02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: ‘Aqiyqah (Akika): Ni Nani Anayepaswa Kuchinja ‘Aqiyqah?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
العَقِيْقَةُ
‘Aqiyqah (Akika)
02-‘Aqiyqah (Akika): Ni Nani Anayepaswa Kuchinja ‘Aqiyqah?
[Subulus Salaam (4/1429) na Al-Mawsuw’ah (30/277)]
Anayetakiwa kuchinja ‘aqiyqah ni baba mtu– au mtu anayewajibikiwa na matumizi ya mtoto- , atamnunua kwa pesa yake na si kwa pesa ya kichanga kilichozaliwa, na mtu mwingine haruhusiwi kufanya hilo ila kwa idhini yake.
Kusema hivi hakukinzani na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) cha kuwachinjia ‘aqiyqah wajukuu zake Al-Hasan na Al-Husayn. Hii ni kwa kuwepo uwezekaniko wa kwamba yeye Rasuli alikuwa ameyabeba masurufu yao na si wazazi wao, lakini pia kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao.
Mashaafi’iy wameshurutisha kwa mwenye kubeba jukumu hilo kuwa awe ni mwenye kujiweza kipesa, awe anaweza kulifanya hilo, na liwe ni la ziada katika mahitaji yake na mahitaji ya wale aliowajibikiwa kuwakimu.
Ama Mahanbali, wao wameeleza kwamba imesuniwa kwa baba kuchinja hata kama hali yake ni ngumu, na anaweza kukopa kama ataweza kulipa. Imaam Ahmad amesema: “Kama hana cha kuchinja, basi akope, nami nataraji Allaah Atampa cha kulipa, kwa kuwa amehuisha Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.