013-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Mwenye Kusema: وَايْمُ اللَّهِ “Waiymul Laah”
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
013- Mwenye Kusema: وَايْمُ اللَّهِ “Waiymul Laah”
Yamini inafungika kwa kusema hivyo. Hili limethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Katika Hadiyth ya ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
" وَايْمُ اللَّهِ، لَوْ أَنَّ فَاطِمَةَ بِنْتَ مُحَمَّدٍ سَرَقَتْ لَقَطَعَ مُحَمَّدٌ يَدَهَا"
“Naapa kwa Allaah, lau Faatwimah bint Muhammad angeiba, basi Muhammad angeukata mkono wake”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6788) na Muslim (1688)].
Na katika Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) -kuhusu kisa cha Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) ambapo aliapa kuwa atawazungukia wakeze 90 [usiku mmoja na kila mmoja atamzalia mtoto mpanda farasi atakayepigana Jihaad]-, Rasuli anasema:
"وَايْمُ الَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَوْ قَالَ إِنْ شَاءَ اللَّهُ، لَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فُرْسَانًا أَجْمَعُونَ "
“Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, lau angesema: In Shaa Allaah, basi wangelipigana Jihaad katika Njia ya Allaah wakiwa wote wapanda farasi”. [Hadiyth Swahiyhy. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6639) na Muslim (1654)].
Asili ya " وَايْمُ اللَّهِ " ni " أَيْمٌنُ الله" aymunul Laah, nalo ni jina linalotumika kwa kiapo kwa maana ya “Yamini ya Allaah”.