012-Yuwsuf: Utangulizi Wa Suwrah

 

012-Yuwsuf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 111

 

Jina La Suwrah: Yuwsuf:

 

Suwrah imeitwa Yuwsuf, na inayodalilisha ni kutajwa kwake Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) mara kadhaa katika Suwrah. Na pia kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Fadhila na Faida.    

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Mazingatio kwa upole, wa mipangilio ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa vipenzi vyake, na kuwapa utulivu wao, na kuwapa mwisho mwema. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumpa kiliwazo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba wake na kuwapa utulivu katika nafsi zao.

 

3-Bainisho kwamba njozi njema anayoiona Muumini usingizini ni ya haki, na bainisho kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Hupindua njama za madhalimu, na kwamba Matakwa Yake yanahakiki, na bainisho la Miujiza Yake Allaah (سبحانه وتعالى) katika njia ya kuelezea visa.

 

4-Kuashiria hadhi, heshima na kujisitiri kwa kujiepusha na machafu, na kumcha Allaah kuingia katika makosa yanayomghadhibisha.  

 

5-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah; Muumba Mmoja na kwamba Yeye Ni Pekee Anayepasa kuabudiwa kwa haki.

 

6-Kubainisha kuwa mwisho mwema ni kwa wamchao Allaah, wenye kuvuta subra juu ya mitihani.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetajwa utukufu na sifa ya Qur-aan ya lugha ya Kiarabu na kuanza usimulizi wa kisa cha Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام).

2-Ikatajwa kuhusu njozi ya Yuwsuf (عليه السلام), hila za ndugu zake na husda na chuki zao kwake, na makubaliano yao na mpango wa kutaka kumuua.   

 

3-Imeelezea msafara ulioweza kumtoa Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) kisimani, kisha kuuzwa kwake akafika katika nyumba ya al-aziyz (waziri au mfalme wa Misri) na mitihani aliyoipata ya kutongozwa na mke wake kwenye qasri lake na jinsi habari zilivyoenea.

 

4-Imeelezewa tukio la Yuwsuf (عليه السّلام) kuingia gerezani baada ya kuonekana kuwa hana hatia, na daawah (ulinganiaji) aliyofanya huko.

 

5-Imeelezewa ndoto aliyoiota mfalme na jinsi Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) alivyoifasiri, na kule kuonekana kuwa Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) hakuwa na kosa hali iliyopelekea yeye kutoka gerezani.

 

6-Maelezo ya Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) kukutana na ndugu zake Misri bila wao kumtambua, na kuwataka warudi tena safari ya kufika Misri, pamoja na ndugu yao ambaye ni ndugu shakiki wa Yuwsuf (عليه السّلام). Kisha pale alipomzuia nduguye shakiki, kwa mbinu aliyoipanga kutokana na ilhaam aliyofunuliwa na Allaah (سبحانه وتعالى). Na huzuni ya baba yao baada ya tukio hilo.

 

7-Maelezo ya Yuwsuf (عليه السّلام) alipokutana na ndugu zake kwa mara ya pili, na kule kujitambulisha kwa ndugu zake, na kuwakumbusha juu ya hila walizomfanyia kutaka kumuua, na kwamba yeye amewasamehe. Kisha alipowaagiza kurudi kwa baba yao wakiwa na kanzu yake ili wafikapo, waitupie usoni mwa baba yao, nae akarudi kuona baada ya kupofuka.

 

8-Imeelezea kuhudhuria kwao nyumbani kwa Yuwsuf baada ya matukio hayo, wakiwa na baba yao, na takrima aliyoifanya Yuwsuf juu yao juu ya kuwa nduguze walimfanyia uadui, lakini kwa kuwa Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) alikuwa ni mwenye subra, mwenye moyo wa kusamehe, mwema na mwenye ihsaan alimnasibisha shaytwaan kuwa ndiye aliyewachochea nduguze kumfanyia uadui.

 

9-Duaa ya Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام) ya kuomba kufishwa na Waislamu na kukutanishwa na Swalihina.

