11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Taratibu Njema Za Kunywa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأَشْرِبَةُ
Vinywaji
011- Vinywaji: Taratibu Njema Za Kunywa:
1- Kupiga Bismil Laah kabla ya kunywa.
2- Kunywa kwa mkono wa kulia. Dalili kuhusu hili imetajwa katika adabu njema za kula.
3- Mtu anywe hali ya kuwa ameketi, lakini pia inajuzu kunywa kwa kusimama. Abu Hurayrah: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا يَشْرَبَنَّ أَحَدٌ مِنْكُمْ قَائِمًا ، فَمَنْ نَسِيَ مِنْكُمْ فَلْيَسْتَقِئْ"
“Asinywe kabisa mmoja wenu akiwa amesimama. Na atakayesahau kati yenu, basi ajitapishe”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (3775)].
Katazo hili linachukuliwa kama la kimakruhu na si la uharamisho. Kwani imethibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas:
"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ شَرِبَ مِنْ زَمْزَمَ مِنْ دَلْوٍ مِنْهَا وَهُوَ قَائِمٌ "
“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikunywa kwenye Zamzam kwa kutumia ndoo ya hapo akiwa amesimama”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5617) na Muslim (2027)].
4- Anywe kwa mapigo matatu, apumue kati ya kila pigo nje ya chombo.
Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapokunywa, anapumua mara mbili au tatu kwa kukitenga kinywa chake na gilasi huku akisema:
"إِنَّهُ أرْوَى وَأَبْرَأُ وَأَمْرَأُ"
“Hakika hivi kunakata haraka zaidi kiu, kunaleta afya zaidi, na kuna manufaa makubwa zaidi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5631) na Muslim (3782), na tamko ni lake].
5- Asipumulie ndani ya chombo au kupulizia humo.
Abu Qataadah: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا شَرِبَ أَحَدُكُمْ ، فَلَا يَتَنَفَّسْ فِي اَلْإِنَاءِ "
“Anapokunywa mmoja wenu, basi asipumulie ndani ya kikombe”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (153) na Muslim (267)].
Ibn ‘Abbaas:
"أّنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى أَنْ يُتَنَفَّسَ فِي الْإِنَاءِ أَوْ يُنْفَخَ فِيهِ"
“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kupumuliwa ndani ya kikombe au kupuliziwa humo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3728), At-Tirmidhiy (1889) na Ibn Maajah (3429)].
6- Asinywe mtu kwa mdomo wa kiriba au gilasi na mfano wake
Abu Hurayrah:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى أَنْ يُشْرَبَ مِنْ فَمِ السِّقَاءِ"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza maji kunywewa moja kwa moja toka mdomo wa kiriba cha kunywea maji”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5627)].
Sababu ya katazo hili ni kuwa maji hububujika na kumiminika kwa mara moja kooni, na hii huleta ugonjwa wa ini na kusababisha madhara kwa tumbo. [Ar-Rawdhwat An-Naddiyyah (2/210)].
7- Kuanza kumpa maji aliye kulia kisha anayefuatia kulia
Anas bin Maalik:
"أَنَّ رَسُوْلَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أُتِيَ بِلَبَنٍ قَدْ شِيبَ بِمَاءٍ ، وَعَنْ يَمِينِهِ أَعْرَابِيٌّ ، وَعَنْ يَسَارِهِ أَبُو بَكْرٍ ، فَشَرِبَ ثُمَّ أَعْطَى الأَعْرَابِيَّ ، وَقَالَ: الأَيْمَنَ فَالأَيْمَنَ"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa maziwa yaliyochangaywa na maji, kulia kwake alikuweko bedui, na kushoto kwake Abu Bakr. (Rasuli) akayanywa, kisha akampa bedui, na akasema: (Mpeni) wa kulia kwanza, kisha anayemfuatia wa kulia”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2352) na Muslim (2029)].
Sahl bin Sa’ad:
"أُتِيَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِقَدَحٍ فَشَرِبَ مِنْهُ، وَعَنْ يَمِينِهِ غُلاَمٌ أَصْغَرُ الْقَوْمِ، وَالأَشْيَاخُ عَنْ يَسَارِهِ فَقَالَ: "يَا غُلاَمُ أَتَأْذَنُ لِي أَنْ أُعْطِيَهُ الأَشْيَاخَ؟ ". قَالَ: مَا كُنْتُ لأُوثِرَ بِفَضْلِي مِنْكَ أَحَدًا يَا رَسُولَ اللَّهِ. فَأَعْطَاهُ إِيَّاهُ"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa gilasi ya maziwa akanywa kidogo. Kuliani kwake alikuweko kijana mdogo kuliko wote waliokuweko, na kushotoni mwake wazee. Akamuuliza (kijana mdogo): Ee kijana! Je, utaniruhusu niwape wazee kwanza? Akajibu: Siwezi kabisa kumpendelea yeyote ufadhilisho wako kwangu ee Rasuli wa Allaah. Rasuli akampa maziwa”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2351) na Muslim (2030)].
8- Anayewanywesha watu awe wa mwisho kunywa
Ni kwa Hadiyth ya Abu Qataadah, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"سَاقِي الْقَوْمِ آخِرُهُمْ شُرْبًا"
“Ahudumiaye watu maji, awe wa mwisho kunywa”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (681)].
9- Kumhimidi Allaah baada ya kumaliza kunywa
Ni kwa neno la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى لَيَرْضَى عنِ العبدِ أَنْ يَشْرَبَ الشَّرْبَةَ فَيَحْمَدَهُ عَلَيْهَا"
“Hakika Allaah Ta’aalaa kwa yakini, Humfurahikia mja anayekunywa mara moja tu (au funda moja tu) akamshukuru Yeye kwa unywaji huo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (2734) na At-Tirmidhiy (1816)].