06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kuwinda Na Hukmu Zake: Njia Ya Tatu Ya Uwindaji: Kuwinda Kwa Bunduki
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الصَّيْدُ وَأَحْكَامُهُ
Kuwinda Na Hukmu Zake
06- Kuwinda Na Hukmu Zake: Njia Ya Tatu Ya Uwindaji: Kuwinda Kwa Bunduki
Bunduki za kuwindia za kisasa zinatumia risasi. Ziko risasi za mviringo, na ziko zenye ncha, na zote zinapenya kwenye mwili wa mnyama na kumjeruhi. Hivyo risasi hizi ni halali kuwindia.
Hapa inafaa kueleza kwamba Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanashurutisha kwamba zana ya kuwindia ni lazima iwe na ncha kali!. Na hili linaweza kuwa ni mushkil juu ya uhalali wa kuwinda kwa kutumia bunduki yenye kutumia risasi za mviringo. Isipokuwa linaloonekana ni kwamba makusudio yao ya ncha kali ni kile chenye kupenya na kuingia ndani ya mwili wa mnyama na kumjeruhi. Na hiki ndicho kiini kama inavyoonekana katika dalili za suala hili. Na kwa muktadha huo, utata unaondoka. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Je, Inafaa Kuwinda Kwa Kutumia Jiwe, Fimbo Na Mfano Wa Hivyo?
[Al-Mughniy (9/313), Al-Muhallaa (7/460) na Naylul Awtwaar (8/156)]
Jiwe lisilo na ncha ambalo lau atapigwa nalo mnyama halitoweza kupenya ndani ya mwili wake au kumjeruhi, ikiwa jiwe hili litamuua, basi si halali kuliwa mnyama huyo, kwa kuwa anakuwa amekufa kwa kupigwa (na si kwa kujeruhiwa). Hii ndio kauli ya Fuqahaa wote. Na dalili zishaelezwa nyuma kuhusiana na sharti ya kuingia zana ya kuwindia ndani ya mwili wa mnyama na kumjeruhi, ili awe halali kuliwa.
Toka kwa ‘Abdullaah bin Mughaffal "رَضِيَ اللهُ عَنْهُ" amesema:
"أَنَّ رَسُوْلَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنِ الْخَذْفِ وَقَالَ : "إِنَّهَا لاَ تَصِيْدُ صَيْدًا ، وَلاَ تَنْكَأُ عَدُوًا ، وَلكِنَّهَا تَكْسِرُ السِّنَّ وَتُفْقِأُ العَيْنَ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kutumia manati akisema: Manati haiwezi kuwinda mnyama, wala haiwezi kumjeruhi na kumuua adui, bali manati inavunja jino na inapofua jicho.” [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5479) na Muslim (1954)].
Akimpata Mnyama Baada Ya Masiku Kadhaa
Mwindaji akimlenga mnyama akampata kisha mnyama akapotea, halafu akaja kumpata hata baada ya kupita masiku –lakini si ndani ya maji- , basi atakuwa ni halali, lakini kwa sharti kwamba asiwe ameharibika, au ijulikane kwamba kilichomuua si silaha yake.
‘Adiyy bin Haatim amesema, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:
إِذَا أَرْسَلْتَ كَلْبَكَ وَسَمَّيْتَ فَأَمْسَكَ وَقَتَلَ، فَكُلْ، وَإِنْ أَكَلَ فَلاَ تَأْكُلْ، فَإِنَّمَا أَمْسَكَ عَلَى نَفْسِهِ، وَإِذَا خَالَطَ كِلاَبًا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّهِ عَلَيْهَا فَأَمْسَكْنَ وَقَتَلْنَ فَلاَ تَأْكُلْ، فَإِنَّكَ لاَ تَدْرِي أَيُّهَا قَتَلَ، وَإِنْ رَمَيْتَ الصَّيْدَ فَوَجَدْتَهُ بَعْدَ يَوْمٍ أَوْ يَوْمَيْنِ، لَيْسَ بِهِ إِلاَّ أَثَرُ سَهْمِكَ، فَكُلْ، وَإِنْ وَقَعَ فِي الْمَاءِ فَلاَ تَأْكُلْ ".
“Ukimwachilia mbwa wako kukamata na ukalitaja Jina la Allaah, na mbwa akakamata na akaua, basi kula. Na kama amekula, basi usile, kwani anakuwa amejikamatia kwa ajili yake mwenyewe. Na ikiwa wamechanganyika naye mbwa wengineo ambao hawakutajiwa Jina la Allaah, wakakamata na wakaua, basi usile, kwani wewe hujui ni yupi kati yao aliyeua. Na kama utamlenga mnyama, na kisha ukampata baada ya siku moja au mbili, naye hana isipokuwa athari ya mshale wako, basi kula, lakini kama utamkuta ameanguka majini, basi usimle”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5484) na Muslim (1929)].