049-Al-Hujuraat: Utangulizi Wa Suwrah
049-Al-Hujuraat: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 18
Jina La Suwrah: Al-Hujuraat
Suwrah imeitwa Al-Hujuraat (Vyumba), na inayodalilisha ni kutajwa neno katika Aayah namba (4).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuutibu ulimi, na kubainisha athari yake katika imaan ya mtu mmoja mmoja na katika jamii. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuwaongoza Waumini katika tabia njema mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waumini wao kwa wao, na kuiweka jamii katika usalama na amani.
3-Kubainisha kwamba ukabila hauna thamani mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kuwa na taqwa.
4-Kubainisha imaan ya uhakika.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kuwaelimisha Waumini miongoni mwa akhlaaq na adabu zinazowajibika kwao kwa Muumba wao na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Nazo ni kutokuamua jambo la Sharia ya Dini kinyume na Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Kutokumpandishia sauti Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wanapoongea wenyewe, au wanapoongea naye. Kutokumuingilia nyumbani kwake bila ya idhini.
2-Waumini wameamrishwa kuchunguza kwanza na kuthibitisha usahihi wa khabari zinazowafikia kabla ya kuhukumu na kuchukua hatua ya jambo.
3-Imebainisha baadhi ya Fadhila za Allaah kwa Waumini.
4-Imeongoza Waumini lipasalo kufanywa pindi yanapotokea mapigano kati ya makundi mawili ya Kiislamu, na katika kusuluhisha baina yao, na kulipiga vita kundi linalochupa mipaka pindi linapoendelea katika uovu wake na kukataa suluhu, mpaka lirudi katika Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى).
5-Imewakataza Waumini kufanyiana kejeli, na kuitana majina maovu, na kuwaamrisha kujiepusha kuwadhania wengine dhana mbaya, na kuwakataza kuchunguzana, na ghiybah (kusengenya).
6-Imetoa wito kwa watu kwamba, wao wote wameumbwa kutokana na mume na mke, na kwamba mbora wao na mtukufu zaidi mbele ya Allaah ni yule mwenye taqwa.
7-Imewajibu mabedui waliodai kuwa wameamini pasi na kutulizana imaan katika nyoyo zao, na kuziweka wazi sifa za Waumini wa kweli.
8-Imekatazwa kujifakharisha mbele ya Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa imaan, na kwamba Neema ni za Allaah (سبحانه وتعالى), na fadhila katika kuongoza (watu) kwenye imaan.
9-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa Ilimu ya Allaah iliyozunguka yaliyofichika mbinguni na aridhini, na kwamba Allaah ni Mwenye kuona yote yatendwayo.