041-Fusw-Swilat: Utangulizi Wa Suwrah
041-Fusw-Swilat: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 54
Jina La Suwrah: Fusw-Swilat
Suwrah imeitwa Fusw-Swilat (Tafsili Ya Wazi), na inayodalilisha ni kutajwa neno hili katika Aayah namba (3).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha hali ya wanaompuuza Allaah (سبحانه وتعالى), na kutaja mwisho wao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuthibitisha kwamba Qur-aan inatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na dalili, ushahidi usiokanushwa wa miujiza ya Qur-aan, na kuthibitisha Risala kwa Mjumbe Wake; Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ni binaadam kuwafikshia wanaadam wenzake na kwamba Dini ya Kiislamu ni haqq.
3-Kusimamisha dalili ya Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake wa kuumba mbingu na ardhi na Aayaat (Ishara na Dalili) Zake.
4-Kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kutajiwa khabari za nyumati zilotangulia waliowakanusha Rusuli wao na upotovu wao duniani na adhabu zao.
5-Kuwabashiria Waumini mema ya duniani na ya Aakhirah.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imebainishwa kwamba Qur-aan ni ya lugha ya Kiarabu, na kwamba ni Kitabu kinachofasili waziwazi Aayah zake, na kwamba zinabashiria na kuonya, lakini wengi ya watu wamekengeuka.
2-Imebainishwa msimamo wa makafiri kuhusu Qur-aan.
3-Imetajwa baadhi ya mambo yanayoonyesha uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) katika Uumbaji Wake.
4-Imetajwa kaumu ya ‘Aad na Thamuwd kuhusu kibri zao na ukanushaji wao wa Risala ya Allaah na ikatajwa adhabu zao.
5-Imeonya washirikina wanaopinga kuisikiliza Qur-aan, ya kwamba yatawapata yaliyo wapata waliopita kabla yao.
6-Imebainishwa hali za Waumini wanapotolewa roho zao kubashiriwa kheri.
7-Imetajwa sifa za mwenye kulingania (daawah) awe mnyenyekevu na mwenye kulipiza uovu kwa wema na kuvuta subira.
8-Imetajwa Aayah (Ishara, dalili) kadhaa zinazoonyesha Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake juu ya kuwafufua wafu. Na katika hizo ni usiku na mchana, jua na mwezi na ikaamrishwa kutokusujudia hivyo bali asujudiwe Allaah (سبحانه وتعالى) Ambaye Ameviumba hivyo. Na hapo inapaswa mtu asujudu kwa kuweko alama ya Sijdah ya tilaawah (kusoma).
9-Ameliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya maudhi anayoyapata kutoka kwa watu wake.
10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuahidiwa makafiri kuwa wataonyeshwa Aayaat (Ishara na Dalili) za wazi katika nafsi zao na angani mpaka iwabainikie kwamba hii (Qur-aan) ni haki, na kwamba makafiri wako katika shaka ya kufufuliwa na kuhesabiwa.