020-Twaahaa: Utangulizi Wa Suwrah
020-Twaahaa: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 135
Jina La Suwrah: Twaahaa
Suwrah imeitwa Twaahaa, na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1), na herufi hizo ni ambazo zinajulikana kuwa ni Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah zinazotokea katika mwanzo wa baadhi ya Suwrah. Na pia kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila za Suwrah.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuishi maisha mazuri kwa kufuata mwongozo wa Qur-aan, na kuubeba ujumbe wake, na kuishi maisha magumu kwa kwenda kinyume na mwongozo wa Qur-aan. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Utukufu na hadhi ya Qur-aan na kubainisha kwamba Qur-aan ni Risala ya kutoka mbinguni, na haikuteremshwa kwa ajili ya kuwatia watu mashakani, bali Allaah (سبحانه وتعالى) Ameiteremsha kuwa ni mwongozo na uwokovu wa watu, na ni sababu ya kufaulu katika maisha ya duniani na Aakhirah.
3-Ulinzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rusuli Wake Aliowachagua kubeba Risala Yake, wakiwemo wafuasi wao.
4-Maelezo kuhusu baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah, na jazaa ya makafiri kuwa ni adhabu, na jazaa ya Waumini kuwa ni Jannah yenye neema na starehe za kudumu.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imekumbusha Utukufu wa Qur-aan, na kwamba imeteremshwa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba haikuteremshwa kwa ajili kutia mashaka bali ni ukumbusho kwa wenye kukhofu.
2-Suwrah imethibitisha Al-Istiwaa ambayo inamaanisha Allaah Kuweko juu ya ‘Arsh Yake Tukufu kwa namna inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake Yeye Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Aayah namba (5) kwenye maelezo bayana.
3-Imeelezea sehemu kubwa ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السلام). Kisa kikianzia Nabiy Muwsaa (عليه السلام) alipoacha ahli wake akaenda katika bonde tukufu la Twuwaa akaongea na Rabb wake. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamkumbusha Nabiy Muwsaa (عليه السلام), pindi alipozaliwa akatiwa katika sanduku na kutupwa katika mto wa Nile, na jinsi alivyofika nyumbani mwa adui yake Firawni na kulelewa humo. Kisha pale Allaah (سبحانه وتعالى) Alipomtuma Nabiy Muwsaa (عليه السلام) na nduguye Haaruwn (عليه السلام) kwenda kwa Firawni na mazungumzo yao huko. Kisha kusilimu kwa wachawi na chukizo la Firawni kuhusu wao. Kisha kuhusu Saamiriyyu kuwapotosha Bani Israaiyl kumwabudu ndama, wakati Nabiy Muwsaa (عليه السلام) alipoondoka kwenda Miyqaat (sehemu na muda maalumu wa miadi) ya Allaah.
4-Mwanaadam amekumbushwa kwamba ameumbwa kutokana na udongo (ardhini), na kwamba atarudishwa humo ardhini kuzikwa, na kwamba atafufuliwa kutoka humo pia.
5-Imetajwa malipo ya wanaoipuuza Qur-aan, na kutaja sehemu fulani ya matukio ya siku ya Qiyaamah.
6-Limetajwa Jina Tukufu kabisa la Allaah; Al-Hayyu Al-Qayyuwm, rejea Aayah (111) na Al-Baqarah (2:255), Aal-‘Imraan (3:2).
7-Imetaja daraja na utukufu wa Qur-aan, na kwamba imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu, lugha yenye ufasaha wa pekee.
8-Imetajwa kisa cha kuumbwa Aadam (عليه السلام).
9-Kuna maamrisho ya mambo mengi kwa Nabiy (صلى الله عليه وسلم) kama vile: Kuvuta subira, Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa wingi. Kutoangalia sana mapambo ya dunia. Kuwaamrisha watu wake Swalaah.
10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuradd (kupinga) madai ya washirikina, na kuwatisha na mafikio mabaya endapo wataendelea na tabia yao ya kumpinga Rasuli wa Allaah (سبحانه وتعالى) na kudai kuletewa miujiza.
Fadhila Za Suwrah:
Suwrah Twaahaa ni miongoni mwa Suwrah zilizotangulia kuteremshwa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akazitaja kuwa ni pato lake la mwanzo:
حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، قَالَ سَمِعْتُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ يَزِيدَ، سَمِعْتُ ابْنَ مَسْعُودٍ، يَقُولُ فِي بَنِي إِسْرَائِيلَ وَالْكَهْفِ وَمَرْيَمَ وَطَهَ وَالأَنْبِيَاءِ إِنَّهُنَّ مِنَ الْعِتَاقِ الأُوَلِ وَهُنَّ مِنْ تِلاَدِي.
Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Yaziyd (رضي الله عنه): Nimemsikia ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) akisema: Suwrah Bani Israaiyl, Al-Kahf, Maryam, Twaahaa na Al-Anbiyaa ndio miongoni mwa pato langu la kwanza na mali yangu kongwe, na (hakika ni) ndio mali yangu kongwe.” [Al-Bukhaariy]