33-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Njia Iliyo Sawa

 

 Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

33- Njia Iliyo Sawa

 

"عَسَى رَبِّي أَن يَهْدِيَنِي سَوَاءَ السَّبِيلِ"

 

Asaa Rabb wangu Akaniongoza njia iliyo sawa”.  [Al-Qaswas: (22)].

 

Hii ni du’aa nyingine ya barakah ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) ndani ya Qur-aan Tukufu.  Ni du’aa iliyo katika muundo wa sentensi taarifu.

 

Alipomuua Mkoptik bila kukusudia kwa kumpiga konde, alipambaukiwa kuwa mwenye khofu katika mji ule huku anaangaza kwa tahadhari.  Akaja mtu kutoka mwisho wa mji ule akiwa anakimbia, akamhabarisha kuwa wakuu wanashauriana kumuua, kwa hiyo atoke haraka, na asidharau ushauri wake huo.

 

Muwsaa bila kusita akatoka mjini hapo kuelekea Madyana.  Alitoka bila maandalizi yoyote ya safari.  Hana masurufu, hana kipando, hana viatu na hata huko anakoelekea hamjui yeyote.  Akiwa katika hali hii ngumu ya ghafla iliyochanganyika na khofu ya kuuawa, hapo alielekea kwa Mola wake na kumwomba du’aa hii akisema:  Asaa Rabb wangu Akaniongoza njia iliyo sawa”.

 

Yaani njia iliyonyooka na fupi ya kumfikisha kwa urahisi aendako.  Na hapo Allaah ‘Azza wa Jalla Akamwongoza njia hiyo, na Akamwongoza katika njia iliyonyooka duniani na aakhirah.  Akafika aendako, akapata ukaribisho wa heshima na akaozeshwa.  Halafu akapata Utume, na kurudi tena kwa Fir-a’wn akiwa na miujiza.  Na yeye akawa ndio sababu ya Fir’awn kuangamia pamoja na jeshi lake.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Katika aayah hii, kuna maelekezo na mafundisho kuwa Muislamu anatakiwa atoe juhudi zake za mwisho za kutumia nyenzo alizonazo, kisha aelekee kwa Allaah kumwomba Amwepesishie kufikia lengo lake kupitia nyenzo hizo.  Huu ndio ukamilifu wa kutawakkal.

 

 

2-  Muislamu anatakiwa amwombe Mola wake ‘Azaa wa Jalla hidaayah ya kihisia na kidhahania mpaka Allaah Amwongoze kwenye njia nyepesi na karibu zaidi itakayomfikisha kwenye kusudio lake katika dini yake na dunia yake.

 

 

3-  Viumbe vyote vinamhitajia Allaah Ta’aalaa kuvihidi na kuviwezesha.

 

 

4-  Ubora wa du’aa katika kuvuta manufaa na kuondosha madhara.

                                                             

Share