014-Ibraahiym: Utangulizi Wa Suwrah
014-Ibraahiym: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 52
Jina La Suwrah: Ibraahiym
Suwrah imeitwa Ibraahiym, na inayodalilisha ni kutajwa kisa chake Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) katika Aayah namba Aayah (35-41). Rejea Faida.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuthibitisha usimamizi wa Rusuli juu ya kubainisha na kubalighisha (daawah) na kuwatishia adhabu wanaopuuza kuwafuata na kuwakadhibisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuthibitisha kwamba Qur-aan ni Kitabu kinachoongoza katika njia iliyonyooka, kwa kumtoa mtu kutoka katika viza na kumuingiza katika nuru.
3-Bainisho kwamba Rusuli wote wametumwa kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah.
4-Kubainisha udanganyifu na ukhaini wa shaytwaan kwa mwanaadam, kwamba Siku ya Qiyaamah, atawakanusha aliowapotosha.
5-Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwathibitisha Waja Wake Waumini duniani na Aakhira kwa al-qawl ath-thaabit (kauli thabiti). Ama madhalimu, wao Allaah (سبحانه وتعالى) Anawapotosha kwa sababu ya kujiepusha kwao na mawaidha Yake, kwa kufuata matamanio yao, na kutajwa adhabu zao Aakhirah.
6-Kukumbusha Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja, na kuwahimiza juu ya kushukuru kwa neema hizo, na tahadhari ya kuzipinga neema na kuzikufuru.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa kwamba Qur-aan ni Kitabu cha hidaaya na ubainifu, na kwamba kinaongoza na kuwahidi watu kutoka katika viza na kuingia katika nuru. Na imebainishwa Ufalme wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa mbingu na ardhi. Na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amewatuma Rusuli kwa lugha za watu wake ili waifahamu Risala Yake.
2-Kimesimuliwa sehemu ya kisa cha Muwsaa (عليه السلام), na neema za Allaah kwa watu wake pale Alipowaokoa kutokana na Firawni. Na kutajwa kwa khabari za baadhi ya Rusuli pamoja na watu wao waliowapinga Risala ya ya Allaah na malipo yao ya adhabu kwa kuwakadhibisha Rusuli wa Allaah.
3-Kuna mahojiano kati ya watu wa motoni; wadhaifu na wale waliofanya kiburi. Na mjadala wa shaytwaan na watu aliowapotosha huko motoni, na kwamba shaytwaan huko Aakhirah, anakana udanganyifu wake na ahadi zake kwa watu waliomfuata.
4-Imetajwa hali za watu wa Jannah na neema za milele.
5-Umepigwa mfano na Allaah (سبحانه وتعالى) wa neno zuri la Tawhiyd, kuwa ni kama mti mzuri. Neno hilo linamaanisha kushuhudia kwamba:
لاَ إِلَه إِلاَّ اللَّه وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُول اللَّه
Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Rasuli Wake.
Rejea Aayah namba (14-15) kwenye maelezo bayana kuwa mti huo ni kama mtende. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anapiga mfano wa neno baya kuwa ni sawa na mti mbaya. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anatofautisha baina ya hayo mawili kwamba: Anawathibitisha wale walioamini kwa al-qawl ath-thaabit katika uhai wa dunia na Aakhirah, na kinyume chake, Anawaacha madhalimu wapotoke. Rejea Aayah namba (27) kwenye maelezo kuhusu maana ya kauli hii inayohusiana na maswali matatu atakayoulizwa mtu kaburini.
6-Suwrah imetaja hali za makafiri ambao walizibadilisha neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na kuzikufuru.
7-Suwrah imetaja pia baadhi ya neema za Allaah za Uumbaji wa ulimwengu na viliomo Akamalizia kusema kuwa Neema Zake haziwezi kuorodheshwa katika hesabu. Rejea Aayah namba (34) kwenye uchambuzi wa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى).
8-Kuna khabari za Nabiy ya Ibraahiym (عليه السلام) na kumwabudu kwake Allaah (سبحانه وتعالى). Na khofu ya dhuria wake kuabudu masanamu. Na kuwaacha dhuria wake katika bonde la Makkah akiwaombea wao na watu rizki na nyoyo zao zielekee kupenda kufika na kuweko huko. Pia shukurani zake kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kumjaalia wana wawili Ismaa’iyl na Is-haaq. Kisha duaa zake kujiombea mwenyewe na dhuria wake kusimamisha Swalaah na kuwaombea Waumini maghfirah. Rejea Aayah namba (41).
9-Suwrah imekhitimishwa kwa Aayah zinazotaja hali za makafiri na madhalimu zitakavyokuwa Siku ya Qiyaamah na aina za adhabu zao.
Faida:
Baadhi ya kisa cha Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kimetajwa katika Suwrah hii pindi alipokuwa Makkah na ahli zake; mkewe Haajar na mwanawe Ismaa’iyl, na kutajwa shukurani zake kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kumruzuku wana wawili ambao ni Ismaa’iyl na Is-haaq, na duaa alizoomba. Rejea tanbihi za Aayah namba (35) na (41).