07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia: Taratibu Njema Za Kuchinja Ngamia Na Mnyama Mfano Wake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
07-Chinjo La Kisharia: Taratibu Njema Za Kuchinja Ngamia Na Mnyama Mfano Wake
Yamestahabiwa katika kumchinja ngamia na mnyama mwenye shingo ndefu mfano wake, yale yote yaliyostahabiwa katika kuwachinja wanyama wenye shingo fupi (kama ng’ombe, mbuzi n.k). Isipokuwa ngamia huchinjwa akiwa amesimama kwa miguu miwili na mkono mmoja wa kulia, na mkono wake wa kushoto hufungwa. [Al-Badaai’u (5/41), Nihaayatul Muhtaaj (8/111), na Al-Muqni’u (1/474)].
1- Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ"
“Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa)”. [Al-Hajj: 36].
Ibn ‘Abbaas amesema صَوَافَّ yaani قِيَامًا kwa maana wakiwa wamesimamishwa.
2- Katika Hadiyth ya Anas bin Maalik wakati Rasuli akifanya Hijja:
...وَنَحَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم بِيَدِهِ سَبْعَ بَدَنَاتٍ قِيَامًا ، وَضَحَّى بِالْمَدِينَةِ بِكَبْشَيْنِ أَقْرَنَيْنِ أَمْلَحَيْنِ"
“ …na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akachinja ngamia saba kwa mkono wake wakiwa wamesimama, na huko Madiynah alichinja madume mawili ya kondoo yenye pembe na rangi nyeupe na nyeusi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1714) na Muslim (690)].
3- Toka kwa Ziyaad bin Jubayr, amesema:
"رَأَيْتُ ابنَ عُمَرَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) أَتَى عَلَى رَجُلٍ قَدْ أَنَاخَ بَدَنَتَهُ يَنْحَرُهَا قَالَ: ابْعَثْهَا قِيَامًا مُقَيَّدَةً سُنَّةَ مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"
“Nilimwona Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) akipita na kumkuta mtu anamchinja ngamia wake akiwa amempigisha magoti. Akamwambia: Mnyanyue umchinje akiwa amesimama na amefungwa (mkono wa kushoto). Hii ndiyo Sunnah ya Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1713) na Muslim (1320)].