010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Mwenye Kusema: وَعَهْدِ اللَّـهِ “Naapa kwa Ahadi ya Allaah”
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
010- Mwenye Kusema: وَعَهْدِ اللَّـهِ “Naapa kwa Ahadi ya Allaah”
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na aliyesema: “Naapa kwa Ahadi ya Allaah”, au “Ni juu yangu Ahadi”, je kiapo chake kinafungika? Wana kauli tatu katika hili:
Kauli Ya Kwanza: Kiapo Kinafungika Kwa Kuapa Kwa Ahadi Ya Allaah
Ni kauli ya Al-Hasan, Twaawuws, Ash-Sha-‘abiy, Al-Awzaa’iy, Maalik na Ahmad. Hoja yao ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأَوْفُوا بِعَهْدِ اللَّـهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلَا تَنقُضُوا الْأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا"
“Na timizeni Ahadi ya Allaah mnapoahidi, na wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha”. [An-Nahl (16:91)].
Kauli Yake Ta’aalaa hapa haikutanguliwa na chochote isipokuwa kutajwa Ahadi, na kwa hivyo, imejulikana kuwa ni kiapo. Wamejibiwa hoja yao hii kwa kuambiwa kuwa hailazimu kuatwifiwa viapo kwa Ahadi kuwa ndio iwe kiapo.
2- Toka kwa Ibn Mas-‘uwd, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
"مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ كَاذِبَةٍ، لِيَقْتَطِعَ بِهَا مَالَ رَجُلٍ مُسْلِمٍ أَوْ قَالَ أَخِيهِ لَقِيَ اللَّهَ وَهْوَ عَلَيْهِ غَضْبَانُ ". فَأَنْزَلَ اللَّهُ تَصْدِيقَهُ: إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا"
“Mwenye kuapa kiapo cha uongo ili aweze kupora kwacho mali ya mtu Muislamu, au alisema nduguye (Muislamu), basi atakutana na Allaah hali ya kuwa Amemkasirikia)). Allaah Akateremsha uthibitisho Wake [kwa hilo Akisema]: Hakika wale wanaobadilisha Ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo”.
Hapa Allaah Ameipa ahadi umahususi na kipaumbele kuliko viapo vingine, na hii inaonyesha uhakika wa kuiapia. Na kwa kuwa pia Ahadi ya Allaah ni yale ambayo Ameyawajibisha juu ya Waja Wake na yale Aliyowapa Waja Wake kama Alivyosema:
"وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ"
“Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah”.
3- Ahadi inaitwa vile vile yamini. Inakuwa kama vile amesema: “Naapa kwa Yamini ya Allaah”. Na ile ni yamini, na ndivyo ilivyo hapa pia.
4- Maana yake inachukulika kama: Maneno ya Allaah, nayo ni Sifa Yake.
5- Ada na mazoea ya matumizi yamelithibitisha. Hivyo ni lazima liwe yamini kwa kulitaja.
Kauli Ya Pili: Kiapo Hakifungiki Kwa Kuapa Kwa Ahadi Ya Allaah Ila Tu Mtu Akinuwia
Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy. Hoja yake ni kuwa neno hili hutumika kwa maana nyingine isiyo yamini (kama Usia wa Allaah kwa Waja Wake kwa kufuata Maamrisho Yake na mengineyo). Hivyo haligeuki na kubeba maana ya yamini ila kwa niya.
Kauli Ya Tatu: Kuapa Kwa Ahadi Ya Allaah Si Yamini
Ni kauli ya Abu Haniyfah na Ibn Hazm. Hoja zao ni:
1- Kuapa kwa Ahadi ya Allaah si kuapa kwa Sifa za Allaah ambazo inajuzu kuapa kwazo.
2- Yamini haiwi ila kwa Allaah tu.