071-Nuwh: Utangulizi Wa Suwrah
071-Nuwh: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 28
Jina La Suwrah: Nuwh
Suwrah imeitwa Nuwh (عليه السّلام) na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha njia ya kufanya da’wah kwa maduaati (walinganiaji). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kupiga mfano kwa washirikina kupitia watu wa Nuwh, na wao ndio washirikina wa mwanzo ardhini.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitishwa kutumwa Nuwh (عليه السّلام) kwa watu wake awaonye Adhabu za Allaah.
2-Ikafuatia uslubu ya Rusuli katika da’wah; kuanza kuwalingania watu katika Tawhiyd ya Allaah. Zikatajwa baadhi ya ada za washirikina kukanusha Risala ya Allaah, na ikatajwa jinsi Nuwh (عليه السّلام) alivomlalamikia Rabb wake kuhusu watu wake.
3-Akaendelea Nuwh (عليه السّلام) kuwanasihi watu wake kwa kuwapa matarajio na kuwakhofisha, na kuwatajia Rehma za Allaah Kuwaghufuria madhambi yao, na kuwatajia fadhila za istighfaar (kuomba maghfirah), na kuwakumbusha kuumbwa kwao, na kuwataka wazingatie Neema za Allaah juu yao za uanzilishi wa Uumbaji wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa mbingu na ardhi na yaliyomo, na kuwakumbusha Siku ya kufufuliwa.
4-Imetajwa msimamo wa watu wa Nuwh (عليه السّلام) na inadi zao za kuwahimiza makafiri wenzao waendelee kuyaabudu masanamu yao kwa kuwatajia majina yao. Wakaendelea katika maasi na ushirikina, na ikatajwa adhabu zao duniani kwa kugharikishwa na Aakhirah kuingizwa motoni.
5-Yametajwa maombi ya Nuwh (عليه السلام) kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Awang’oe makafiri ardhini asibakie kafiri yoyote.
6-Suwrah imekhitimishwa kwa Nuwh (عليه السلام) kuomba maghfirah yeye na wazazi wake na Waumini, na kuwaombea madhalimu wateketezwe.