008-Al-Anfaal: Utangulizi Wa Suwrah
008 -Al-Anfaal: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya 'Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 75
Jina La Suwrah: Al-Anfaal
Suwrah imeitwa Al-Anfaal (Mali Inayopatika Vitani), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Faida. Na kutajwa Al-Anfaal (Mali Inayopatika Vitani) katika Aayah namba (1) na (41).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Waumini kuneemeka na Nusra ya Allaah kwao katika Vita vya Badr na kubainisha desturi ya Allaah kuwajaalia ushindi Waislamu na kushambuliwa (kwa makafiri). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Maelezo ya vita vya Badr na maamrisho ya maandalizi ya Jihaad, na kubainisha sababu za ushindi wa vita na baadhi ya hukmu za Jihaad na ugawaji wa ghanima (ngawira inayopatikana baada ya kupigana vita) pamoja na matekwa wa vita.
3-Kubainisha hukmu za mahusiano ya jamii, familia kwa maadili na akhlaaq (tabia) njema.
4-Kumtii Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kubainishwa hukmu za Anfaal (mali inayopatikana katika vita) na ghanima (ngawira inayopatikana baada ya kupigana vita) na uchambuzi wa jinsi ya kuzigawa kwake. Pia maamrisho ya kumcha Allaah kwenye suala hilo na mengineyo, na watu kutakiwa kumtii Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenye jambo la ghanima na mengineyo. Pia kuwaamrisha Waislamu kupatana wao kwa wao, na hilo ndio linakamilisha imaan zao.
2-Waumini wa kweli wamesifiwa na kuwapa bishara ya kuwa watapata daraja na mahali patukufu.
3-Suwrah imetaja jinsi Waislamu walivyotoka kwenda katika Vita vya Badr, na kwamba baadhi yao walichukia jambo hilo, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akalazimisha kwa Hikma Yake Vita hivi, kwa kuwa Alitaka kuthibitisha haki na Abatilishe baatwil. Pia Suwrah imetaja Nusra ya Allaah walioipata Waumini katika Vita hivi. Pia amri ya kujiandaa na vita, na makatazo ya kukimbia vita na watu kugombana na kutofautiana.
4-Suwrah imeelezea yaliyotokea katika Vita vitukufu vya Badr na miujiza ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuteremsha Malaika tele wawasaidie Waislamu na jinsi gani ilivyokuwa ushindi kwa Waislamu juu ya kuwa idadi yako ilikuwa ni ndogo mno kulingana na idadi ya makafiri. Pia miujiza ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwarushia makafiri mchanga. Pia miujiza ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwateremshia Waislamu utulivu juu ya kuwa walikuwa na kiwewe Akawajaalia usingizi mzito mno hadi wakaota usingizini kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawateremshia mvua ya kujitwaharisha, na Akathibitsha miguu yao ardhini.
5-Maelekezo kwa ulingano wa aina mbalimbali kwa Waumini, na kuwaelekeza kwa kila ulingano kwenye jambo maalum lenye kheri na wao, na kufaulu kwao.
6-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amekumbushwa Neema ya Allaah juu yake, pale alipomuokoa na vitimbi vya washirikina wa mji wa Makkah.
7-Suwrah imetaja pia tabia za washirikina ambazo ni ujinga na ukaidi.
8-Imebainishwa kwamba, kuishi kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pale Makkah ilikuwa ni amani kwa washirikina, na alipoondoka ndipo ikaja kuwathibitikia adhabu ya dunia kutokana na yale waliyoyafanya ambayo ni kuwazuia watu na Masjid Al-Haraam.
9-Maamrisho ya kuwalingania washirikina kuwataka waache kuufanyia uadui Uislamu na kuwaudhi Waislamu kwa kuwapiga vita, na kutowa tahadhari juu ya wanafiki.
10-Suwrah imetaja hukmu za ahadi kati ya Waislamu wao kwa wao, na kati ya Waislamu na makafiri, na madhara yanayopatikana kutokana na kuvunja ahadi.
11-Kuna uchambuzi wa ghanima (ngawira inayopatikana baada ya kupigana vita) na kubainisha kuwa mwanzoni mwa Suwrah limetajwa hilo kwa ujumla.
12-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa hukmu ya Waislamu waliohajiri na wakafanya Jihaad katika njia ya Allaah na waliobaki Makkah baada ya Hijrah, na hali ya maisha yao.
Faida:
Suwrah Al-Anfaal imeteremka siku ya Vita vya Badr:
عَنْ سَعِيدِ بْنِ جُبَيْرٍ، قَالَ قُلْتُ لاِبْنِ عَبَّاسٍ سُورَةُ التَّوْبَةِ قَالَ التَّوْبَةُ هِيَ الْفَاضِحَةُ، مَا زَالَتْ تَنْزِلُ وَمِنْهُمْ وَمِنْهُمْ، حَتَّى ظَنُّوا أَنَّهَا لَمْ تُبْقِ أَحَدًا مِنْهُمْ إِلاَّ ذُكِرَ فِيهَا. قَالَ قُلْتُ سُورَةُ الأَنْفَالِ. قَالَ نَزَلَتْ فِي بَدْرٍ. قَالَ قُلْتُ سُورَةُ الْحَشْرِ. قَالَ نَزَلَتْ فِي بَنِي النَّضِيرِ.
Amesimulia Jubayr: Nilimuuliza Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nini Suwrah At-Tawbah? Akasema At-Tawbah ni fedheha (yaani Suwrah inayofichua maovu yote ya makafiri na wanafiki). Na iliendelea kuteremka; Wa minhum, wa minhum (na miongoni mwao, na miongoni mwao), mpaka wakadhani kuwa Suwrah hiyo haikubakisha hata mtu mmoja isipokuwa atakuwa ametajwa humo.” Nikamuuliza: Nini kuhusu Suwrah Al-Anfaal? Akanijibu “Imeteremka kuhusu Badr.” Nikamuuliza: Suwrah Al-Hashr? Akasema “Imeteremka kuhusiana na Bani Nadhiyr.” [Al-Bukhaariy Kitaab At-Tafsiyr]