008-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kuapa Kwa Qur-aan

 

 Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

08- Kuapa Kwa Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Qur-aan ni Maneno ya Allaah ambayo hayakuumbwa.  Na Maneno ya Allaah ni Sifa kati ya Sifa Zake.  Na kwa ajili hiyo, Jumhuwri ya ‘Ulamaa –kinyume na Abu Haniyfah- wanasema kuwa inajuzu kuapa kwa Qur-aan, na mtu akiapa kwayo, basi kiapo kinafungika.  Kutilia nguvu hili ni kuwa, kuomba kinga (kusema A’uwdhu bil Laah) hakuwi isipokuwa kwa Allaah tu, mbali na kuthibiti hilo toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa alikuwa anaomba kinga kwa baadhi ya Sifa za Allaah Ta’aalaa.  Alikuwa anasema:

 

"أَعُوذُ بِوَجْهِكَ..."

 

“Najilinda kwa Wajihi Wako…”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4628) na wengineo kutoka Hadiyth ya Jaabir].

 

Na:

 

"أَعُـوْذُ بِكَلِـماتِ اللّهِ التّـامّاتِ..."

 

“Najilinda kwa Maneno ya Allaah Yaliyotimia…”. [Hadyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (2708) na wengineo toka Hadiyth ya Khawlah bint Hakiym].

 

Na:

 

"أَعُوْذُ بِرِضَاكَ مِنْ سَخَطِكَ"

 

“Najilinda kwa Radhi Zako kutokana na Hasira Zako”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (486) na wengineo toka Hadiyth ya ‘Aaishah].

 

Na mfano wa haya ni mengi.  [Al-Mughniy (11/193) na Majmuw’ul Fataawaa (35/237).  Ibn Al-Hammaam na Al-‘Ayniy wameungana na madhehebu ya Jumhuwri ya kufungika kiapo kwa kuapa kwa Qur-aan. Angalia Al-Fiqhul Islaamiy wa Adillatuhu (3/379)].

 

·        Zindusho

 

Mwenye kuapa kwa Musw-haf, ikiwa anakusudia kwao Qur-aan iliyoandikwa ndani yake ambayo ni Maneno ya Allaah, basi itajuzu. Lakini akikusudia karatasi zilizoandikwa, basi haijuzu.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

 

Share