017-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Vilivyoharamishwa Ni Halali Wakati Wa Dharura

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

017-Vilivyoharamishwa Ni Halali Wakati Wa Dharura

 

 

 

·        Vilivyoharamishwa Ni Halali Wakati Wa Dharura

 

Waislamu wote kwa pamoja wanakubaliana kuwa inafaa kula mfu na mfano wake kwa yeyote aliyelazimika.  Allaah ‘Azza wa Jalla Amepataja mahala patano ndani ya Qur-aan Tukufu ambapo mwenye kulazimika anaweza kula vilivyoharamishwa.

 

1-  Allaah Amesema - baada ya kutaja kuharamisha maiti na mfano wake -:

 

"فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"

 

“Lakini aliyefikwa na dharura (akala) bila ya kutamani wala kupindukia mipaka, basi si dhambi juu yake.  Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.  [Al-Baqarah: 173].

 

2-  Amesema tena  - baada ya kutaja kuharamisha maiti na mfano wake -:

 

"فَمَنِ اضْطُرَّ فِي مَخْمَصَةٍ غَيْرَ مُتَجَانِفٍ لِّإِثْمٍ ۙ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"

 

“Basi atakayelazimika katika njaa kali bila kulalia kwenye dhambi (akala vilivyoharamishwa), basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [Al-Maaidah: 03].

 

3-  Na Akasema tena - baada ya kuvitaja -:

 

"فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ رَبَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"

 

“Lakini atakayefikwa na dharura bila ya kutamani wala kuvuka mipaka, basi hakika Rabb wako Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [Al-An’aam: 145].

 

4-  Amesema pia:

 

"وَمَا لَكُمْ أَلَّا تَأْكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَقَدْ فَصَّلَ لَكُم مَّا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ"

 

“Na mna nini hata msile katika ambavyo limetajwa Jina la Allaah na ilhali Ameshafasilisha waziwazi kwenu yale Aliyokuharamishieni isipokuwa vile mlivyofikwa na dharura navyo”.  [Al-An’aam: 119].

 

5-  Amesema vile vile:

 

"فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"

 

“Basi atakayefikwa na dharura bila ya kutamani wala kuvuka mipaka, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [An-Nahl: 115].

 

 

·        Mpaka Wa Dharura Unaoruhusu Kilichoharamishwa

 

Maana ya dharura katika Aayah hizi Tukufu, na mpaka wa dharura wenye kuruhusu kula mfu na vingine vilivyoharamishwa, ni hofu ya kuhiliki. [Ahkaamul Qur-aan cha Al-Jas-Swaasw (1/150) na Adh-waaul Bayaan (1/64-95)].

 

·        Makusudio Ya Kuhalalisha (Kuruhusu) Kilichoharamishwa

 

Mafuqahaa wamekhitalifiana kuhusiana na makusudio ya kuhalalisha mfu na mfano wake katika kauli mbili:

 

Ya Kwanza:

 

Makusudio ni kuwa inajuzu kula au kutokula. Ni kauli ya baadhi ya Wamaalik, Mashaafi-‘iy, na Mahanbali.  Ni kwa uwazi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ"

 

“Basi si dhambi juu yake”.  [Al-Baqarah: 173].

 

Ya Pili:

 

Makusudio ni kuwa ni waajib kula kwa aliyekurubia kufa.  Ni madhehebu ya Jumhuwr kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ"

 

“Wala msijitupe katika maangamizi kwa mikono yenu”.  [Al-Baqarah: 195].

 

Wamesema:  Na hakuna shaka kuwa yule anayewacha kula mfu na mfano wake mpaka akafa, basi huyo anazingatiwa kuwa amejiua na amejitupa mwenyewe kwenye maangamizi.  Kwa kuwa kujizuia kula ni kitendo kinachonasibishwa kwa mtu mwenyewe.

 

Ama Neno Lake Ta’aalaa فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ, hili halipingani na kauli ya kusema ni waajib, kwa kuwa kukanusha dhambi kwa kula ni suala jumuishi, linakusanya hali ya kujuzu na hali ya ulazima.

 

·        Masharti Ya Kuruhusika Kula Mfu Kwa Aliyedharurika

 

Fuqahaa wameweka masharti ya mtu kuruhusika kula mfu au mfano wake katika vilivyoharamishwa.  Wamekubaliana katika baadhi ya masharti na wamekhitalifiana katika baadhi nyingine.  Kati ya waliyokubaliana kwayo ni:

 

1-  Asipate kabisa chakula cha halali japo tonge moja.  Kama atalipata, basi ni lazima alile kwanza, na kama halikumtosha, hapo basi kilichoharamishwa kitahalalika kwake.

 

2-  Asiwe amekurubia kufa kwa hali ambayo hata akila chakula hakitomfaa tena. Ikiwa ataishilia katika hali hii, basi hapo kilichoharamishwa hakitohalalika tena kwake.

 

3-  Asipate chakula cha halali cha Muislamu au Dhimmiy.  Kuna ufafanuzi wa Fuqahaa kuhusiana na sharti hii.

 

·        Zindushi Mbili:

 

1- Hairuhusiwi kuvuka kiasi cha kuokoa maisha yake au kumwondoshea madhara.  Hili ndilo Aliloliashiria Allaah ‘Azza wa Jalla:  غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ  (Bila ya kutamani wala kuvuka mipaka).

 

2-  Kilichoharamishwa kwa kuwa kinamuua mwanadamu kama sumu, hicho hakiruhusiwi kwa aliyedharurika, kwa kuwa kukila ni kuharakisha mauti na kuiua nafsi, na hili ni katika madhambi makubwa, nalo limekubaliwa na wote.

 

 

 

Share