005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Kiapo Hakiapiwi Ila Kwa Allaah Tu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

05- Kiapo Hakiapiwi Ila Kwa Allaah Tu

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Toka kwa Ibn ‘Umar kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimpata ‘Umar bin Al-Khattwaab akiwa anakwenda na msafara huku akiapa kwa baba yake.  Akamwambia:

 

"ألاَ إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَنْهَاكُمْ أَنْ تَحْلِفُوا بِآبَائِكُمْ فَمَنْ كَانَ حَالِفًا فَلْيَحْلِفْ بِاللَّهِ أَوْ لِيَصْمُتْ"

 

“Jua utambue kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Anakukatazeni kuapa kwa baba [mababu] zenu, na mwenye kuapa, basi na aape kwa Allaah, au anyamaze”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6646) na Muslim (1646)].

 

Hadiyth hii inadulisha mambo mawili:  [Fat-hul Baariy (11/533)].

 

La Kwanza:  Inakataza kuapa kwa asiye Allaah.  Katika Hadiyh hii ya ‘Umar, mababu wamehusishwa kwa kuwa ndio walioapiwa, au wamehusishwa kwa kuwa ndio waliokuwa wakiapiwa zaidi kwa ushahidi wa neno la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika riwaayah nyingine isemayo:

 

"وَكَانَتْ قُرَيْشٌ تَحْلِفُ بِآبَائِهَا"

 

“Na Maquraysh walikuwa wakiapa kwa mababu zao”.  [Al-Bukhaariy (3836) na Muslim (1636)].

 

Na linadulisha ujumla wa katazo la kuapia kwa chochote kisicho Allaah neno lake Rasuli:

 

"مَنْ كَانَ حَالِفًا فَلاَ يَحْلِفْ إِلاَّ بِاللَّه"

 

“Mwenye kuapa, basi asiape kwa kingine chochote isipokuwa kwa Allaah tu”.

 

La Pili:  Kwamba mwenye kuapa kwa asiye Allaah, akaapa kwa chochote kile, basi kiapo chake hakifungiki, ni sawa akiapia kwa chenye kustahiki kutukuzwa utukuzo usiobeba maana ya ‘ibaadah kama Manabii, Malaika, ‘Ulamaa, watu wema, mababu na Al-Ka’abah, au kisicho stahiki kutukuzwa kama watu wa kawaida, au chenye kustahiki kudharauliwa na kudhalilishwa kama Mashaytwaan na vingine vyenye kuabudiwa kinyume na Allaah.  Kigezo cha kutofungika kiapo chake hapa ni kuwa hakuapa kwa Allaah, wala kwa lenye kuwakilisha Dhati Yake.

 

·        Faida:

 

Mwislamu Akimwapia Nduguye Kwa Allaah, Basi Inatakikana Amsadiki Hata Kama Atajua Kinyume Cha Ukweli Wa Jambo.

 

Toka kwa Abu Hurayrah amesema, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

"رَأَى عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ عَلَيْهِ السَّلاَمُ رَجُلاً سَرَقَ، فَقَالَ عِيسَى أسَرَقْتَ قَالَ كَلاَّ وَالَّذِي لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ.‏ فَقَالَ عِيسَى آمَنْتُ بِاللَّهِ وَكَذَّبْتُ عَيْنيْ"

 

“‘Iysaa bin Maryam (‘Alayhis Salaam) alimwona mtu ameiba.  ‘Iysaa akamwambia: Umeiba?  Akasema hapana la hasha, naapa kwa Ambaye hapana mwingine wa kuabudiwa isipokuwa Yeye.  ‘Iysaa akasema: Nimemwamini Allaah, na nimelikadhibisha jicho langu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (3444) na Muslim (2368)].

                                               

 

 

Share