031-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Nadhiri Ya “Al-Lijaaj” (Nadhiri Itokanayo Na Hasira)
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ
Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri
031- Nadhiri Ya “Al-Lijaaj” (Nadhiri Itokanayo Na Hasira)
Hii ni nadhiri ambayo mtu anakusudia kwayo kujizuia na jambo au kuhimizia alifanye (wakati yuko katika hali ya hasira au hamaki), na si kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah. Ni kama kusema: “Nikifanya kadhaa mimi, basi ni juu yangu kwa Allaah nihiji, au nitoe swadaqah au nifunge”, na mfano wa hivyo. Kauli hii inatokea pale pale inapotokea yamini, kwa kuwa mweka nadhiri hapa hakukusudia kujikurubisha kwa Allaah, na maneno yanazingatiwa kwa maana yake na si kwa matamshi yake. Na haya ndio hasa makusudio yake ya kufanya au kutokufanya. Na juu ya msingi huu, si lazima ayatekeleze maneno yake, bali atalazimika kutoa kafara ya kiapo kama atavunja nadhiri yake.
Haya ni madhehebu ya Ahmad na Ash-Shaafi’iy. Nayo ni madhehebu ambayo Abu Haniyfah aliyarejelea. Ni kauli pia ya Ishaaq, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr na Ibn Al-Mundhir. Vile vile, ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Kadhalika, ni kauli ya Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, ‘Aaishah na Maswahaba wengine. [Fat-hul Qadiyr (5/93), Al-Majmuw’u (8/459), Al-Mughniy (11/194) na Majmuw’ul Fataawaa (35/253)].
Imesimuliwa toka kwa ‘Imraan bin Huswayn ikiwa marfuw’u:
"لاَ نَذْرَ فِي غَضَبٍ وَكَفَّارَتُهُ كَفَّارَةُ الْيَمِينِ".
“Nadhiri haizingatiwi katika hali ya hasira, na kafara yake ni kafara ya yamini”.
Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haizingatiwi. [Imekharijiwa na Ahmad (4/433) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (2587)].
Na Ibn ‘Abbaas aliulizwa:
"مَا تَقُوْلُ فِي امْرَأةٍ جَعَلَتْ بُرْدَهَا عَلَيْهَا هَدْيًا إِنْ لَبِسَتْهُ؟ فَقَالَ: ابْنُ عَبَّاسٍ: فِيْ غَضَبٍ أَمْ فِيْ رِضا؟ قَالُوْا: فِيْ غَضَبٍ، قَالَ: إِنَّ الله تَعَالى لا يُتَقَرَّبُ إِلَيْهِ بِالْغَضَبِ، لِتُكَفِّرَ عَنْ يَمِيْنِهَا".
“Unasemaje kuhusu mwanamke aliyesema atachinja kama atajifunika burda lake? Ibn ‘Abbaas akauliza: Katika hali ya ghadhabu au ya kawaida? Wakasema: Katika hali ya ghadhabu. Akasema: Hakika Allaah Ta’aalaa hakurubiwi kwa ghadhabu. Basi akitolee kafara kiapo chake”. [Isnaad yake ni Layyin. Sheikh wa Uislamu (35/256) ameinasibisha kwa Al-Athram].
Maalik na Abu Haniyfah –katika kauli yake ya zamani- wamesema ni lazima atekeleze nadhiri.