024-An-Nuwr: Utangulizi Wa Suwrah
024-An-Nuwr: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 64
Jina La Suwrah: An-Nuwr
Suwrah imeitwa An-Nuwr (Mwanga), na inayodalilisha ni kutaja katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Faida. Na pia kutokana na kutajwa katika Aayah namba (35):
اللَّـهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ
“Allaah Ni Nuru ya mbingu na ardhi.”
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuwalingania watu juu ya kujizuia, na kuhifadhi heshima za watu. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kumtakasa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutokana na usingiziaji wa kashfa juu yake. Na hukmu za kuwasingizia machafu wanawake watwaharifu.
3-Kutajwa kwa hukmu ya kujizuia na maasi na yaliyoharamishwa.
4-Hukmu za Hijaab.
5-Kubainishwa maadili mema katika familia na katika jamii ya Kiislamu.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitisha uwajibu wa kufuata Sharia Alizoziteremsha Allaah (سبحانه وتعالى), hukmu na adabu.
2-Kisha ikabainisha hukmu ya zinaa.
3-Imebainisha pia hukmu ya kuwasingizia (zinaa) wanawake wenye kujizuia na maachafu, na hukmu ya kusingiziana (zinaa) kwa wanandoa, na Sharia ya Liaan (kulaaniana).
4-Suwrah imemtakasa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa kuelezewa tukio la ifk (uzushi wa usingiziaji kashfa) na ikawafundisha Waumini adabu kwamba, wanaposikia jambo la uzushi wasiwe wenye pupa ya kuliamini mpaka wapatikane mashahidi wanne.
5-Imeongoza Waumini katika kuendelea kuwafanyia ihsaan wahitaji japokuwa jamaa hao wameingia makosani.
6-Suwrah imetoa mafunzo kwa waliojaaliwa uwezo, waendelee kuwasaidia wahitaji na kuwafanyia ihsaan, hata kama walimkosea mfadhili.
7-Imebainishwa kwamba kauli ovu inaendana na watu waovu, na watu waovu wanaendana na kauli ovu. Na kauli njema inaendana na watu wema, na watu wema wanaendana na kauli njema.
8-Suwrah imetoa maamrisho kwa Waumini wanaume na wanawake, kuwajibika kufumba macho na kuhifadhi tupu. Na pia kuna amri ya hijaab kwa Wanawake Waumini, kwa makatazo ya kuonyesha mapambo yao, isipokuwa kwa wale walioruhusiwa na Allaah (maharim wao).
9-Kuna maamrisho ya kuwaozesha wasio na uwezo wa kuoa na kuolewa.
10-Imeelezea Nuru ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya mbingu na ardhi na imefafanua kwa mifano ya Nuru Yake. Na Nuru hiyo inapatikana Misikitini. Na imebainishwa kwamba Nuru ya Allaah Humfikia Muumin tu!
11-Imetoa mfano wa amali za makafiri kuwa kama ni sarabi (mazigazi), au kama giza ndani ya bahari yenye kina, na kwamba Aakhirah hatakuta malipo yoyote yale.
12-Imebainisha kwamba viumbe vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsabbih Allaah (سبحانه وتعالى).
13-Imebainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa kuumba viumbe, mbingu na ardhi na Neema Zake za kuteremsha mvua.
14-Imetaja kuzibughudhi hali za wanafiki.
15-Imetaja Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waumini ya kuwapa utawala katika ardhi, na kuwaondosha katika khofu.
16-Suwrah imetajwa adabu kadhaa katika jamii na familia. Katika jamii kubisha hodi katika nyumba za watu. Na pia adabu za kula na kuingia majumbani. Adabu za kifamilia kama watoto kupiga hodi vyumbani mwa wazazi katika nyakati kadhaa.
17-Suwrah imekhitimishwa kwa kubainisha sifa za Waumini wa kweli na imewafunza Waumini adabu katika kumwita Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
Faida:
عَنِ الشَّيْبَانِيِّ، سَأَلْتُ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ أَبِي أَوْفَى هَلْ رَجَمَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ نَعَمْ. قُلْتُ قَبْلَ سُورَةِ النُّورِ أَمْ بَعْدُ قَالَ لاَ أَدْرِي.
Amesimulia Ash-Shaybaaniy (رضي الله عنه): Nilimuuliza Abdullaah bin Abiy Awfaa: Je, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitekeleza adhabu ya rajm (kupigwa mawe hadi kufa)? Akajibu: Naam. Nikasema: Kabla ya Suwrah An-Nuwr au baada yake? Akajibu: Sijui. [Al-Bukhaariy]