037-Asw-Swaaffaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

037-Asw-Swaaffaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 182

 

Jina La Suwrah: Asw-Swaaffaat

 

Suwrah imeitwa Asw-Swaaffaat (Safusafu), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1), na pia katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida.   

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumuepusha Allaah (سبحانه وتعالى) na yale waliyomnasibishia washirikina, na kubatilisha madai yao dhidi ya Malaika na majini. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kusimamisha dalili ya Tawhiyd ya Allaah na kwamba kufufuliwa ni haki, na kuelezea baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah.

 

3-Kuelezea kuhusu nyumati za nyuma na upotovu wa ‘Aqiydah zao na ushirikina na hali zao motoni kwa kuwapinga Rusuli wao.

 

4-Kuradd madai na usingiziaji mkubwa wa Maquraysh kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na Viumbe Vyake na kuwataka Waislamu kubakia imara. 

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kuapia Kwake Allaah (سبحانه وتعالى) Malaika wanaojipanga safusafu, wanaosukumiza mbali mawingu, wanaosoma Maneno ya Allaah. Kisha ikathibitishwa Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

2-Imetajwa tabia ya mashaytwaan ya kusikiliza na kuiba habari za mbinguni, na hali yao ya kupigwa na vimondo.

 

3-Imetajwa baadhi ya ada za washirikina ya kufanya istihzai na kutokuamini kufufuliwa.

 

4-Imetajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah, na hali ya washirikina watakapokabiliana kulaumiana walivyofuatana katika upotofu duniani. Hivyo basi watashirikiana katika adhabu kutokana na kibri zao za kukataa haki na kumpachika sifa ovu Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) .

 

5-Imetajwa baadhi ya neema na raha za Jannah (Peponi) kwa Waumini. Na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya kuwasifu Waja Wake waliokhitariwa kwa ikhlasi zao, na kuwatakia Amani juu yao, na kwamba hivyo ndivyo Allaah (سبحانه وتعالى) Anavyowalipa wafanyao ihsaan, imekariri mara kadhaa katika Suwrah pindi anapowataja Waja Wake wema na Manabii Wake.

 

6-Imetajwa mja mwema aliyekuwa Janna (Peponi), akimsemesha rafiki muovu aliyekuwa motoni, akishukuru kwa Rehma ya Allaah kumjaalia kutokumfuata rafiki huyo muovu aliyekuwa haamini kufufuliwa.

 

7-Imetajwa hali za makafiri motoni na watakayoyapata humo kama mti mchungu wa az-zaquwm.

 

8-Ametajwa Nabiy Nuwh (عليه السّلام). Na imetajwa kisa cha Nabiy   Ibraahiym (عليه السّلام) na watu wake waliomuingiza motoni, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akumuokoa. Na pia kisa cha mwanawe Ismaa’iyl (عليه السّلام) na njozi aliyoiona usingizini kwamba anamchinja mwanawe. Ikawa ni jaribio kubwa kwake! Lakini akaiamini njozi hiyo, na wote wawili wakaridhia kuitekeleza. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akawateremshia fidia ya dhabihu (mnyama wa kuchinja), na hiyo ndio Sunnah inayotekelezwa siku ya ‘Iydul-Adhwhaa (‘Iyd ya kuchinja). Kisha wametajwa Nabiy wengineo ambao ni Is-haaq, Muwsaa, Haaruwn, Ilyaas, Luutw, na Yunus (عليهم السّلام).

 

9-Imebainisha ukafiri na dhulma kubwa mno za washirikina kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Malaika ni mabinti Wake ilhali wao wenyewe hawakupenda kuzaa watoto wa kike! Juu ya hayo, wakamsingizia kuwa Ana unasaba na majini! Subhaanahu wa Ta’aalaa! (Ametakasika na kila dosari na Ametukuka kwa Uluwa) Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaradd  kwa hilo na Akawaahidi kuwaadhibu motoni!

 

10-Imetajwa Allaah (سبحانه وتعالى) kuwaunga mkono Rusuli Wake na kuwaahidi nusra, na kumtaka Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwapuuza makafiri na kwamba watakuja kukutana na Adhabu Yake.

 

11-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitisha Nguvu za Allaah (سبحانه وتعالى) Asiyeshindika, na kumtakasa Allaah (سبحانه وتعالى) kutokana na wanayoyavumisha washirikina. Kisha ikatolewa Salaamun (Amani) iwe juu ya Rusuli, na AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu.

 

Faida:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ، قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَأْمُرُ بِالتَّخْفِيفِ وَيَؤُمُّنَا بِالصَّافَّاتِ

Amesimulia ‘Abdullaah Bin ‘Umar (رضي الله عنهما) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiamrisha kufupisha (Swalaah), na alikuwa akituamimisha (Swalaah) kwa (Suwrah) Asw-Swaaffaat (kwa kuwa ni makhsusi kwake). [Swahiyh An-Nasaaiy (825)]

 

 

 

Share