10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Yasiyopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

10-Udhwhiyah: Yasiyopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama

 

 

1-  Haijuzu kuuza chochote kitokanacho na mnyama.  Si Ngozi, wala sufi, wala nywele, wala nyama, wala mfupa wala kingine chochote kiwacho.  Katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"...وَلا تَبِيْعُوا لُحُوْمَ الهَدْيِ وَالأَضَاحِي ، فَكُلُوا وَتَصَدَّقُوا وَاسْتَمْتَعُوا بِجُلُوْدِهَا وَلاَ تَبِيْعُوهَا .."

 

“…wala msiuze nyama za wanyama wa amali za Hijja na wa kudhwahi, bali kuleni, zigaweni swadaqah, na tumieni ngozi zao, lakini msiziuze..”.  [Hadiyth hii ni Dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Ahmad katika Al-Musnad (4/15)].

 

Lakini mali inayostahiki kwa ‘ibaadah kwa ajili ya Allaah, haijuzu kwa mtoaji wake kuiuza kama zakah na kafara.  Na inadulisha juu ya hili pia kwamba haijuzu kumlipa mchinjaji ujira wake kutokana na nyama ya udhwhiya. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad.  Abu Haniyfah amesema:  Anaweza kuuza chochote kitokanacho na mnyama na kutoa swadaqah kwa thamani yake!!  Lenye nguvu ni kuwa hilo halipo.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

                                                                   

  2-  Mchinjaji hapewi ujira wake kutokana na udhwhiyah.  Kwa kuwa kama atapewa, atakuwa kama anamegewa fungu la thawabu za mnyama huyo huyo.  Mwenye mnyama anatakiwa amlipe mchinjaji ujira wake kutokana na mali yake, lakini pia anaruhusiwa kumpa chochote cha mnyama kama ni swadaqah, lakini si kama ujira wake.

 

‘Aliy amesema:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَمَرَهُ أَنْ يَقُومَ عَلَى بُدْنِهِ، وَأَنْ يَقْسِمَ بُدْنَهُ كُلَّهَا، لُحُومَهَا وَجُلُودَهَا وَجِلاَلَهَا، وَلاَ يُعْطِيَ فِي جِزَارَتِهَا شَيْئًا‏"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru asimamie uchinjaji wa ngamia wake, na awagawe wote kuanzia nyama zao, ngozi zao na (hata) matandiko waliyovishwa (au vigwe), na asitoe chochote kama malipo ya kuchinjiwa kutoka kwao”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Na katika tamshi jingine:

 

"نَحْنُ نُعْطِيْهِ مِنْ عِنْدِنَا"

 

“Sisi tunampa kutoka mifukoni mwetu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1317)].

 

Haya ndiyo yaliyosemwa na Jumhuwr ya ‘Ulamaa.  Lakini  Hasan Al-Baswriy, na ‘Abdullaah bin ‘Ubayd bin ‘Umayr wamejuzisha mchinjaji apewe ngozi kama ujira wake.

 

Faida: 

 

1-  Kudhwahi mnyama ni bora zaidi kuliko kutoa swadaqah thamani yake.

 

Huu ndio msimamo wa ‘Ulamaa.  Kwa kuwa udhwhiyah ni sunnah kokotezwa kinyume na swadaqah ya hiari, mbali na kuwa udhwhiya ni nembo kati ya nembo za Uislamu.  [At-Tamhiyd (23/192), Al-Majmuw’u (8/425) na Majmuw’ul Fataawaa (36/304)].

 

 

2-  Mnyama akipotea kabla ya kuchinjwa, basi aliyekusudia kudhwahi halazimiwi chochote.

 

Tamiym bin Huwaysw amesema:

 

 "اشْتَرَيْتُ شَاةً بِمِنَى أُضْحِيَةً فَضَلَّتْ ، فَسَأَلْتُ ابْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنْ ذَلِكَ فَقَالَ : لاَ يَضُرُّكَ"

 

“Nilinunua kondoo Mina kwa ajili ya kudhwahi akapotea.  Nikamuuliza Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) akasema:  “Hakuna neno”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (9/289) na Ibn Hazm (7/358)].

 

Ibn ‘Umar amesema:

 

" مَنْ أَهْدَى بَدَنَةً ثُمَّ ضَلَّتْ أَوْ مَاتَتْ فَإِنَّهَا إِنْ كَانَتْ نَذْرًا أَبْدَلَهَا وَإِنْ كَانَتْ تَطَوُّعًا فَإِنْ شَاءَ أَبْدَلَهَا وَإِنْ شَاءَ تَرَكَهَا"

 

“Mwenye kujitolea mnyama kisha akapotea au akafa, ikiwa ni wa nadhiri, basi alete mwingine badala yake, na kama alikuwa ni wa swadaqah tu, basi ikiwa atataka, ataleta mwingine badala yake, au akitaka ataacha”.   [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Maalik (866) na Al-Bayhaqiy (9/289)].

 

Ninasema:  “Linaunganishwa na hili kama ataugua au akafa kabla ya kuchinjwa.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

 

3-  Je mnyama wa kudhwahiwa anaweza kupelekwa mji mwingine?

 

Asili, ni kwamba mahala pa mnyama ni pale alipo mmiliki wake aliyekusudia kudhwahi.  Hii ni kwa vile masikini wa sehemu ile watakuwa na kiu kubwa ya kugawiwa nyama yake.  Lakini pamoja na hivyo, hakuna kizuizi cha kumpeleka sehemu nyingine kama kutakuwa na maslaha makubwa zaidi.  Katika Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullaah kuhusiana na nyama za wanyama wa kuchinjwa amesema:

 

"كُنَّا لاَ نَأْكُلُ مِنْ لُحُومِ بُدْنِنَا فَوْقَ ثَلاَثِ بمِنًى، فَرَخَّصَ لَنَا النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏ "‏ كُلُوا وَتَزَوَّدُوا ‏"‏‏.‏ فَأَكَلْنَا وَتَزَوَّدْنَا‏"

 

“Tulikuwa hatuli nyama za wanyama wetu Mina kwa zaidi ya siku tatu, kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaturuhusu kwa kutuambia: Kuleni na chukueni masurufu ya safari.  Tukala na tukachukua”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1719) na Muslim (1972)].

 

                                                 

 

 

 

 

 

Share