36-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Maghfirah Kwa Waumini Waliotangulia

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

36- Maghfirah Kwa Waumini Waliotangulia

 

 

"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ"

 

Rabb wetu!  Tughufurie pamoja na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan, na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini.  Rabb wetu!  Hakika Wewe Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu”.  [Al-Hashr: (10)].

 

 

Du’aa hii ina umuhimu mkubwa mno.  Allaah Ta’aalaa Ameitaja kwa watu wa iymaan safi baada ya Maswahaba (Allaah Awaridhie wote) kati ya Taabi’iyna na waliowafuatia kwa wema hadi Siku ya Qiyaamah.  Ni du’aa inayoonyesha mapenzi ya kweli na udugu uliojikita ndani ya nyoyo za Waislamu.  Kwani haki za Muislamu juu ya nduguye Muislamu ni nyingi.  Kati ya haki hizo ni kumwombea nduguye kwa siri katika uhai wake na baada ya kufa kwake. Udugu wa dini ndio udugu uliotukuka zaidi na wenye faida za kudumu zaidi kuliko udugu wa damu.  Udugu wa kidini ni wa kufaana duniani na aakhirah, lakini wa damu unaweza usiwe na faida yoyote; si duniani wala aakhirah.

 

Al-‘Allaamah bin Sa’adiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Du’aa hii inawajumuisha Waumini wote waliotangulia kati ya Maswahaba, waliopita kabla yao na watakaokuja baada yao.  Na hii ni katika fadhwaail za iymaan kwamba Waumini wananufaishana wao kwa wao, na wanaombeana wao kwa wao kwa kuwa iymaan yao ni moja.  Iymaan hii imewafunga wote ndani ya duara la udugu ambao moja kati ya matawi yake ni kuombeana wao kwa wao na kupendana wao kwa wao. Na kwa ajili hiyo,  Allaah Ta’aalaa Ametaja katika du’aa hii mafundo ya chuki ambayo kama yataondoka, kinyume chake huthibiti, nayo ni mapenzi ya kweli kati ya Waumini”.

 

Hivyo wamekusanya ndani ya du’aa hii ya barakah kati ya usalama wa moyo na usalama wa ndimi zao.  Hakuna ndani ya nyoyo zao chuki yoyote, hikdi yoyote wala kumtaja yeyote kwa ubaya.  Na hili ndilo jumuiko la mapenzi ya kweli kati ya Waumini kwa ajili ya Rabbi wa walimwengu.

 

Abu Mudhwaffar As-Sam’aaniy (Rahimahul Laah) amesema:  “Katika aayah, kuna dalili kwamba kuwaombea rahmah waliotangulia, kuwaombea kheri na kuacha kuwataja kwa ubaya, ni alama ya Waumini wa kweli”.

 

Na Waislamu wenye sifa hii ya kupendana, kuombeana na kuwataja kwa wema ndugu zao, Allaah Atawalipa malipo mema kabisa.  Allaah Anatuambia:

 

"وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ ۖ وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَـٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ"

 

“Na Tutaondosha mizizi ya mafundo ya kinyongo yaliyomo vifuani mwao,  itapita chini yao mito.  Na watasema:  AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ametuongoza kwa haya, na tusingelikuwa  wenye kuhidika kama Allaah Asingetuongoza”.  [Al-A’raaf: (43)].

 

Haifichikani ee ndugu yangu Muislamu kwamba kuna kheri nyingi za dunia na aakhirah katika kukithirisha du’aa hii.  Kwanza, kufanya hivyo ni kuitikia Agizo la Allaah Ta’aalaa.  Pili, kuna thawabu nyingi anazozipata mwombaji.  Tatu, du’aa hii hukuza mapenzi kwa nduguze Waislamu ndani ya moyo wake.  Nne, humweka mbali na chuki, hasadi, mafundo na kinyongo.  Na kwa hivyo, nyoyo husafika, na hii ni moja kati ya makusudio makubwa ya dini.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Ni kuwa du’aa hii ina umuhimu mkubwa sana kwa Muislamu ambaye anatakiwa aikithirishe mchana na usiku, kwani matunda na manufaa yake hayakokoteki duniani na aakhirah.

 

 

2-  Kati ya haki kubwa za Muislamu kwa nduguye Muislamu, ni kumwombea du’aa.

 

 

3-  Kuna umuhimu mkubwa wa kumwomba Allaah Ta’aalaa maghfirah.  Kati ya matunda makubwa ya maghfirah ni kuondoka mabaya, kupatikana kheri, na kufuzu Jannah.

 

 

4-  Muislamu asisahau fadhla za waliomtangulia katika iymaan.  Awataje kwa wema na awaombee.

 

 

5-  Du’aa hii imekusanya tawassuli mbili muhimu ambazo ni:

 

 

(a)  Kutawassal kwa Umola wa Allaah (Rubuwbiyyah) waliposema:  “Rabbi wetu”, na kwa Majina Yake Mawili Matukufu;  “Rauwf” na “Rahiym”.

 

 

(b)  Kutawassal kwa neema Aliyowapa ya iymaan wao na waliowatangulia.

 

 

Share