07-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Fadhila za Kuwa Mpole katika Kuuza, Kununua, Kuchukua, Kutoa, Ubora wa Kulipa, Kudai kwa Njia Nzuri na Kukatazwa Kupunja katika Kupima na Ubora wa Kuwapatia Afueni Mwenye Usiri na Kumsamehe Deni

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب فضل السماحة في البيع والشراء

والأخذ والعطاء وحسن القضاء والتقاضي وإرجاح المكيال والميزان

والنهي عن التطفيف وفضل إنظار الموسِر المُعْسِرَ والوضع عَنْهُ

07-Mlango Wa Fadhila za Kuwa Mpole katika Kuuza, Kununua, Kuchukua, Kutoa, Ubora wa Kulipa, Kudai kwa Njia Nzuri na Kukatazwa Kupunja katika Kupima na Ubora wa Kuwapatia Afueni Mwenye Usiri na Kumsamehe Deni

 

 

Alhidaaya.com

 

قال الله تَعَالَى :

وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٢١٥﴾

Na lolote mlifanyalo katika kheri basi hakika Allaah kwa hilo Ni Mjuzi. [Al-Baqarah: 215]

 

وَيَا قَوْمِ أَوْفُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ ﴿٨٥﴾

Na enyi kaumu yangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu, na wala msipunje watu vitu vyao [Huwd: 85]

 

وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

Ole kwa wanaopunja.

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾

Ambao wanapopokea kipimo kwa watu wanataka wapimiwe kamilifu.

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

Na wanapowapimia (watu) kwa kipimo au wanawapimia kwa mizani wanapunja.

أَلَا يَظُنُّ أُولَـٰئِكَ أَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ ﴿٤﴾

Je, hawadhanii kwamba wao watafufuliwa?

لِيَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥﴾

Kwenye Siku adhimu.

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾

Siku watakayosimama watu kwa Rabb wa walimwengu. [Al-Mutwaffifiyn: 1-6]

 

Hadiyth – 1

وعن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه : أنَّ رَجُلاً أَتَى النَّبيَّ صلى الله عليه وسلم يَتَقَاضَاهُ فَأغْلَظَ لَهُ ، فَهَمَّ بِهِ أصْحَابُهُ ، فَقَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( دَعُوهُ ، فَإنَّ لِصَاحِبِ الحَقِّ مَقَالاً )) ثُمَّ قَالَ : (( أعْطُوهُ سِنّاً مِثْلَ سِنِّهِ )) قالوا : يَا رسولَ اللهِ ، لا نَجِدُ إِلاَّ أمْثَلَ مِنْ سِنِّهِ ، قَالَ : (( أعْطُوهُ ، فإنَّ خَيْرَكُمْ أحْسَنُكُمْ قَضَاءً )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kutaka deni lake kwa ukali. Swahaba wakataka kumshika, hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: "Muacheni kwani mwenye haki yake ana ruhusa ya kuzungumza kwa ukali." Kisha akasema: "Mpatieni ngamia kama ngamia wake aliyemtoa (kama mkopo)." Wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Hakuna mfano wa kama wake isipokuwa walio bora kuliko wake." Akasema: "Mpatieni (huyo aliyebora), kwani mbora miongoni mwenu ni yule mzuri wenu zaidi katika kulipa." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth – 2

وعن جابر رضي اللهُ عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( رَحِمَ اللهُ رَجُلاً سَمْحاً إِذَا بَاعَ ، وَإِذَا اشْتَرَى ، وَإِذَا اقْتَضَى )) رواه البخاري .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Allaah amrehemu mja aliye sahali katika kuuza, na anaponunua na anapodai (anapotaka) haki yake." [Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth – 3

وعن أَبي قتادة رضي اللهُ عنه قَالَ : سَمِعْتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم يقول : (( مَنْ سَرَّهُ أنْ يُنَجِّيَهُ اللهُ مِنْ كُرَبِ يَوْمِ القِيَامَةِ، فَلْيُنَفِّسْ عَنْ مُعْسِرٍ أَوْ يَضَعْ عَنْهُ )) رواه مسلم.

Amesema Abu Qaatadah (Radhwiya Allaahu 'anhu): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Mwenye kutaka Allaah amuondoshee (au amlinde) kwa shida za Siku ya Qiyaamah, ampatie muda mdeni wake aliye katika hali ngumu au amsamehe deni lake." [Muslim] 

 