 

10-Baada ya kisa cha Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام), Allaah (سبحانه وتعالى) Anamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa si watu wengi watakaoamini japo kama atapania na kutilia hima kuwalingania. Hivyo basi, watu wake; washirikina wa Makkah, wataendelea shirki zao, naye asijali kwani adhabu itawafikia tu ya duniani na Qiyaamah kitawasimamia.

 

11-Amrisho na ukumbusho wa kulingania Dini juu ya nuru za ilimu na utambuzi.

 

12-Allaah (سبحانه وتعالى) Anaendelea kumliwaza Rasuli Wake Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwaambia washirikina kwanini wasiende kutembea katika ardhi wajionee jinsi gani hatima ilikuwa ya madhalimu wa awali? Na kwamba hatima yao ilikuwa ni kuangamizwa! Ama Rusuli Wake,  Aliwateremshia Nusra Yake Akawaokoa na madhalimu.

  

13-Suwrah imekhitimishwa kwa ukumbusho kwamba, katika visa vya Rusuli, kuna mazingatio (na mafunzo) kwa wenye akili. Na kwamba Qur-aan haikuwa hadithi zinazotungwa, lakini ni sadikisho la (Vitabu) vya kabla yake na tafsili ya waziwazi ya kila kitu, na ni mwongozo na rehma kwa watu wanaoamini.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Suwrah Yuwsuf ni Suwrah pekee ambayo imeelezea kwa urefu kisa kamilifu cha Nabiy Yuwsuf (عليه السلام). Hakijatajwa kisa cha Nabiy yeyote katika Qur-aan kwa urefu kama kilivyotajwa kisa hiki cha Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) kwenye Suwrah hii. Na Jina la Yuwsuf limetajwa kwa wingi katika Suwrah hii, na limetajwa mara moja tu katika Suwrah Al-An’aam (7:84) na katika Ghaafir (40:34) bila ya maelezo bayana.

 

2-Rejea Suwrah Yuwsuf (12:4) kupata fadhila za Nabiy huyu mtukufu na kujaaliwa kwake nusu ya ujamali wa dunia.

 

Faida:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، قَالَ كُنْتُ بِحِمْصَ فَقَالَ لِي بَعْضُ الْقَوْمِ اقْرَأْ عَلَيْنَا ‏.‏ فَقَرَأْتُ عَلَيْهِمْ سُورَةَ يُوسُفَ - قَالَ - فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ وَاللَّهِ مَا هَكَذَا أُنْزِلَتْ ‏.‏ قَالَ قُلْتُ وَيْحَكَ وَاللَّهِ لَقَدْ قَرَأْتُهَا عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ لِي ‏ "‏ أَحْسَنْتَ ‏"‏ ‏.‏ فَبَيْنَمَا أَنَا أُكَلِّمُهُ إِذْ وَجَدْتُ مِنْهُ رِيحَ الْخَمْرِ قَالَ فَقُلْتُ أَتَشْرَبُ الْخَمْرَ وَتُكَذِّبُ بِالْكِتَابِ لاَ تَبْرَحُ حَتَّى أَجْلِدَكَ - قَالَ - فَجَلَدْتُهُ الْحَدَّ ‏.‏

Amesimulia ‘Abdullaah (Bin Mas’uwd) (رضي الله عنه): Nilipokuwa Hims, baadhi ya watu walinitaka niwasomee Qur-aan. Nikawasomea Suwrah Yuwsuf. Mtu mmoja kati yao akasema: Wa-Allaahi! Hivyo sivyo ilivyoteremshwa! Nikamwambia: Ole wako! Wa-Allaahi! Nilimsomea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia “Umeisoma vizuri.” Nikawa naongea naye (huyo mtu) nikasikia harufu ya pombe kutoka kwake. Nikamwambia: Je unakunywa pombe na unakadhibisha Kitabu (cha Allaah?).  Hutoondoka mpaka nikupige mijeledi! Basi nikampiga mijeledi kwa mujibu wa adhabu ya Sharia (ya uasi wa kunywa pombe) [Muslim]

 

 

 

Share