05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Sifa Za Ukamilifu Zinazopendeza Kuwepo Kwa Mnyama Wa Kudhwahiwa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
05-Udhwhiyah: Sifa Za Ukamilifu Zinazopendeza Kuwepo Kwa Mnyama Wa Kudhwahiwa:
[Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/465), Al-Haawiy (19/92), Al-Mughniy (9/347), na Al-Muhallaa (7/370)]
(a) Anapendeza mnyama aliyenona zaidi na aliye mkamilifu zaidi. Kuchinja kondoo aliyenona vizuri ni bora zaidi kuliko kuchinja kondoo wawili walio na hali duni kuliko huyo aliyenona, kwa kuwa lengo kuu hapo ni nyama, na aliyenona ndiye mwenye nyama nyingi zaidi na nzuri zaidi, na nyama nyingi ni bora zaidi kuliko shahamu nyingi zaidi. Yanayothibitisha kuwa aliyenona vizuri anastahabiwa zaidi ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾
32. Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj: 22].
Ash-Shaafi’iy (Rahimahul Laah) ametolea dalili kwa Aayah hii kuwa inastahabiwa kumwadhimisha mnyama wa kuchinjwa na kumnenepesha. [Al-Haawiy (19/94)].
2- Abu Umaamah bin Sahl amesema:
"كُنَّا نُسَمِّنُ الأُضْحِيَةَ بالمَدِيْنَةِ ، وَكَانَ المسْلِمُوْنَ يُسَمِّنُوْنَ"
“Tulikuwa tukiwanenepesha wanyama wa kudhwahi Madiynah, na Waislamu walikuwa wakinenepesha”. [Isnaad yake ni Hasan. Al-Bukhaariy (10/12) kasema ni Mu’allaq, na Abu Nu’aym kasema ni Mawswuul katika Mustakhraji wake kama ilivyo katika At-Ta-‘aliyq (5/6)].
(b) Wanyama walio bora zaidi
Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik, wanaona kwamba wanyama bora zaidi wa kudhwahi ni kwanza kabisa ngamia, kisha ng’ombe, halafu mbuzi na kondoo. Wametoa dalili kadhaa kuhusiana na hili:
1- Kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمْعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ، ثُمَّ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الأُوْلَى فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ ..."
“Mwenye kuoga kikamilifu siku ya Ijumaa kama anavyofanya katika ghuslu ya janaba, kisha akaenda (Msikitini) katika saa la mwanzo, anakuwa kama ametoa swadaqah ngamia, na mwenye kwenda saa la pili, anakuwa kama ametoa ng’ombe, na mwenye kwenda saa la tatu, anakuwa kama ametoa kondoo dume mwenye pembe..”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)].
2- Hadiyth ya Abu Dharrin (Radhwiya Allaah ‘anhu), alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"فَأَيُ الرِّقَابِ أَفْضَلُ؟ قَالَ : أَغْلَاهَا ثَمَنًا ، وَأَنْفَسُهَا عِنْدَ أَهْلِهَا..."
“Ni mtumwa yupi aliye bora zaidi (kuachwa huru)? Akasema: Ni mwenye thamani zaidi, na aliye bora zaidi kwa watu wanaommiliki….”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2518) na Muslim (84)].
Wamaalik wamesema: Mbora zaidi ni mbuzi na kondoo, kisha ng’ombe, halafu ngamia kutokana na uzuri wa nyama. Na kwa vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wa kondoo wenye rangi nyeupe na nyeusi. Kadhalika, wametoa dalili kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾
107. Na Tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu. [Asw-Swaaffaat: 37].
(c) Mbora zaidi ni mweupe, kisha wa rangi ya udongo, halafu mweusi. Hii ni kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wa kondoo wenye rangi nyeupe iliyochanganyika kidogo na weusi.
Shaykhul Islaam (26/308) amesema: “Mwenye rangi ya udongo ni bora zaidi kuliko mweusi. Na kama kuna weusi kuzunguka macho yake na mdomo wake, na kwenye miguu yake, basi huyo atafanana na mnyama aliyemchinja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ninasema: “Anaashiria kwa maneno yake haya Hadiyth ya ‘Aaishah:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ..."
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi. Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiyah). [Imekharijiwa na Muslim (1967) na wengineo].
An Nawawiy kasema: “Maana yake ni kwamba miguu yake na tumbo lake, na kuzungukia macho yake kuna weusi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
(d) Kuchinja dume ni bora zaidi kuliko jike. Hii ni kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na mtumwa bora zaidi wa kuachwa huru:
"أَغْلَاهَا ثَمَنًا ، وَأَنْفَسُهَا عِنْدَ أَهْلِهَا..."
“Ni mwenye thamani zaidi, na aliye bora zaidi kwa watu wanaommiliki….”.