01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kuwinda Na Hukmu Zake:Taarifu Na Hukmu Ya Kuwinda:
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الصَّيْدُ وَأَحْكَامُهُ
Kuwinda Na Hukmu Zake
01-Kuwinda Na Hukmu Zake: Taarifu Na Hukmu Ya Kuwinda:
"الصَّيْدُ" ni “maswdar” (kiini) ya kitenzi cha wakati uliopita "صَادَ" (amewinda) na cha wakati uliopo "يَصِيْدُ" (anawinda). Na katika lugha, ina tafsiri mbili:
Kwa tafsiri ya kwanza, inaweza kukusudiwa kuwinda, mkono kumfikia mnyama mwindwa, kumkamata na kumdhibiti (yaani purukushani yote ya kumsaka mnyama hadi kumtia mkononi). Ni kama Neno Lake Ta’alaa:
"وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَاصْطَادُوا"
“Na mkishatoka kwenye ihraam basi windeni (mkitaka)”. [Al-Maaidah : 03].
Na kwa tafsiri ya pili, inaweza kukusudiwa mnyama mwindwa mwenyewe kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ"
“Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko k atika ihraam”. [Al-Maaidah : 95].
Na kwa mujibu wa tafsiri ya kwanza, taarifu ya "الصَّيْدُ"kiistilahi inakuwa ni kumwinda na kumkamata mnyama pori ambaye kikawaida ni halali kuliwa, asiyemilikiwa na mtu, na ambaye hawezi kuwa rafiki wa binadamu au kutiishwa (kama alivyo ng’ombe n.k).
Ama kwa tafsiri ya pili, "الصَّيْدُ"taarifu yake kiistilahi inakuwa ni mnyama pori kimaumbile, asiyemilikiwa na yeyote, na ambaye hawezekani kutulizwa au kudhibitiwa.
Hukmu Ya Kuwinda:
‘Ulamaa wamekubaliana kwa kauli moja kuwa kuwinda na kumla mnyama aliyewindwa ni jambo la halali. Na hii ni kutokana na uthibitisho toka kwenye Qur-aan na Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
(a) Kutoka kwenye Qur-aan:
1- Ni Kauli Yake Ta’aalaa:
"أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ ۖ وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا"
“Mmehalalishiwa mawindo ya bahari, na chakula chake ni manufaa kwenu na kwa wasafiri. Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika ihraam”. [Al-An’aam : 96].
2- Na Kauli Yake Subhaanah:
"وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَاصْطَادُوا"
“Na mkishatoka kwenye ihraam basi windeni (mkitaka)”. [Al-Maaidah : 03].
3- Na Kauli Yake ‘Azza wa Jalla:
"يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۙ وَمَا عَلَّمْتُم مِّنَ الْجَوَارِحِ مُكَلِّبِينَ تُعَلِّمُونَهُنَّ مِمَّا عَلَّمَكُمُ اللَّـهُ ۖ فَكُلُوا مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهِ"
“Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa vilivyo vizuri na mlivyowindiwa na wanyama na ndege wakali mliowafundisha kiweledi, na mnawafunza katika ambayo Allaah Amekufunzeni. Basi kuleni walichokukamatieni, na mkitajie Jina la Allaah”. [Al-Maaidah : 04].
(b) Ama kwenye Hadiyth:
Ni Hadiyth ya ‘Adiyy bin Haatim aliyesema:
"قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنِّي أُرْسِلُ الْكِلاَبَ الْمُعَلَّمَةَ فَيُمْسِكْنَ عَلَىَّ وَأَذْكُرُ اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهِ ، فَقَالَ: "إِذَا أَرْسَلْتَ كَلْبَكَ الْمُعَلَّمَ وَذَكَرْتَ اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهِ فَكُلْ" . قُلْتُ وَإِنْ قَتَلْنَ ، قَالَ : "وَإِنْ قَتَلْنَ مَا لَمْ يَشْرَكْهَا كَلْبٌ لَيْسَ مَعَهَا" . قُلْتُ لَهُ : فَإِنِّي أَرْمِي بِالْمِعْرَاضِ الصَّيْدَ فَأُصِيبُ ، فَقَالَ : "إِذَا رَمَيْتَ بِالْمِعْرَاضِ فَخَزَقَ فَكُلْهُ ، وَإِنْ أَصَابَهُ بِعَرْضِهِ فَلاَ تَأْكُلْهُ "
“Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi huwachochea mbwa wangu waliopata mafunzo wakanikamatia (wanyama), nami hulidhukuru Jina la Allaah wakati nikiwaachilia. Akasema: Ukimwachilia mbwa wako aliyepata mafunzo, na ukalitaja Jina la Allaah wakati wa kumwachilia, basi kula”. Nikamuuliza: Hata kama watamuua? Akasema: Hata kama watamuua madhali hajashirikiana nao mbwa mwingine asiye pamoja nao”. Nikamwambia: Mimi ninamrushia mnyama mi’iradh nikampata. Akasema: Ukimrushia mi’iradh ikamwingia hadi ndani ya mwili, basi mle, lakini ikimpiga kwa ubavu (na si kwa ncha yake), basi usimle”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2054) na Muslim (1929)].
Mi’iradh "المِعْرَاضُ"ni kipande kizito cha mti kilichochongwa nchani, au kilichofungiwa nchani mwake kipande cha chuma chenye ncha kali na kuwa mithili ya mkuki.