonazo, bali amtegemee Muumba wake na Mpatishaji wake.  Waumini hao pamoja na wingi wao, hawakuangalia wingi huo kama ndio mwega, bali walitegemeza kusimama kwao imara mbele ya adui na kushinda kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

 

Share