004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Vivazi Vinavyoruhusiwa Na Vinavyopendeza Zaidi Kuvaliwa Na Wanaume: Kanzu Ndio Vazi Bora Zaidi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ
Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume
004- Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vinavyoruhusiwa Na Vinavyopendeza Zaidi Kuvaliwa Na Wanaume: Kanzu Ndio Vazi Bora Zaidi
Ummu Salamah amesema:
"كَانَ أَحَبُّ الثِّيَابِ إِلَى رَسُوْلِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ القُمُصُ"
“Vazi alilokuwa akilipenda zaidi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kanzu”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1762, 1763), Abu Daawuwd (4025), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (9668), Abu Ya’alaa (7014) na Al-Bayhaqiy (2/239)].
· Suruali Inaruhusiwa Kuvaa
Kuvaa suruali kunaruhusiwa kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote. Na asili ya kuruhusiwa ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ لَمْ يَجِدْ إِزَارًا فَلْيَلْبَسْ سَرَاوِيلَ، وَمَنْ لَمْ يَجِدْ نَعْلَيْنِ فَلْيَلْبَسْ خُفَّيْنِ"
“Asiyepata nguo ya kujifunga chini (izari), basi avae suruali, na asiyepata viatu viwili, basi avae khufu mbili”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1841, 5804), An-Nasaaiy (2672) na Ibn Maajah (2931)].
Suruali inayovaliwa inatakikana iwe pana isiyochora uchi, na kama si pana, basi ni lazima ivaliwe juu yake kanzu ndefu inayositiri uchi. Abu Umaamah amesema:
"قُلْنَا : يَا رَسُوْلَ اللهِ، إِنَّ أَهْلَ الكِتَابِ يَتَسَرْوَلُوْنَ ولاَ يَأْتَزِرُوْنَ، فَقَالَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : "تَسَرْوَلُوْا واتَّزِرُوْا"
“Tulisema: Ee Rasuli wa Allaah! Mayahudi na Manaswara wanavaa suruali na hawavai vikoi (izari). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Vaeni suruali, vaeni vikoi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (5/264) na At-Twabaraaniy (5/121)].
Angalizo:
Baadhi ya ‘Ulamaa wanaoheshimika katika enzi yetu ya leo, wameegemea mrengo wa kusema kuwa kuvaa suruali na kuswalia nayo ni karaha ya uharamu. Sababu wanasema ni kujifananisha na makafiri!! Wamesahau kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshaeleza ni ipi nguo ya kikafiri. Hii ni pale mtu mmoja alipomjia akiwa amevaa nguo ya rangi ya zafarani akamwambia:
"هَذِهِ مِنْ ثِيَابِ الْكُفَّارِ فَلاَ تَلْبَسْهَا"
“Hii ni katika nguo za makafiri, usizivae”. [Hadiyth Swahiyh. Takhriyj yake iko njiani].
Ninasema: “Kuvaa suruali hakuwapambanui tena makafiri kuwa ndio kivazi chao na alama yao mpaka kuharamishwe kwa hoja ya kujifananisha nao. Bali linaloshurutishwa ni hilo tulilolieleza nyuma kidogo kuwa iwe pana isiyochora uchi. Lakini pamoja na hayo, kuacha kuivaa na kuvaa kanzu ni bora zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.