Hadiyth – 4

وعن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه : أنَّ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( كَانَ رَجُلٌ يُدَايِنُ النَّاسَ، وَكَانَ يَقُولُ لِفَتَاهُ: إِذَا أَتَيْتَ مُعْسِراً فَتَجَاوَزْ عَنْهُ ، لَعَلَّ اللهَ أنْ يَتَجَاوَزَ عَنَّا ، فَلَقِيَ اللهَ فَتَجَاوَزَ عَنْهُ )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraoyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kulikuwa na mtu aliyekuwa na mahusiano ya kifedha  na watu, nayo alikuwa akimwambia kijana (mtumishi) wake: "Unapokwenda kwa mtu mwenye dhiki, msamehe, huenda Allaah naye Atakusamehe." Alipokutana na Allaah baada ya kufariki kwake, Allaah Alimsamehe madhambi yake yote." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي مسعود البدريِّ رضي اللهُ عنه قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( حُوسِبَ رَجُلٌ مِمَّنْ كَانَ قَبْلَكُمْ ، فَلَمْ يُوجَدْ لَهُ مِنَ الخَيْرِ شَيْءٌ ، إِلاَّ أنَّهُ كَانَ يُخَالِطُ النَّاسَ وَكَانَ مُوسِراً ، وَكَانَ يَأمُرُ غِلْمَانَهُ أنْ يَتَجَاوَزُوا عَن المُعْسِر . قَالَ اللهُ عزوجل : نَحْنُ أَحَقُّ بذلِكَ مِنْهُ ؛ تَجَاوَزُوا عَنْهُ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muwsaa Al-Badriy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu mmoja aliyekuwa kabla yenu aliitwa kuhesabiwa, naye hakupatikana na kheri ya aina yoyote isipokuwa alikuwa akiamiliana vizuri katika biashara na madeni yake na watu, na alikuwa sahali sana katika hayo. Na alikuwa akiwaamuru watumishi wake wawapatie muda wenye matatizo na shida. Akasema Allaah 'Azza wa Jalla: 'Sisi tuna haki zaidi katika hilo kuliko yeye, hivyo msameheni'." [Muslim]

 

Hadiyth – 6

وعن حذيفة رضي اللهُ عنه قَالَ : أُتَي اللهُ تَعَالَى بِعَبْدٍ مِنْ عِبَادِهِ آتَاهُ اللهُ مَالاً ، فَقَالَ لَهُ : مَاذَا عَمِلْتَ في الدُّنْيَا ؟ قَالَ : (( وَلاَ يَكْتُمُونَ اللهَ حَدِيثاً )) قَالَ : يَا رَبِّ آتَيْتَنِي مَالَكَ ، فَكُنْتُ أُبَايعُ النَّاسَ ، وَكَانَ مِنْ خُلُقِي الجَوَازُ ، فَكُنْتُ أَتَيَسَّرُ عَلَى المُوسِرِ، وَأُنْظِرُ المُعْسِرَ . فَقَالَ الله تَعَالَى : (( أنَا أَحَقُّ بِذا مِنْكَ تَجَاوَزُوا عَنْ عَبْدِي )) فَقَالَ عُقْبَةُ بن عامِر ، وأبو مسعودٍ الأنصاريُّ رضي الله عنهما : هكَذا سَمِعْنَاهُ مِنْ فيِّ رسولِ الله صلى الله عليه وسلم . رواه مسلم

Amesema Hudhayfah (Radhwiya Allaahu 'anhu): Ataletwa kwa Allaah Ta'aalaa mja miongoni mwa waja Wake aliyepewa mali na Allaah. Atamuuliza: "Umefanya nini duniani?" Atasema na wala hataweza kuficha chochote mbele ya Allaah: "Ee Rabb Wangu! Ulinipatia mali yako, ambayo nilifanya biashara na watu. Na katika maadili yangu ni kuwavumilia wadeni wangu. Nilikuwa sahali kwa aliyekuwa mwepesi na kumpatia mtu mwenye dhiki muda." Hapo Allaah Ta'aalaa atasema: "Mimi nina haki zaidi katika hilo kuliko wewe, hivyo mvumilieni na msameheni mja wangu huyu." Akasema 'Uqbah bin 'Aamir na Abu Mas'uwd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhumaa): "Hivi ndivyo tulivyosikia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)." [Muslim] 

 

Hadiyth – 7

وعن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه قَالَ: قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( مَنْ أَنْظَرَ مُعْسِراً ، أَوْ وَضَعَ لَهُ ، أظَلَّهُ اللهُ يَومَ القِيَامَةِ تَحْتَ ظِلِّ عَرْشِهِ يَومَ لا ظِلَّ إِلاَّ ظِلُّهُ )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kumpatia muda mdeni wake aliye na dhiki au kumuondolea (kumsamehe) deni lake, atawekwa chini ya kivuli cha Allaah Siku ya Qiyaamah chini ya kivuli cha Arshi Yake siku ambayo hakuna kivuli ila kivuli Chake." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Hadiyth – 8

وعن جابر رضي اللهُ عنه : أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلم ، اشْتَرَى مِنْهُ بَعِيراً، فَوَزَنَ لَهُ فَأرْجَحَ . متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinunua kutoka kwake ngamia na kumlipa thamani ya juu zaidi baada ya kupimwa. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth – 9

وعن أَبي صَفْوَان سُويْدِ بنِ قيسٍ رضي اللهُ عنه قَالَ : جَلَبْتُ أنَا وَمَخْرَمَةُ العَبْدِيُّ بَزّاً مِنْ هَجَرَ ، فَجَاءنا النبيُّ صلى الله عليه وسلم ، فَسَاوَمَنَا بسَرَاوِيلَ ، وَعِنْدِي وَزَّانٌ يَزِنُ بِالأجْرِ ، فَقَالَ النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم لِلْوَزَّانِ : (( زِنْ وَأرْجِحْ )) رواه أَبُو داود ، والترمذي وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Abu Swafwaan Suwayd bin Qays (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Mimi na Makhramah Al-'Abdiy tulileta nguo kutoka Hajar kwa ajili ya kuuza. Alikuja kwetu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kununua suruali. Nilikuwa na mtu aliyekuwa akipima vitu kwa ujira. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mpimaji huyo: "Ipime (hii suruali) kwa thamani yake na uongeze kitu kidogo juu yake." [Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

 

Share