064-At-Taghaabun: Utangulizi Wa Suwrah

 

064-At-Taghaabun: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 18

 

Jina La Suwrah: At-Taghaabun

 

Suwrah imeitwa At-Taghaabun (Kupata na Kukosa), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (9).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kutahadharisha mambo yanayosababisha watu kupata majuto na kunyimwa kheri Siku ya Qiyaamah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha uhalisia wa kupunjana na sababu zake pamoja na mwisho wake, kama inavyoongoza Suwrah hii katika njia ya kupata na kukosa au kufuzu na kufaulu.

 

3-Kutahadharishwa yanayomzuia mtu kutoa mali katika Njia ya Allaah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitishwa kwamba vyote vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsabbih Allaah, na kwamba Yeye Pekee Mwenye Kustahiki kuhimidiwa na Mweza wa kila kitu.  

 

2-Imebainishwa aina mbali mbali za Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na upana wa Ilimu Yake, na imethibitisha Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola; Uumbaji, Uongozaji, Utoaji Rizki, Uendeshaji na kadhaalika)

 

3-Imewaonya washirikina kwa kuwakumbusha yale yaliyowapata nyumati zilizopita kabla yao, pamoja na kubainisha ada zao za kuwakanusha Rusuli na kuwafanyia istihzai.

 

4-Imewaradd washirikina kwa madai yao ya kutokuamini kufufuliwa na Allaah Akawathibitishia kwa kiapo kuwa, bila shaka watafufuliwa na kwamba Siku hiyo Allaah Atawakusanya viumbe vyote na itakuwa ni Siku ya At-Taghaabun (kupata na kukosa, kufaulu na kukhasirika).

 

5-Imeainisha kati ya Waumini na mwisho wao mwema, na makafiri na mwisho wao mbaya.

 

6-Imebainishwa kwamba misiba yoyote ile inayowasibu watu ni kwa Qadar ya Allaah.

 

7-Waumini wamehimizwa kumtii Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

8-Imethibitishwa Tawhiyd Al-Uwuluwhiyyah (Kumwabudu Allaah Pekee).

 

9-Imeelezwa kwamba miongoni mwa wake na watoto ni maadui kwa mtu, na kwamba mali na watoto ni mitihani, hivyo basi wamehimizwa Waumini kumcha Allaah na kumtii, na kutoa mali katika Njia ya Allaah.

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kukumbushwa Waumini, kwamba mali yoyote waitoayo ni mkopo mzuri kwa Allaah, na kwamba Atawazidishia malipo maradufu, na Atawaghufuria, na Yeye ni Mwenye Kupokea Shukurani zao, na zikatajwa Sifa Zake Allaah (سبحانه وتعالى) nyenginezo ikiwemo Sifa ya Mjuzi wa yaliyo ghaibu na yaliyo dhahiri. 

 

 

 

 

 

Share